PACSO YATETA NA WANANCHI KOJANI

MTANDAO wa Asasi za kiraia wa Pemba (PACSO) umeandaa mkutano maalumu kwa wananchi wa Kisiwa kidogo cha Kojani wenye lengo la kuiwezesha jamii kupata uwelewa mpana juu ya masuala ya kisheria na haki za binaadamu.

Mkutano huo uliowashirikisha wananchi wa Kisiwa cha Kojani umeandaliwa na jumuiya PACSO kwa ufadhili wa shirika la UNDP na kufanyika huko ukumbi wa skuli ya msingi Kisiwani humo.

Akizungumza na wananchi Mkurugenzi Mkuu wa PACSO Pemba Mohamed Najim Omar katika mkutano huo alisema, mpango huo una lengo la kuiwezesha jamii kupata ufahamu wa kisheria na haki za binaadamu.

"Jamii zetu bado zina changamoto nyingi na baada ya kuliona hili tumeamua kuandaa mpango wa kupita kwenye jamii kutoa taaluma ya kuwawezesha watu ufahamu juu mambo haya, elimu zinatolewa nyingi lakini na sisi pia tumeona kuja haja ya kuwafikia", alisema. 

Aidha alisema, kutokana na kujitokeza masuala mbali mbali ya unyanyasaji wa kijinsia, watoto kudhalilishwa, wanawake, watu wenye ulemavu na hata wazee ndani ya jamii zao ndio PACSO ikaamua kuandaa mpango wa kupita kwa jamii kutoa taaluma hiyo itakayowasaidia wananchi.

Kwa upande wake, Mratibu wa mradi wa UNDP Gamaliel Sunu aliwashukuru PACSO kwa kuendelea kuyafikia makundi mbali mbali ya kijamii kuwapatia elimu hiyo huku akiahidi kuendelea kushirikiana nao kuhakisha makundi yote yanafikiwa.

Akiwasilisha mada ya sheria na sera inayohusu wazee katika mafunzo hayo Afisa ustawi wa jamii Pemba Salim Juma Mbarouk alisema, lengo la sheria hiyo ni kulinda haki za wazee, kuweka mfumo wa huduma na ulinzi kwa wazee na kupata huduma zao za msingi.

"Kuna haki ya wazee ya kuheshimiwa na kutokubaguliwa, kupatiwa huduma za afya, kutokufanyiwa unyanyasaji wa aina yoyote, kutokufanyiwa ukatili, kuwalinda wazee, kuwapatia mahitaji yao ya msingi ikiwemo mavazi, chakula na matibabu bora", alisema. 

Akiwasilisha mada ya sheria na sera ya vijana Zanzibar Afisa kutoka Ustawi wa jamii Nuwairat Yussuf Salim alisema, madhumuni ya sheria hiyo ni serikali kuwa na lengo la kuongoza maendeleo ya vijana kupitia sekta mbali mbali ikiwemo kuwajengea uwezo katika stadi za maisha.

Mapema, sheha wa Kojani Omar Ali aliipongeza PACSO kwa kuwapatia elimu ya kisheria wananchi wa Kojani huku akiwataka wananchi ambao wamepatiwa taaluma hiyo wakawe mabalozi wazuri wa kuifikisha elimu hiyo kwa wengine ambao hawakupata fursa ya kushiriki mkutano huo.

                           MWISHO.

Comments

Popular posts from this blog

Masheha wanawake wa Wilaya ya Magharib B walivyoleta mabadiliko na maendeleo kwenye shehia zao.

UHABA WA VITUO VYA POLISI WILAYA YA CHAKE CHAKE BADO MLIMA MREFU KUDHIBITI UHALIFU VITENDO VYA UDHALILISHAJI NA UVUNJIFU WA HAKI ZA BINAADAMU.

MPANG0 MKAKATI JUMUISHI WA JINSIA KATIKA MICHEZO UTEKELEZAJI WAKE UZINGATIWE.