UHABA WA VITUO VYA POLISI WILAYA YA CHAKE CHAKE BADO MLIMA MREFU KUDHIBITI UHALIFU VITENDO VYA UDHALILISHAJI NA UVUNJIFU WA HAKI ZA BINAADAMU.
- Get link
- X
- Other Apps
NA AMINA AHMED MOH’D - PEMBA
CHAKE Chake ni moja kati ya wilaya mbilizi zinazopatikana katika Mkoa wa Kusini Pemba Zanzibar Tanzania.
Ambayo kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012 ina idadi ya wakaazi 97,249 na anuani za makazi zikiwa ni 74200
Idadi Mpya ya wakaazi wa Chake Chake kwa takwimu za Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 iliyotolewa hivi karibuni bado hazijapokelewa katika ngazi za wilaya ni kutokana na takwimu hizo kuikiishia katika ngazi za Mikoa pekee jambo ambalo limewia ugumu kupatikana idadi mpya ya wakazi wake wa sasa.
Chake Chake ina jumla ya shehia 32 ambazo wakaazi wake hulazimika kutumia kituo kimoja pekee cha polisi katika kuripoti matukio mbali mbali.
Matukio hayo ni pamoja uhalifu, udhalilishaji wa kijinsia wazee wanawake na watoto, wizi wa mazao , mifugo, Pamoja na Ajali za Barabarani .
Akina mama na watoto hukwazika zaidi kukifikia kituo hicho bila kujua hatima na ufumbuzi wa suala hilo utakuwa lini .
Baadhi ya wakaazi wa chake chake wanasema kuwa matumaini yao ni kusogezewa kwa karibu vituo vya polisi katika shehia zao ili kuondokana na usumbufu.
" Tuna matumani na serikali pamoja na watu wenye uwezo kutusaidia kutuongezea vituo vya polisi wilayani kwetu na kwa vile tukionana na viongozi wahusika akiwemo mkuu wa wilaya tunalalamika sana suala hili.
Ni maneno ya " Pascal Mkuba mwanaharakati wa dini juu ya kupinga udhalilishaji wa kijinsia Gombani Chake Chake.
" Tupo tayari kujitolea nguvu zetu , tushike pauro tubebe mabero yaani uwezo wa kujenga hatuna lakini uwezo kujitolea nguvu kusaidia tuko tayari ". Akaongeza pascal Mkuba
"Kituo kimoja pekee kinarudisha nyuma mapambano dhidi ya udhalilishaji na Matukio mengi huishia njiani kutokana umbali wakufata kituo kwajili ya kuripoti matukio.
Watu hufanya suluhu na kuishia majumbani baadhi ya kesi za udhalilishaji zinapojitokeza hawaendi vituoni wanahofia umbali lakini vingekuwa vipo karibu matukio yakitokea yanaripotiwa tu kama sehemu nyengine.
Saivi mtoto wa miaka 16 kakatishwa masomo kesi haijenda popote anaolewa siku mbili anarudishwa kwao haki yake ya kusoma kaikosa ,
Akaendelea "kwa mume hajakaa na kawa mkosaji hana pakudai haki walau akarudishwa skuli yupo tu " .
Ni Maneno ya Saumu Ali mkaazi wa Ole .
" Watoto hawatuogopi tena unamkataza kitu hichi kibaya anafanya hicho hicho ukiona kawa msugu anapelekwa polisi ijapo kutishiwa inakuwa dawa anaogopa
Lakini ngumu tunawaacha tu mana mpka ukifunga safari kuenda uko kituoni si leo kesho na kesho kutwa wamekuwa wizi kwa vile wamekosa miongozo mapema.
Tunaibiwa mifugo yetu inachinjwa usiku huko huko tulikoilaza mtu ata akipiga kelele muibaji anaacha kisu na mapolo apo apo anakimbia
Tusubiri asubuhi tuende Kutoa tarifa polisi mana uwezo wa kuenda kwa miguu kutoa taarifa hatuna kituo mpka uende Chake mjini ".
" Tunamuomba Dokta Mwinyi atusaidie kutuondolea usumbufu tunaoupata sisi akina mama mifugo yetu inaibiwa
Tunakosa haki zetu kutokana na kushindwa kufikia kwa wakati sahihi vituoni kutoa taarifa za kuibiwa".
