TAMWA YAWAASA WANAHARAKATI

NA ASIA MWALIM 

MJUMBE Wa Bodi kutoka Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA-ZNZ) Mwatima Issa Rashid, amewataka wanaharakati kuzitumia siku 16 za kupinga udhalilishaji kuleta mabadiliko ya muda mrefu katika kujenga jamii yenye utu, heshima amani na utulivu nchini.

Alitoa wito huo katika maadhimisho ya kupinga siku 16 za udhalilishaji yalioandaliwa na TAMWA Zanzibar, kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) hafla iliyofanyika ukumbi wa Bima, Mperani Mjini Unguja.

Alisema michango ya wanaharakati ina nafasi kubwa na inathaminika kusaidia mapambano ya vitendo vya udhalilishaji na unyanyasaji wa kijinsia nchini.

Aidha aliwataka wanaharakati kuitumia siku hiyo kupokea na kujadiliana mchango mbali mbali itakayowasilishwa ili kuwa chanzo cha kujenga ari mpya kuwavutia wengine kuungana nao kupinga vitendo hivyo.

Alisema kwa sasa TAMWA ina nafasi kubwa ya kupaisha sauti za wanawake na makundi mengine kwa kua mstari wa mbele kushajihisha na kutoa taaluma kupitia vyombo vya habari ili kufikia jamii kubwa na kwa wakati.

Mjumbe huyo alifahamisha kuwa serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zinafanya jitihada mbali mbali kupinga vitendo vya udhalilishaji ni vyema wanaharakati kuendelea kuungana bila ya kuchoka kupinga vitendo hivyo.

Alieleza lengo la maadhimisho hayo ni kujenga jamii iliyohuru kuepukana na vitendo vya udhalilishaji na majanga mengine yanayochafua sifa na maadili yanayochafua maisha ya kila binaadamu.

Akiwasilisha ripoti Afisa Programu kutoka Mradi wa Michezo kwa Maendeleo (GIZ) Khairat Haji, alisema kwa mujibu wa takwimu kutoka ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, kutoka Januari hadi Oktoba 2024 jumla ya matukio ya udhalilishaji yaliotokea na kuripotiwa ni 1582 huku waathirika ni 1583.

Alisema kati ya idadi hiyo 1337 ni watoto ambapo wasichana ni 1095 na wavulana ni 242 ambao ni sawa na asilimia 84.4 ya waathirika wote.

Alieleza kuwa watoto wenye umri wa miaka 17 hadi 17 ni 693 ni sawa asilimia 52, ambapo wanawake watu wazima walioathirika 183 na wanaume watu wazima 63, huku wilaya ya Magharibi B ikiongoza kwa matukio ya udhalilishaji 386, ikifuatiwa na Mjini 344 na 373 magaharibi A.

Nayla Abdulbasit Omeyar, Hakimu wa Mkoa wa Kusini Unguja, alisema serikali imeweka juhudi ya kuweka midoli kwenye mahakama kuelewesha watoto ili waweze kujieleza na kutoa ushahidi kwa urahisi wanapokutwa na vitendo hivyo.

Baadhi ya wanaharakati waliohudhuria maadhimisho hayo, Shukuru Maloda, Sabah Bakari Hassan walisema ni vyema jamii kuona ukubwa wa tatizo hilo kwa kufanya mambo yatakayoleta mabadiliko  ikiwemo viongozi wa dini ili kuijenga jamii kiroho.

Akifunga maadhimisho hayo, Meneja Mawasiliano TAMWA Zanzibar, Sophia Ngalapi alizishauri taasisi mbali mbali za serikali na binafsi kuona haja ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu sheria kwani jamii kubwa haina uelewa wa kujitetea wanapokutwa na masuala ya udhalilishaji.

Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni "kuelekea 2030 tuungane kutafakari na kuchukua hatua kumaliza udhalilishaji dhidi ya wanawake Zanzibar".

Comments

Popular posts from this blog

BAJAJI WAMLILIA RAIS DK MWINYI PEMBA ,WAOMBA MSAADA KWAKWE WASEMA WAMECHOSHWA NA HILI KUTOKA MAWASILIANO

Masheha wanawake wa Wilaya ya Magharib B walivyoleta mabadiliko na maendeleo kwenye shehia zao.

MPANG0 MKAKATI JUMUISHI WA JINSIA KATIKA MICHEZO UTEKELEZAJI WAKE UZINGATIWE.