ATHARI ZA KUTOWASHIRIKISHA WANAWAKE MICHEZO.
ASIA MWALIM
WANASOKA wengi wanawake kutoka Zanzibar wanatamani kufikia angalau viwango vya wenzao kutoka Tanzania Bara, ambako soka la wanawake linaonekana kufanya vizuri.
Mwaka 2016, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilianzisha ligi kuu ya wanawake ambayo imeendelea kufanyika na msimu wa mwisho wa 2023/2024 timu ya Simba Queens waliibuka mabingwa.
Ikumbukwe kuwa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ambayo ni 17 kati ya hayo lengo namba 5 linazungumzia “Usawa wa Jinsia” hii ina maana ya ushirikishwaji na ushirikiano kwenye kufanikisha usawa wa jinsia kwa upande wa wanaume, wavulana wanawake na wasichana.
Kutowashirikisha watoto wa kike katika michezo kuna sababisha athari mbaya ambazo zinaweza kudumaza maendeleo yao ya kimwili, kiakili, na kijamii.
Ni muhimu kuhakikisha wasichana wanapata nafasi sawa katika michezo ili waweze kufikia uwezo wao kamili.
Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania -Zanzibar (TAMWA-ZNZ), ni mmoja wa wadau wanaojaribu kukabiliana na changamoto hizo kwa kutekeleza programu zenye lengo la kuiwezesha jamii kuwa na mitazamo chanya kuhusu soka la wanawake na wanamichezo wenyewe.
WACHEZAJI
Farida Khamis Kombo Mchezi wa timu ya Green Qeens ya Kiembesamaki anasema moja ya changamoto inayowakabili watoto wa kike ni Kukosa fursa ya kukuza vipaji, “Wanawake wanapozuiliwa kushiriki katika michezo, wanakosa fursa ya kukuza vipaji vyao na kupata ufanisi katika sekta ya michezo”.
Hii inaweza kupunguza uwezo wa wanawake kuonyesha uwezo wao, kupiga hatua, na kufikia malengo yao binafsi na kitaifa.
“tunashuhudia watoto wa kike kwa muda mrefu walikua wanakosa ujasiri, kwani ukishiriki michezo mara nyingi hujifunza kujitambua na kuwa jasiri ni vyema wazazi kuwaruhusu watoto wa kike ili wasijisikie dhaifu au wasiokua na thamani.
Anataja changamoto nyengine ni Kukosa mifano ya kuigwa, Wanapokosa nafasi za kushiriki katika michezo, wanawake wanakosa mifano ya kuigwa ya wanawake wanaofanya vizuri kwenye michezo.”tunatamani zanzibar nayo ipate wachezaji wengi wakike, ni lazima kupata mifano mizuri ya kuigwa na wengine” anasema.
Hii inaweza kuchangia katika kupunguza motisha kwa wasichana kujiunga na michezo na kufikia malengo yao.
WAZAZI
Fatma Bakari Bilali anasema miongoni mwa athari alizozishuhudia ni pamoja na Ukosefu wa usawa wa kijinsia, Kutokuwashirikisha wanawake katika michezo kunachangia katika kudumisha usawa wa kijinsia mdogo.
“Kwanini watoto wazazi hawatengi muda wa michezo kwa ajili ya watoto wao wa kike na kuwapa kazi za ndani muda wote tofauti na watoto wa kime jambo hili si sawa na wala halitoi fursa sawa” anasema.
Hii inazidi kudhoofisha juhudi za jamii na serikali katika kuhakikisha wanawake wanapata haki sawa na wanaume katika nyanja mbalimbali za maisha.
Anataja changamoto nyengine ni Kupunguza ufanisi wa taifa: Ikiwa wanawake hawashirikishwi katika michezo, taifa linakosa timu au wachezaji wa kiwango cha juu kutoka kwa wanawake ambao wanaweza kuchangia mafanikio ya kitaifa katika mashindano ya kimataifa.
Hii pia inachelewesha maendeleo ya taifa katika medani za kimichezo.