"Binafsi mwaka huu nimeibiwa Ng'ombe wangu akachinjwa lakini kesi nikaenda polisi siku moja zilizobakia sijaenda kufuatilia mpka kesho.
Inabaki kumbukumbu tu nilichoka kwenda na kurudi kila siku Nimerudia nyuma kimaendeleo " .
Ni maneno ya bi Asha Bakari Juma mkaazi Wa Kijiji Cha Simaongwe Shehia ya Mjini Ole wilaya ya Chake Chake.
"Haki za binaadamu hazipo zinakosekana kabisa kuna nyakati tumekuwa tukiogopa hata kukatisha njia na watoto
Vurugu za vyombo vya miguu miwili nyakati za jioni na usiku wale hawana kofia ngumu, wale wanaendesha wanavyojua" .
"kwa sababu hakuna polisi imekuwa vijana wanapoteza nguvu kazi na kupoteza maisha huku kwetu zaidi,
kungekuwepo na kituo hakuna kijana angeendesha chombo ovyo akapita mbele ya kituo anajua atachukuliwa hatua lakini hakuna anafanya anavyojiskia ".
" Serikali tunaomba itusaidie kuwekwe kituo na sehemu nyengine zenye barabara za ndani vijana wanapoteza maisha kizembe .
"Mkasi Haji Mkaazi wa Wesha.
Mzee Hassan Yakoub alisema kuwa Baadhi ya vijana wasiopenda amani wamekuwa wakiutumia mwanya huo kufanya vitendo vya uhalifu .
"Tunaomba Tusogezewe karibu vituo vya polisi Sababu vitendo vya uhalifu vinavunja amani na watu hujichukulia sheria mikononi mwao kwa vile vyombo vya sheria havipo karibu yao". Alidai Mzee huyo mkaazi wa Ole
"Mbuzini ndio shehia ambayo ina lango kuu la kuingilia na kutokea chake chake hapa ndio kuna umuhimu mkubwa wa kuwepo kituo cha polisi lakini hakipo.
kudhibiti uhalifu Tunaiomba serikali na wahisani itusaidie suala hili tunataka chake chake ambayo haina uhalifu".
Hemed Abeid Hemed Sheha wa shehia ya Mbuzini Wilaya ya Chake Chake.
SHEHIA AMBAYO IPO KARIBU SANA NA KITUO CHA POLISI INASEMAJE.
Mafunda hamad Rubea Sheha wa shehia ya Madungu anasema Matukio mengi ya kiuhalifu yanayoripitiwa kwake yamekuwa na urahisi kufikishwa kituoni kutokana na kuwa karibu na kituo.
"Kesi za udhalilishaji zinaporipotiwa kwangu dakika tumezifikisha kituoni ufuatiliaji unaanza zinapelekwa mahakamani hazina nenda uje ambayo itawasumbua wananchi wangu
Mtu anamudu kuenda kituoni hata kwa miguu ni jambo la kujivunia kuwa karibu na kituo, lakini hata uhalifu sio mara nyingi kuskia kumeibiwa nguo mara mifugo mazao tunajivunia ilo ubalifu ni mchache ".
Wakaazi wilaya ya Chake Chake wanazidi kuongezeka katika maeneo ya miji na vijiji na hii inasababishwa ni kutokana na kuwepo mji mkuu wa kibiashara ambapo wannanchi wengi kutoka nje ya wilaya hiyo hulazimika kufuata mahitaji mengi katika mji huo.
Ofisi Ya Mkurugenzi wa Mashtaka Mkoa wa kusini Pemba mkoa ambao umeundwa kuputia wilaya mbili Mkoani na Chake Chake inasema inapokea kesi nyingi zaidi za makosa na vitendo mbali mbali vya uhalifu h kutoka wilaya ya Chake Kuliko wilaya ya Mkoani.
"Wilaya ya hake tunapokea kesi nyingi zaidi kuliko Wilaya ya Mkoani na zinatokea kesi na jalada linaletwa Ofisini lakini kutokana na ushahidi kuwa dhaifu tunaelekeza kufungwa.
kutokana na kukosa ushahidi zipo kesi ambazo watu walifunguwa na kushindwa kurudi tena kufuatilia Zipo kesi ambazo aliefanya kosa hajulikani alieripoti kaja siku moja tu harudi tena".
