UJENZI WA MIUNDO MBINU YA VIWANJA VYA MICHEZO UZINGATIE JINSIA.
NA ASIA MWALIM
KATIKA Nchi nyingi siku hizi miundo mbinu ya viawanja vya michezo huzingatia mambo mengi ikiwemo vyumba vya kubadilishia nguo wachezaji ili watu wa rika zote na jinsia tofauti waweze kuvitumia viwanja hivyo bila ya matatizo.
Kwa bahati mbaya hapa kwetu vigezo hivi havijapewa umuhimu unaostahiki kwenye viwanja vidogo vidogo na vinavyotumika kwa ajili ya mazoezi na mechi za kirafiki.
Ni hali ya kusikitisha na hili kwa kiasi kikubwa imekua inachangia wanawake na wasichana kujiona wanatengwa na kudhalilishwa na kwamba wanakosa haki zao za kibinaadamu.
Zanzibar imebarikiwa viwanja vingi vya michezo mjini na vijijini lakini unapofuatilia kwa karibu utabaini miundo mbinu hiyo sio rafiki kwa watoto wa kike na mara nyengine huwa sababu ya vitendo vya udhalilishaji kwao.
WANAFUNZI WA KIKE
Ashura Omar Majaaliwa mwanafunzi wa darasa la nne skuli ya msingi Salim Turky, anasema anapenda michezo tofauti ingawa katika mazingira ya skuli hiyo kuna kiwanja kimoja tu cha kucheza mchezo wa kikapu ambapo kiwanja hicho wanatumia wanafunzi wa kiume kucheza mpira wakati wa mapumziko.
Anasema ni vyema viwanja vinavyojengwa skuli na nje ya skuli kuzingatia jinsia ili kuwa na mazingira wezeshi kwa wasichana wanapotaka kucheza, “Kukiwa na michezo mengine wanafunzi hulazimika kutoka nje ya skuli na kuomba kiwanja kilichopo pembezoni wa skuli ili kucheza mpira wa wavu au wa miguu jambo hili linawarudisha nyuma shauku ya wasichana na wavulana wa skuli hii kupenda na kuendeleza michezo” anasema.
Fatma Ali Chanzi msichana wa chuo kikuu ambae ni mshabiki na mpenzi wa michezo hasa mpira wa vikapu anasema viwanja vingi vya michezo sio rafiki kwa watoto wa kike na mara nyingine hulazimika kukatisha ndoto zao kutokana na mazingira ya wanayoyakuta vuiwanjani.
“Hakuna mzazi anaependa mtoto wake adhalilike, sifikirii kama kuna mzazi atakaeruhusu binti yake kuvaa nguo katika kiwanja cha mnazi mmoja au chengine chchote ambacho hakina sitara huku akiwa amezungukwa na wanaume pembeni, kwa sababu viwanja vinazungukwa na watu wengi na kila mmoja ana uhuru wa kuvitumia” anasema Fatma.
“Tunaona jamii yetu ilivyokosa imani kwa wachezaji wa kike, anapita mzazi anamkuta mtoto wa kike anabadilisha nguo katika mazingira yasiyo rafiki hawezi kukubali mtoto wake kuwa mchezaji, huo ndio ukweli”anafafanua.
VIONGOZI WA TIMU
Riziki Aboubakar Islah, mwalimu wa mpira wa miguu, anasema viwanja vingi havina mazingira rafiki kwa watoto wa kike ikiwemo kushindwa kupata nafasi ya kubadilisha nguo wakati wa kujiandaa na michezo na kulazimika kubadilisha nguo ndani ya viwanja.
“Sasa hivi mwandishi wa habari nikikwambia nenda kiwanja cha Mnazi Mmoja, kanitafutie sehemu ya vyumba vya kubadilisha nguo, huipati, lakini ni kiwanja,” anasema Riziki akiwa pembezoni ya uwanja huo.
Anasema hali hiyo huzifanya ndoto za watoto wa kike kuishia njiani na kwa vile wengi wao wanapenda kujistiri. “Unaweza ukatimiza ndoto za wasichana wengi kwenye kile kiwanja, mazingira ndiyo yanasababisha zile ndoto zao zife.”
Msichana anatoka nyumbani kwao amevalia vizuri, baibui na kila kitu chake, akifika sehemu ya michezo abadilishe [nguo], aingie mchezoni, afanye shughuli ya michezo, amalize, avae tena vizuri, [mazingira ya kuwezesha] hicho kitu hakuna,” anatoa ushuhuda mwalimu Riziki.
“Ili soka liweze kuwatoa wasichana kimaendeleo, miundo mbinu yenye mazingira rafiki kwa watoto wakike, na mengine mengi yanapaswa kubadilika kwanza.” anasema.
WADAU WA MICHEZO.
Hija Mohamed Ramadhani ni Mshauri wa masuala ya jinsia kwenye Mradi wa michezo na Maendeleo unaotekelezwa na Shirika la Maendeleo la Ujerumani amesema mradi huo unapanga kuboresha viwanja 7 vya michezo Visiwani Zanzibar maana Unguja na Pemba ili kutoa fursa za uhamasishaji wa michezo kwa wasichana na wanawake.
Ameishauri serikali pia iangalie jinsi ambavyo itasaidia kuwepo kwa viwanja vya michezo katika skuli”Ni vyema kuwepo kwa viwanja ili vipaji viwe na muendelezo na ushawishi katika jamii hivyo ni serikali iangalie hili wakati inapojenga na kufanya ukarabati kwenye skuli “Amemalizia Hija .
WANAHARAKATI
DK.Mzuri Issa Mkurugenzi Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania upande wa Zanzibar (TAMWA ZNZ) anasema ikiwa miundo mbinu ya viwanja vya michezo yatakuwa rafiki kwa watoto wa kike pamoja na kujengewa sehemu za kubadilisha nguo ili kujistiri matumaini makubwa ya kuibua vipaji vya wachezaji wanawake yatatimia.
“Sio rshisi kwa mzazi yeyote awe mjini au kijijini kumruhusu mtoto wake kwenda mahala hatarishi au pasipo salama, umefika wakati sasa kila mmoja kuona umuhimu wa kulisemea suala hili ili kuhamasisha wasichana kutimiza ndoto zao”anasema.
“vipaji vitaibuka kwa kwa kasi ikiwa miundo mbinu ya viwanja vya michezo vitakuwa na mazingira wezeshi kwa wanawake kujistiri, na kujiandaa kabla na baada ya kumaliza michezo, jambo ambalo kwa muda mrefu halipo”anasema.
WIZARA YA HABARI
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana Utamaduni na Michezo Fatma Hamad Rajab amesema seriali imeamua kujenga viwanja vya michezo vya kisasa ili kuondoa changamoto zinazojitokeza kawa wachezaji wa kike na kiume kwa upande wa Unguja na Pemba.
“Tunashuhudia kasi ya maendeleo inayofanywa na Dk.Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi katika kuimarisha sekta ya michezo tunaamini changamoto hizo zitaondoka muda sio mrufu kwani viwanja viatkuwepo vya kutosha vikiwa na mazingira salama kwa wote”anasema.
Comments
Post a Comment