USHIRIKI NA USHIRIKISHWAJI WA WATU WENYE ULEMAVU KWENYE MICHEZO

 

NA ASIA MWALIM
MICHEZO kwa watu wenye ulemavu sio tukio la ushiriki wa mchezo wenyewe tu lakini ni hali halisi ya mabadiliko ya kijamii.

Mabadiliko hayo ni pamoja na ushiriki na ushirikishwaji wa makundi ya watu wenye ulemavu kwenye michezo kuonekana na kila mmoja katika jamii.
Kwa kuangazia vipaji vya watu wenye ulemavu azma na utofauti wao, michezo huchangia kubadilisha mawazo, kukuza ushirikishwaji na kujenga jamii yenye haki na jumuishi zaidi kwa wote.

Itakumbukwa kuwa kupitia siku ya kimataifa ya watu wenye ulemavu ya mwaka 2023, Katibu Mkuu Umoaja wa Mataifa (UN) Antonio Guterres alisema ili kufikia malengo ya maendeleo endelevu kunahitaji kutimiza ahadi ya kuto muacha nyuma mtu yeyote hasa mwenye ulemavu duniani kote.

Pia katika hatua ya nusu safari ya ajenda ya mwaka 2030, watu wenye ulemavu wanakabiliwa na ubaguzi wa kimfumo na vikwazo vinavyozuia ushirikishwaji katika maeneo yote ya kijamii ikiwemo michezo.

Makala haya yatajikita kuangalia ushiriki na ushirikishwaji wa watoto wa kike wenye ulemavu kwenye michezo.
 
WANAWAKE WENYE ULEMAVU
Amina Daudi Simba, mwanamke mwenye ulemavu wa viungo, alisema kwake michezo imekua sehemu ya maisha na anauthubutu wa kushiriki michezo mbali mbali licha ya hali yake aliyonayo.
Alitaja baadhi ya michezo anayoshiriki ni kuogolea, mpira wa kikapu, basket well chair, mbio za baskeli ya maringi matatu, na kurusha mishale.

Alisema licha ya ujuzi na uzoefu wake kwenye michezo bado jamii kubwa ina mitazamo mibaya juu yake na kumuwekea baadhi ya vikwazo kushiriki kikamilifu michezo hiyo.

Changamoto nyengine ni baadhi ya familia hawashirikishi ipasavyo watoto wao wa kike kwenye michezo kwa dhana mbaya na potofu walizonazo.

“Zipo baadhi ya familia wanahisi mtoto wa kike mweney ulemavu akishiriki michezo ni sehemu ya kumdhalilisha” alisema.

Alitaja miongoni mwa mafanikio aliyoyapata ni pamoja na kushiriki michezo ndani na nje ya nchi jambo amablo linampa faraja ya kuipenda Zaidi michezo.
 
WAZAZI
Baadhi ya wazazi wa watoto wenye ulemavu Zanzibar walisema, mazoezi ni kitu muhimu hasa kwa watoto wenye ulemavu ambao mara nyingi viungo vyao vinahitaji kufanyiwa mazoezi mara kwa mara.

Walisema kuna wakati hawaoni umuhimu wa kuwashirikisha watoto wao kutokana na changamoto wanazozipata wakati watoto wakike kwenye michezo badala yake kupata mzigo mkubwa wa kuwahudumia tofauti na walivyotegemea.

Khadija Salum Miraji, ni miongoni mwa wazazi wanaoishi na watoto wenye ulemavu, aliataja baadhi ya changamoto hizo ni gharama za vifaa vya michezo, na kukosa wafadhili wa wa kusaidia matibabu ya watoto hao wanapopata matatizo.
Hata hivyo aliwasisitiza wazazi kuwa mstari wa mbele kusimamia watoto wao kwani bila ya utayari wa wazazi watoto hao ni vigumu kushiriki kutokana na kuhitaji usaidizi.

“Wazazi tujitahidi kufanikisha suala la michezo kwa watoto wenye ulemavu bila ya kubagua jinsia zao kwani maendeleo hayajengwi upande mmoja bali tuwajenge watoto wote” alisema.
 
CHAMA CHA MICHEZO CHA WATU WENYE ULEMAVU
Mwenyekiti wa chama cha michezo cha watu wenye ulemavu wa akili Zanzibar, Sada Hamad Ali, alisema ushiriki na ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu kwenye michezo kwa watoto wa kike bado hauridhishi kwani kiwango chake kipo chini.

Alisea rasilimali fedha katika chama hicho ni miongoni mwa vikwazo vinavyorejesha nyuma ushiriki wa watu hao kujitokeza kwa wingi kwenye viwanja vya michezo.