"Sababu zinaweza kuwa nyingi zinazopelekea tofauti hiyo kiwilaya kwanza Wilaya ya Chake ina idadi kubwa ya watu kuliko mkoani.
lakini Wilaya ya chake ni wilaya yenye mji mkubwa kuliko mkoani, na wilaya zote ambazo zina miji makosa ni mengi kuliko ambazo hazina mijini kifupi mjini makosa ni mengi na wahalifu ni wengi".
jengine wilaya ya Chake ina upungufu wa vituo vya Polisi, kipo kimoja tu tofauti na wilaya ya Mkoani yenye vituo vitatu vya Polisi Pia inapelekea kupungua kwa makosa endapo vituo vikiwa karibu na wahalifu kwani huingiwa na hofu.
Lakini pia Jamii zinazoishi wilaya ya Mkoani wanaishi kijamii kwa maana wengi ni ndugu tofauti na Wilaya ya Chake yenye wahamiaji wengi".
ni maneno ya Wakili wa Serikali kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Pemba Ali Amour Makame
Jeshi la Polisi linadai kutokana na changamoto hiyo hulazimika kutumia askari wakaguzi ambao wamekuwa mbadala wa kuimarisha ulinzi na usalama katika shehia ambazo zipo mbali na kituo hicho cha Polisi.
" Tunao maafisa wakaguzi ambao tumewaweka maalum katika kila shehia kuona kwamba wanaimarisha na kutoa mashirikiano juu ya kutatua changamoto mbali mbali katika kuimarisha ulinzi"
" Changamoto iliyopo kwa sasa bado tuna uhaba wa askari hao na tunashughulikia kuona kwamba wanatosheleza bado askari mmoja hulazimika kusimamia shehia zaidi ya tatu".
" Kuhusu Suala la vituo ni jambo la Jamii husika watakapoona kuna ulazima wa kuwepo Jeshi halitosita kupeleka askari vituoni humo.
Hivyo ni jambo la kukaa na kujadilina uongozi wa wilaya kuona namna gani wanafanikisha hilo sababu jukumu letu ni kuimarisha ulinzi na usalama na askari wetu wapo tayari".
Maneno kutoka kwa Kamishna Wa Polisi Zanzibar Hamad Khamis Hamad.
UNGOZI WA WILAYA UNASEMAJE.
Masheha waliowengi mara kwa mara katika vikao vyetu wamekuwa wakiligusia suala hili na sisi uongozi tayari tumeanza kulijadili katika vikao vya mkoa kuona vipi tutalipatia ufumbuzi suala hili.
kutokana na ukuaji wa miji, na ongezeko la idadi ya watu kwa wilaya yetu ya chake chake sasa ivi bado tuna kituo kimoja tu cha polisi
"Miji yetu inakuwa zaidi, watu wanaongezeka, harakati za kiuchumi za kijamii pia zinakua, ni kiri kuwa kituo hichi hakitoshelezi hivyo ni wazi kuwa ipo haja ya kuongeza vituo hivyo ili kudhibiti zaidi usalama zaidi.
"Bado uongozi wa wilaya mpaka sasa haujafanikisha suala hilo la ujenzi wa vituo vyengine vya polisi katika maeneo mbali mbali ya mji wa Chake Chake.
Tumebahatika kupata barabara kubwa hii ya ole kengeja ambayo imekuwa na tija kubwa na wananchi wameanza kuvutika kuanza kuishi katika ukanda wa barabara.
Lakini bado utakuta ole mpka kufika kengeja bado hakuna kituo cha Polisi ni maeneo muhimu ambayo pia yana umuhimu na ulazima wa kuwepo na kituo".
"Serikali ya wilaya tayari imetenga maeneo maalum ambayo itakuwa tayari kuyatumia kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya Polisi katika wilaya hiyo endapo serikali kuu itaridhia na wadau watajitokeza kujenga vituo hivyo katika wilaya ya chake chake.
Aidha amesema uongozi wa Wilaya unaendelea kuzungumza na wadau na wazalendo wa nchi ili kupata msaada wa kujengewa vituo vya polisi katika badhi ya maeneo muhumu na yenye ulazima wa kuwepo vituo vya polisi katika wilaya hiyo.
