SIRI ILIYOJIFICHA YA UDHALILISHAJI KATIKA USAFIRI WA UMMA (BODABODA NA DALADALA.
HABIBA ZARALI PEMBA Katika mitaa ya Zanzibar na maeneo mengine ya mijini, bodaboda na daladala zimekuwa uti wa mgongo wa usafiri wa kila siku. Ni vyombo vinavyorahisisha maisha, vinavyounganisha watu na shughuli zao za kiuchumi, elimu na kijamii. Hata hivyo, nyuma ya urahisi huo wa usafiri, kuna simulizi zinazoumiza za udhalilishaji, unyanyasaji wa kijinsia, na vitendo vinavyotishia utu wa baadhi ya abiria, hususan wanawake, wasichana na wakati mwingine watoto. Wahanga wengi wamekuwa wakibeba maumivu haya kimya kimya, hofu ya kuaibika, kutoaminiwa au kukosa ushahidi wa moja kwa moja imewafanya wengi wasiripoti matukio wanayokumbana nayo. Katika uchunguzi wa makala haya, umebaini hali hiyo imejenga mazingira ambayo udhalilishaji unaendelea kujificha ndani ya mifumo ya kawaida ya usafiri wa umma hali inayoendelea kuathiri jamii kimya kimya. SAUTI ZA WAHANGA Saa kumi na moja jioni, Asha mkaazi wa Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba (siyo Jina lake halisi) alikuwa akirejea nyumba...