Alitaja miongoni mwa hatua walizochukua kuhakikisha watu hao wanashiriki michezo alisema wamekua na utaratibu wa kuhima wazazi wenye watoto wenye ulemavu kuwapeleka viwanjani ingawa bado ushiriki wao ni mdogo.
 
WALIMU WA MICHEZO
Kocha na muwezeshaji wa michezo Riziki Issa, alisema wamekua na kawaida ya kutoa mafunzo kwa makundi mbali mbali ili kuona watoto wakike na watu wenye ulemavu kushiriki michezo kwa lengo la kutatua changamoto wanazokumbana nazo.

Alisema wasichana na watu wenye ulemavu wanakabiliwa na changamoto nyingi wanaposhiriki michezo ukilinganisha na wanaume ambao jamii imewajengea mazingira ya kuwafanya wao pekee ndio wenye haki ya kucheza hasa mchezo wa mpira.

Nae, Tahir Abubakar Kocha wa mpira wa miguu, Timu ya watu wenye ulemavu alisema miongoni mwa changamoto zianazorejesha nyuma ushiriki wa watu wenye ulemevu hasa wanawake kwenye michezo ni pamoja na mila potofu na jamii kukosa elimu.

Tahir ni mmoja ya watu wenye ulemavu wa (viuongo) mkono alisema kwa upande wake jamii kubwa inamchukilia kuwa hawezi kufindisha michezo kutokana na hali yake ya ulemavu lakini kiuhalisia anaweza.

Kwa sasa anaendelea kufundisha watu wenye ulemavu na wale wasio walemavu, na maendeleo yao ni mazuri kwenye michezo.

“Jamii inatuchukulia kuwa hatuna uwezo wa kufindisha lakini ki uhalisia tunaweza kushiriki ni vyema tushirikishwe bila ya kuangaliwa jinsia zetu na hali zetu za kimaumbile” alisema.

Sambamba na hayo aliishauri jamii kuacha tabia ya kuwaficha watu wenye ulemavu badala yake kuwashirikisha katika timu za michezo za watu wenye ulemavu ili kuimarisha afya zao na kuonesha vipaji.
 
JUMUIYA YA WATU WENYE ULEMAVU
Mratibu wa Jumuiya ya Wasiona Zanzibar (ZANAB) Adil Muhammed Ali, alisema licha ya Zanzibar kuwa na vipaji vingi vya wachezaji lakini hakuna uhamasishaji mkubwa katika michezo kwa watoto wa kike hasa wenye ulemavu aina mbali mbali ikiwemo wasioona.

Alisema michezo kwa watu wenye ulemavu inasemwa kwa mdomo lakini utekelezaji wake ni mdogo na hilo linaonekana pale zinapotokea sherehe mbali mbali za kitaifa, kwani watu wasioona hawashiriki wala hawashirikishwi.

Licha ya kuwepo timu ya watu wenye ulemavu lakini ushiriki wa watoto wa kike ni mdogo ikilinganishwa na wanaume hali inayotokana na utamaduni na mazoea mabaya ya jamii.

“Mara nyengine watu wenye ulemavu wanacheza michezo midogo midogo wakiwa ndani ya nyumba na sio kwenye viwanja husika ambako wataonekana vipaji vyao” alisema.

Aliomba serikali kulipa uzito suala la michezo kwa watu wenye ulemavu kwa kuwashirikisha ipasavyo sambamba na kutoa elimu, vifaa vya michezo na kuwafundisha wahusika namna ya kuklikabili jambo hilo.

Pia aliwataka viongozi wa majimbo kutoa vifaa ndani ya shehia zao kuandaa mabonaza yatakayowashirikisha watu wenye uemavu hasa wanawake ili jamii kulikubali na jambo hilo kwa wepesi.

“wanawake wanakua na aibu, kuvaa nguo za michezo na kucheza hasa watu wenye ulemavu kutokana na mila na tamaduni za wazanzibar” alisema.

Naye Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Watu wenye ulemavu Zanzibar, Ussi Debe alisema jumuiya hiyo inasiadia masuala mbali mbali ya watu wenye ulemavu ikwemo michezo kuchangia shilingi milioni mbili kila mwaka.

Alisema mipango ya serikali ni kuhakikisha watu wenye ulemavu wanashiriki na kushirikishwa kwenye michezo, pamoja na kuwapa mafunzo ili kuwaunga mkono watu hao.

