MATUMAINI YA WANAWAKE KWENYE MICHEZO YANATEGEMEA MIFUMO SHIRIKIKISHI.
NA ASIA MWALIM
MATUMAINI ya wanawake kwenye michezo yanategemea mifumo shirikishi ambayo yanawapa nafasi ya kushiriki kikamilifu, kujifunza na kukua kama wanamichezo
“Huwezi kumwambia mgeni apite wakati mlango wa nyumba yako ukiwa umeufunga” Maneno yanapokua asilimia 90 lakini vitendo ni asilimia 0, hatuwezi kusema tuna mifumo Shirikishi ambayo inayowajumuisha wanawake katika maamuzi, mipango, na utekelezaji wa shughuli mbalimbali za michezo.
Ni wakati sasa kwa wadau mbali mbali wa michezo na jamii kushirikiana katika kuweka mifumo shirikishi kwenye sekta ya michezo ili kufikia usawa wa jinsia kwenye michezo.
Mifumo shirikishi inatoa matumaini makubwa kwa wanawake katika michezo kwa kuimarisha ushiriki wao, kutoa fursa za maendeleo, na kuboresha mazingira ya ushindani.
Kwa hivyo ni muhimu kuimarisha mifumo hii ili kuhakikisha kwamba wanawake wanaweza kufikia malengo yao katika ulimwengu wa michezo.
WACHEZAJI WAKIKE
Mchezaji Kidawa Kheri Hamad na kapteni wa timu ya mpira wa miguu ya wanawake ya Green Queens anasema ili matumaini ya wanawake katika soka yatimie ni lazima kuwe na Ushiriki wa Wanawake Katika Uongozi, Kwa mfano, uwepo wa wanawake katika bodi za uongozi unaweza kusaidia kutunga sera zinazowasaidia wanawake.
“Wanawake wanapokuwa katika nafasi za uongozi ndani ya mashirika ya michezo, wanaweza kuleta mabadiliko chanya yanayosaidia kukuza ushiriki wa wanawake” anasema.
Nae mchezaji Salama Mcha Khamis anadai kuwa njia nyengine ni uwepo wa Mafunzo na Rasilimali,Hii inaweza kujumuisha programu za mafunzo ya kocha, ufadhili wa safari za mashindano, au vifaa vya michezo”.
“Unakuta timu za wanawake hazifikii malengo kwa kukosa Mifumo shirikishi ikiwemo mafunzo na rasilimali kwa wanawake ili waweze kujiendeleza katika michezo.” anasema.
WACHEZAJI WA KIUME
Ahmed Ishaka Haji mchezaji timu ya KMKM anasema umefika wakati wa Kuunda Jamii za Kusaidiana, kwani Mifumo shirikishi hujenga jamii ambazo zinawasaidia wanawake kushiriki katika michezo pamoja.
“njia hii inaweza kuwa vikundi vya wanamichezo au mitandao ambayo inawapa wanawake nafasi ya kushiriki uzoefu wao na kusaidiana”anasema.
Anasema jambo jengine lakufanywa ili kupata mifumo shirikishi kwa wachezaji wakike ni kujenga Uelewa wa Usawa katika jamii.
“Mifumo shirikishi husaidia kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa usawa kati ya jinsia katika michezo ni vyema jamii kulitambua hili” anasema.
JAMII
Baadhi ya wazazi wanasema ili kuwa na mifumo shirikishi katika michezo ni lazima kuwa na ushiriki mpana ili kukuza vipaji vyao na kuonekeana.
“Wanawake wanaposhiriki zaidi katika shughuli za michezo, wanapata fursa zaidi za kuonyesha vipaji vyao, Kukuza vipaji miongoni mwa wanawake” anasema.
