KUVUNJIKA KWA NDOA NA HATARI ZA WATOTO WA
KIKE KUKATISHA NDOTO ZAO
Na HABIBA ZARALI PEMBA
NDOTO za watoto wengi wa kike huanza kujengwa tangu
wakiwa wadogo.
Wengine hutamani kuwa madaktari, walimu, wanasheria
au wataalamu watakaosaidia familia zao na taifa kwa ujumla.
Hata hivyo, kwa baadhi ya watoto wa kike, ndoto hizo
zimekuwa zikififia na hatimaye kutoweka kutokana na changamoto zinazotokana na
kuvunjika kwa ndoa za wazazi wao.
Ingawa talaka huonekana kuwa mwisho wa uhusiano wa wanandoa,
ukweli ni kwamba athari zake huendelea kuonekana kwa muda mrefu katika maisha
ya watoto.
Watoto wa kike ndio huonekana kubeba mzigo mkubwa zaidi,
wakikabiliwa na hatari ya kuacha shule, kuozeshwa mapema, kukosa malezi bora au
kushindwa kufikia ndoto walizojijengea tangu utotoni.
Katika Mkoa wa Kaskazini Pemba Wilaya ya Micheweni na
maeneo mengine, simulizi za watoto wa kike walioathirika zinaonesha namna
migogoro ya kifamilia inavyoweza kubadili kabisa mwelekeo wa maisha yao.
Pamoja na Hali hiyo kuwepo lakini inaonekana
kujificha na kuumiza polepole bila ya kujulikana kiurahisi huku maumivu na
athari ya watoto wa kike ikiendelea.
Fatma Ali Juma (16) wa Micheweni alikuwa na ndoto ya
kuwa daktari, tangu akiwa mdogo alipenda masomo ya sayansi na aliamini siku
moja angevaa koti jeupe na kuwahudumia wagonjwa hospitalini.
Hata hivyo, baada ya wazazi wake kuachana, hali ya maisha
ilibadilika, changamoto za malezi na ukosefu wa mazingira mazuri ya kuendelea
na masomo zilianza kujitokeza na kuathiri safari yake ya elimu.
Ndoto yake ya kuwa daktari ikaanza kufifia taratibu
na kujiona kabakia tu bila muelekeo wowote
ule kwani hakuna mzazi yoyote aliemshughulikia maendeleo yake ya elimu
na badala yake ilikuwa ni uhasama dhidi yao.
“Mimi licha ya hamu kubwa niliyokuwa nayo ya kusoma hadi
kufikia udaktari ilikufa baada ya wazazi wangu kuachana alisema kwa huzuni.
Shufaa Said Faki wa Micheweni, ndoto yake ilikuwa ni
kuwa mwalimu, alitamani kusimama mbele ya darasa na kuwafundisha watoto ili
kuwasaidia kufikia mafanikio yao.
Lakini baada ya wazazi wake kuachana na kukosekana kwa
mawasiliano mazuri kati yao, maisha yake yalibadilika,Katika mazingira hayo,
Shufaa aliozeshwa akiwa bado mdogo kabla hajamaliza masomo yake.
“Ndoa yangu ya mapema ilikatiza safari yangu ya
elimu na kuzima ndoto nilikuwa nayo ya kuwa niwe mwalimu”, alisema.
Katika kijiji cha Msuka Wilaya ya Michweni, Aziza
Bakar alikuwa na ndoto ya kuwa mwanasheria, alitamani kutetea haki za watu na
kusaidia jamii kupitia taaluma ya sheria.
Leo hii anaamini kuwa kama angepata mazingira bora
ya malezi na msaada wa kutosha, angekuwa karibu zaidi na kutimiza ndoto yake.
“Baada ya wazazi wangu kuachana nililelewa na bibi nikawa
sina hata msukumo wa kusoma” alieleza.
Naye Maryam Ali Zahor wa Gando Wilaya ya Wete alikuwa
na ndoto ya kufanya kazi ofisini na kujitegemea kupitia elimu yake.
Aliona elimu kama daraja la kufikia maisha bora
ingawa changamoto za kifamilia zilizotokana na kuvunjika kwa ndoa ya wazazi
wake, ziliathiri safari ya masomo na matumaini yake ya kufikia malengo,
Afisa ustawi wa jamii Wilaya ya Wete Mkoa wa
Kaskazini Pemba Salama Saleh Hamad anataja kesi 34 zikiwemo 16 za huduma na 18
za mvutano wa malezi zimeripotiwa kwa mwezi January hadi Aprili 2026.
Kesi za migogoro ya ndoa zilizoripotiwa zilikuwa ni
tano ambapo madai ya talaka zilikuwa mbili.
Anasema athari kwa watoto wa kike ni kukosa huduma muhimu
ikiwemo elimu na kuathiri msongo wa mawazo na kubakia kudhalilika .
Mzazi Asha Suheil wa Chimba ,anakiri talaka zimekuwa
miongoni mwa sababu zinazowakwamisha watoto wa kike kutimiza ndoto zao.
“Baadhi ya akina baba huondoka kwa muda mrefu kwenda
nje ya maeneo yao ya makazi, huacha familia bila huduma muhimu na wakati
mwingine huwapa talaka wake zao bila sababu za msingi.
“Matokeo yake wazazi wanapogombana na kutengana watoto
ndio wanaobeba maumivu na athari kubwa zaidi, anasema.
Naye Moza Faki Shaaban wa Finya anasema migogoro ya kifamilia
mara nyingi husababisha mahitaji muhimu ya watoto kuwekwa pembeni.“Wakati
wazazi wanapokuwa katika mgogoro, suala la elimu, afya na mahitaji mengine ya
watoto hupoteza kipaumbele mwishowe watoto ndio wanaoumia zaidi, anasema.