" Chake ina zaidi ya bandari zisizo rasmi 88 ambazo wahalifu huzitumia jeshi la Polisi linaendelea kudhibiti na kukamata wanaotumia maeneo hayo lakini shida ni kukosekana kituo maeneo yakaribu na bandari hizo. "
"Wezetu wilaya ya Mkoani wana vituo vingi hata kasi yao ya kudhibiti vitendo vya kihalifu inaongezeka maeneo yao ya bandari kuna kituo, Kengeja, Mtambile na mote humo ukaguzi unakuwa unafanyika.
na kunazuilika uhalifu unapotokezea kwa upande wa mashariki kituo kipo karibu magharibi lakini pia center ya mji kipo kituo karibu,kadhalika wete na micheweni Alisema".
" Kituo kipo Mjini lakini kuna maeneo ambayo ufikiaji wake ni mgumu kwa mfano Mgelema, kilindi Ndagoni ni mbali na yote ni maeneo ambayo kuna bahari, kote huko kwa umuhimu wake kunastahiki kabisa kuwa na vituo vya polisi.
Abdalla Rashid aliwataka wananchi kutosita kuisadia Serikali na jeshi la Polisi kudhibiti vitendo vya kihalifu endapo watabaini kuwepo kwa vitendo viovu katika jamii zao kwa kutoa taarifa.
" Tuko Tayari kutoa mashirikiano kwa yeyote atakaekuwa tayari kusaidia suala hili la ujenzi wa vituo vya polisi katika wilaya yangu.
Wadau wa kupinga udhalilishaji, kulinda haki za binaadamu watu binafsi kikundi cha watu taasisi za fedha na wasamaria wema wajitokeze kufanikisha kupunguza changamoto hii lengo ni kuona tunaendeleza mapambano ya kudhibiti uhalifu wa aina mbali mbali. "
Wilaya ya Chake Chake ina shehi 32 Ambazo ni Shehia ya Wara, Kichungwani, Chanjaani, Matale, Kilindi, Kibokoni, Uwandani, Ng'ambwa, Wawi, Mchanga Mrima, Ndagoni, Wesha, Birikau, Madungu, Shungi, Msingini, Chachani, Mgelema, Tibirinzi, Kwale, Michungwani, Gombani, Vitongoji, Mfikiwa, Mgogoni, Ole, Mjini ole, Mbuzini, Mvumoni, Pujini, Chonga Pamoja na Chanjamjawiri
Shehia zote hizo zimekuwa zikiendelea kuishi kwa wasi wasi endapo vitajitokeza vitendo vya kihalifu nyakati za usiku ambapo Wananchi wengi wanaoishi katika baadhi y vijiji vilivyomo ndani shehia hizo hushindwa kuripoti matukio ya kiuhalifu huku wengine kuripoti matukio mara moja bila kuyafuatilia sababu ikiwa ni umbali wa vituo vya Polisi.
Suala hili hupelekea kukosa haki zao muhimu huku watoto vijana na wanawake wakiendelea kukosa haki zao muhimu kutikana na kufanyiwa vitendo vya kikatili ikiwemo udhalilishaji jambo ambalo hupelekea kuvunjwa sheria mbali mbali ya usalama wao Huku shehia moja ya Madungu ikibakia kuwa Salama Juu ya mapamabo dhidi ya uhalifu.
Waswahili wanasema "Usipoziba Ufa Utajenga Ukuta " Wakiwa na maana ya tahadahari ya mapema juu ya kudhibiti Tatizo dogo kuwa kubwa hivyo natamani kabla hakujatokea maafa kutokqna na upungufu huu Ufa huu uonekane katika kuendeleza mapambano ya kutunza na kulinda haki za binaadamu.
Huku wengine wakisema kuwa " Kinga ni bora kuliko tiba" na kumalizia kwa kusema usipoziba ufa utajenga ukuta. yote haya huenda yakaja kuleta madhara endapo suala hili halitochukuliwa hatua.
Mwisho.
- Get link
- X
- Other Apps
kweli kabisa Mwandishi kuna umuhimu ili suala
ReplyDelete