VIONGOZI WA TIMU
Neema Machano Athumani (kocha) na Kocha wa timu ya Mamlaka ya Maji na Nishati Zanzibar (ZURA) Simai Mwinyi, wanasema mifumo shirikishi na matumaini ya wachezaji wa kike yatafikiwa kwa haraka endapo watajengwa ujasiri
Kuwa na Ushiriki katika mifumo shirikishi hujenga ujasiri miongoni mwa wanawake ambao wanaweza kuwa viongozi bora na wanamichezo wenye mafanikio.
WADAU
Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu wilaya ya Mjini (UDFA) Mohammed Rashid Bwaksi anasema wanawake wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi zinazohusiana na ushiriki wao, fursa za maendeleo, na upatikanaji wa rasilimali ni vyema kuwekwa mifumo shirikishi katika jamii ili kundi hilo kupata fursa sawa.
Anabainisha kuwa wanawake wakiekewa mifumo shiriki wataweza kushughulikia changamoto zinazowakabili kupitia ushirikiano na msaada kutoka kwa wenzao na kusaidia kubadilisha mitazamo potofu kuhusu uwezo wa wanawake katika michezo.
Matumaini ya wanawake kwenye michezo yanategemea mifumo shirikishi ambayo inawapa nafasi ya kushiriki kikamilifu, kujifunza, na kukua kama wanamichezo.
Kwa hivyo, ni muhimu kuimarisha mifumo hii ili kuhakikisha kwamba wanawake wanaweza kufikia malengo yao katika ulimwengu wa michezo.
WANAHARAKATI
Haura Shamte Muandishi wa Habari mongwe na mtaalamu wa masuala ya kijinsia, anasema umefika wakati jamii kubadili mitazamo hasi juu ya suala la ushiriki wa wanawake katika michezo mbalimbali ili nao waweze kupata haki yao ya msingi ya kuchangamana kupitia michezo hiyo.
Alieleza wasichana wengi wanashindwa kufikia ndoto zao kutokana na vikwazo mbalimbali ikiwemo mifumo isiyowashirikisha moja kwa moja hivyo mara nyingine kukosa matumaini.
“Bado hakuna idadi sawia ya wanawake wanaopata mamlaka katika tasnia ya michezo, ukatili na ujira mdogo kwa wanawake wanamichezo ni miongoni mwa sababu zinazoshusha hamasa kwa wasichana wengi kujihusisha na michezo.” alisema.
IDARA YA MICHEZO
Kamishna Idara ya Michezo Zanzibar, Ameir Mohammed Makame anasema bado jamii haina muamko wa kuhamasisha michezo kwa mtoto wa kike kwani wanahisi ni kitendo kinachokwenda kinyume na maadili yao.
Alisema Idara hiyo imekua ikitoa fursa nyingi kupitia michezo, umefika wakati kuwa na mifumo shirikishi ili wafaidike kwenye fursa hizo kwani serikali imekua ikitoa fursa mbali mbali za kimaendeleo ikiwemo ajira na kushiriki mabonanza ndani na nje ya Zanzibar.
Sambamba na hayo alisema ipo haja kwa serikali kushirikiana na wadau mbali mbali kuelimisha jamii na wazazi umuhimu wa michezo ili kuweka tumaini kubwa kwa wanawake katika soka.
VIONGOZI WA SERIKALI
Katika hotuba zake za hivi karibuni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi DK.Huusein Ali Mwinyi alisema serikali ya awamu ya nane imeelekeza nguvu zake katika michezo kwa kujenga viwanja vya michezo ili kila mmoja apate fursa ya kushiriki bila ya kujali jinsia zao.
Alibainisha kuwa anatambua michezo ni ajira, afyana ndio maana imeamua kujenga viwanja katika wilaya zote za Unguja na Pemba kwa lengo la kutoa fursa sawa kwa wanawake na wanaume kwenye sekta hiyo.
Katika uongozi wa Dk.Mwinyi michezo ni miongoni mwa vipaumbele vyake akiamini michezo inaongeza ufahamu kwa wanafunzi kufanya vizuri kwenye masomo yao pia kuimarisha afya ili kuondosha maradhi mbali mbali.
Comments
Post a Comment