Alibainisha kuwa mwaka jana timu ya watu wenye ulemavu wa akili ilifanikiwa kushiriki katika mashindano ya Olimpiki nchini Barlin, ambapo Rais wa Zanzibar na Mwenyeketi wa Barazala la Mapinduzi DK.Hussein Ali Mwinyi alifanikiwa kuungana na timu hiyo nje ya nchi.

WADAU
Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa habari Wanawake Tanzania (TAMWA Zanzibar), Dk. Mzuri Issa Ali alisema, watoto wa kike hasa wenye ulemavu wanapaswa kushiriki michezo kutokana na umuhimu wake katika kuimarisha afya na kupata fursa kama ilivyo wanaume.

Alisema sekta ya michezo ni miongoni mwa sekta muhimu kwa jamii imefika wakati watoto wakike na watu wenye ulemavu kuwekwa mstari wa mbele kwenye michezo ili nao kufikiwa na fursa mbali mbali zinazopatikana nchini.
Mshauri wa masuala ya michezo Jumuiya ya ushirikiano wa Kimataifa ya Ujerumani (GIZ) Hija Mohammed Ramadhan alisema kwa makusudi wameamua kushirikiana katika mradi wa wanawake na maendeleo kupitia michezo amabao utasaidia kuimarisha afya za watoto wa kike.

Ofisa Mradi wa michezo kwa Maendeleo kutoka TAMWA ZNZ, Khairat Haji Ali, wameamuamua kuanzisha mradi wa michezo kwa lengo la kuengeza ushiriki wa wanawake kwenye michezo ikiwemo wanawake wenye ulemavu.
 
SERIKALI KUPITIA IDARA YA MICHEZO YA ZANZIBAR
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar, ZFF Sleiman Mohammed Jabir alisema, licha jitahada mbali mbali wanazofanya katika michezo bado Zanzibar hakuna timu ya mpira wa miguu ya wanawake wenye ulemavu wa viungo kutokana na uchache wa watu hao viwanjani.

Alisema kwa mujibu wa sharia ya mchezo huo lazima timu iwe na wachezaji wasiopungua 12 na mpaka sasa idadi ya waliojitokeza haijafikia kiwango hicho.

Rais aliwashauri wazazi na jamii kiujumla kubadilika na kuchukua jitihada za makusudi katika kuhakikisha watu wenye ulemavu ikiwemo wanawake kushiriki michezo kama ilivyo kwa makundi mengine.
 
WIZARA YA HABARI VIJANA UTAMADUNI NA MICHEZO
Waziri wa Habari, vijana utamaduni na michezo Zanzibar, Tabia Mulid Mwita, akiwa kwenye mahujiano maalumu kabla ya kufanyika kongamano la kutimiza miaka mitatu ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kuingia madarakani alisema, serikali imezifanyia kazi changamomoto mbali mbali za michezo ikwemo kuwapa mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi wana michezo wakike.

Wakati huo ligi ya wanawake Zanzibar ilikua karibuni kuanza, alisema tayari changemoto nyingi zimea kazi zinazo kwamisha ushiriki wao katika michezo kwa lengo la kuondosha unyanyasaji wa kijinsia katika sekta ya michezo.

Aisema ili kuongeza ari ya wanawake katika michezo wanaendelea kusimamia vilabu na kutatuachangamoto zinazowafanya wanawake washindwa kujitokeza kwa wingi kushiriki.

Alitaja miongoni mwa hatua walizochukua katika kuimarisha michezo kwa watoto wa kike ni kushirikiana na wizara ya elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kutoa elimu kwa watoto wa kike juu ya umuhimu wa michezo kwa wanawake.
 
SERA NA SHERIA
Katiba ya shirikisho la mpira wa miguu (ZFF) ya mwaka 2018 toleo la 2021 inaeleza kuwa miongoni mwa wanachama wa shirikisho hilo watu wenye ulemavu wa aina mbali mbali ikiwemo viungo bila ya kujali jinsia zao.

Tamko la sera ya michezo ni kuwa serikali itahakikisha watu wenye mahitaji maalumu wanapatiwa fursa sawa za kushiriki michezo pamoja na kuweka mikakati ya kushajihisha jamii kutowaficha watu hao badala yake kuwashirikisha kwenye michezo.

Comments

Popular posts from this blog

BAJAJI WAMLILIA RAIS DK MWINYI PEMBA ,WAOMBA MSAADA KWAKWE WASEMA WAMECHOSHWA NA HILI KUTOKA MAWASILIANO

Masheha wanawake wa Wilaya ya Magharib B walivyoleta mabadiliko na maendeleo kwenye shehia zao.

MPANG0 MKAKATI JUMUISHI WA JINSIA KATIKA MICHEZO UTEKELEZAJI WAKE UZINGATIWE.