WALIMU
Neema Machano Athumani, mwalimu wa mchezo wa mpira wa miguu (KOCHA) anasema moja ya ya athari za kutowashirikisha wasichana na wanawake katika michezo ni Kupunguza fursa za ajira,
“Kutowashirikisha wanawake katika michezo kunapunguza fursa za ajira kwa wanawake katika sekta ya michezo, kama vile mafunzo ya michezo, usimamizi wa timu, au kazi za kitaalamu zinazohusiana na michezo”.anasema.
Watoto wa kike wanaokosa fursa ya kushiriki michezo, wanakosa ujuzi wa maisha na kujifunza ujuzi umuhimu wa mawasiliano, ushirikiano na uongozi jambo ambalo husababisha wengi wao wasiwe tayari kukabiliana na changamoto mbali mbali za kimaisha.
Anasema changamoto nyengine ni kuwa na matarajio duni, wasichana amabao hawajihusishi na michezo wanweza kukosa motisha ya kufikia malengo yao na kukosa kufanya juhudi.
DAKTARI WA MICHEZO
Rahma Abdallah Munir, (29) ambae hivi sasa anajulikana kama daktari wa kike katika timu ya Baraza la wawakilishi Zanzibar (BLW) anasema licha ya athari hizo za kijamii pia kuna Athari kwa afya ya kimwili na kiakili.
“Michezo ni njia muhimu ya kuboresha afya ya kimwili na kiakili Kutokuwashirikisha wanawake katika michezo kunapunguza nafasi zao za kushiriki katika shughuli zinazoweza kuboresha afya zao, kuzuia magonjwa, na kupunguza mfadhaiko” anasema.
“watoto ambao hawajihusishi na shughuli za kimwili mara nyingi wanashindwa kudhibiti uzito kupita kiasi au unene na kupelekea magonjwa kama kisukari na sinikizo la damu” anasema.
Anataja maradhi mengine ni pamoja na afya ya moyo kwa kushindwa kufanya kazi vizuri ambapo michezo huimarisha afya ya moyo na mfumo wa mzunguko wa damu.
WANAHARAKATI NA WADAU WA MICHEZO
Rahma Ali Juma, Afisa kutoka Kituo cha Majadiliano ya Vijana (CYD), alisisitiza umuhimu wa michezo katika kuunda mustakabali wa wasichana hao. "Tunajivunia kuwa na wasichana 150 kutoka shule za msingi wanaoshiriki katika shughuli zetu mwaka huu.
Wasichana hawa si tu kucheza netball-wanajifunza jinsi ya kujilinda kutokana na jinsia zao ili kuepusha athari mbali mbali kuwapata.
“Wasichana hawa hawachezi tu mpira wa wavu - wanajifunza jinsi ya kujilinda dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia na kupata ujuzi katika uongozi ambao utawanufaisha katika maisha yao yote." Anasema Rahma.
Khairat Haji, Afisa Michezo wa Maendeleo katika TAMWA-Zanzibar, anasisitiza athari pana za kijamii za mipango hii.
"Kupitia michezo, tunawafundisha wasichana sio tu thamani ya kazi ya pamoja lakini pia kwamba wana haki ya kushiriki sawa katika nyanja zote za maisha. “Ni juu ya kubadilisha mawazo na kukuza utamaduni wa kuingwa Zanzibar." anasema.
anasema changamoto hizo hupelekea moja kwa moja kudhoofisha haki za wanawake na wasichana, “Kutokuwashirikisha wanawake katika michezo ni sehemu ya udhalilishaji wa kijinsia” anasema.
Inadhihirisha mtindo wa kudumisha mifumo dume ya kijamii na kisheria ambayo inawaweka wanawake nyuma na kutoweza kuwa na usawa katika fursa zinazopatikana kwa jinsia zote.
Kwa hivyo, ni muhimu kuhamasisha na kuunga mkono ushiriki wa wanawake katika michezo ili kuepuka athari hizi na kuleta maendeleo bora katika jamii na taifa.
Comments
Post a Comment