Faki Abdalla Shauri wa Konde anasema anajutia
kitendo alichokifanya cha kumuacha mke aliyezaa nae watoto nane, huku
akisisitiza wanandoa kuwa na busara bila hivyo ndoa huvunjika na kusambaratisha
watoto.
Fatma Shaaban Omar wa Wete ni mmoja kati ya wanawake walioachwa akiwa na watoto
sita, anasema ugumu wa maisha ,ulezi wa watoto hao sita pekee bila usaidizi wa
baba kunapelekea kukosa huduma muhimu ikiwemo chakula, elimu ,mavazi.
“Wanawake tunatwishwa mzigo mzito kwani wanaume
wanapotuacha na tukiwa tayari tumeshazaa watoto ndio wanaohangaika”anasema.
Nae Sada Ali Juma wa Konde ambae ameachwa na watoto
wanne wote wakiwa wanawake anasema
kutokana na ulezi wa peke yake imebidi watoto wake wajishughulishe na ajira za
utotoni ikiwemo kuuza biashara ndogondogo, ili wapate mahitaji hasa ya chakula.
Kutokana na hali hiyo, Chama cha Waandishi wa Habari
Wanawake Tanzania (TAMWA Zanzibar) kinatekeleza mradi wa tunaweza pamoja
kumaliza udhalilishaji wakijinsia kwa wanawake na wasichana EVAWG.
Mradi huo ambao kwa kisiwa cha Pemba umejikita Mkoa wa
kaskazini utaweza kuibua changamoto zilizojificha ambazo zinawarejesha nyuma
wasichana na watoto wakike na kudhalilishwa.
Mratibu wa mradi huo Asya Hakim Makame anasema tathmini
zilizofanywa na shirika hilo zimeonesha kuwa
watoto wengi wanaokulia katika malezi ya upande
mmoja hukabiliwa na changamoto za elimu, malezi na ustawi wa kisaikolojia.
“Tulibaini kuwa talaka ni miongoni mwa sababu zinazochangia
ongezeko la watoto wanaolelewa na mzazi mmoja.
“Watoto wa kike ndio wanaoathirika zaidi kwa kuwa
baadhi yao hulazimika kuacha skuli, kuingia katika ndoa za mapema au kukosa msaada
unaohitajika kufikia ndoto zao”, anasema.
Kwa mujibu wa TAMWA, mradi huo unalenga kuongeza
uelewa kwa wazazi, viongozi wa dini, viongozi wa serikali na jamii kwa ujumla
kuhusu umuhimu wa kulinda haki za mtoto na kuhakikisha kuwa migogoro ya wazazi
haiwi sababu ya kuwanyima watoto fursa za maendeleo.
Mwalimu wa skuli ya Sekondari ya Msuka Wilaya ya Micheweni
Amini Khamis Khatib anasema mara nyingi wanafunzi hasa wa kike wanapotoka
katika familia zenye migogoro huonesha kushuka kwa mahudhurio, ufaulu na
kujiamini.
“Wanafunzi hao wapo hasa wa kike ingawa
tunapowagunduwa tunawapa ushauri mzuri kuwaondowa na msongo wa mawazo ili
waweze kusoma huku wakitimiza malengo yao”,anasema.
Mshauri nasaha Fatma Mohamed Khalfan anasema wazazi
wanapoachana kuna maumivu ya kihisia anayapata mtoto, na kujawa na huzuni huku akijiona duni na hana thamani.
Anasema talaka inaathiri jamii kwa kuongezeka watoto
wa mitaani wanaoweza kujishughulisha na vikundi viovu na hatimae kuwa wizi ama
watumiaji madawa ya kulevya.
Kwa mujibu wa sensa ya watu na makaazi ya 2022 ,
ripoti ya OECD inayotumia takwimu za Tanzania inaonesha
kuwa asilimia 37 ya wanawake wenye umri wa miaka 15 na
zaidi Kaskazini Pemba waliopewa kabla ya kutimiza miaka 18.
Ambapo kwa mujibu wa sensa hiohio Mkoa wa Kaskazini Pemba
una asilimia 17.5 walioacha skuli.
Akizungumzia suala hilo, Sheikh Said Abdalla kutoka ofisi ya mufti Pemba anasema
uislamu unatambua talaka kama suluhisho la mwisho pale maridhiano yanaposhindikana,
lakini hauondoi wajibu wa wazazi kwawatoto wao.
“Katika Uislamu, mtoto ana haki ya kupata malezi,
elimu, matunzo na mapenzi kutoka kwa wazazi wake, talaka inaweza kuvunja ndoa,
lakini haiwezi kuvunja wajibu wa wazazi kwa watoto wao”, anasema.
Mchungaji wa Kanisa la ‘TAG’ Kaskazini Pemba Samwel
Elias Maganga anasema familia ni taasisi ya kwanza ya malezi iliyowekwa na
Mungu na kwamba wazazi wanapaswa kuhakikisha watoto hawawi waathirika wa
migogoro yao.
“Watoto wanahitaji upendo, mwongozo na usalama wa
kihisia, migogoro ya ndoa isipopewa ufumbuzi mzuri,
watoto ndio hubeba maumivu yake kwa muda mrefu
zaidi, anasema.
Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mgeni Khatib Yahya, anasema serikali inaendelea kuweka mazingira bora ya kuhakikisha watoto wote, hususan watoto wa kike, wanapata haki zao za msingi ikiwemo elimu, malezi bora na ulinzi dhidi ya changamoto z


Comments
Post a Comment