UMUHIMU WA WAZAZI KUTOA FURSA KWA WATOTO WA KIKE KUSHIRIKI MICHEZO
NA ASIA MWALIM
LICHA ya vikwazo na changamoato zinazowakuta watoto wa kike katika michezo, kwa sasa Soka la wanawake linakuwa kwa kasi zaidi Tanzania ingawa hakuna takwimu rasmi.
Ulimwengu wa michezo ni mahali ambapo wanawake wanachukuliwa tofauti na wanaume.
Tofauti hii inaonekana ngazi zote na kuanzia wanariadha mashuhuri, wachezaji mpira wa vyuo vikuu, mashuleni hata wasichana wadogo wanaocheza majumbani.
Kwa mujibu wa jarida la mtandaoni la INSIDER mchezaji mwanamke wa soka kiulimwengu anaelipwa pesa nyingi ni mchezaji wa timu ya USWTT anaitwa Carli LIoyd, anaekadiriwa kupokea mshahara kiasi cha dola za kimarekani 518,000 kwa mwaka.
Mataifa ya Brazil na Seierra Leone hivi karibuni yametangaza kwamba malipo ya wachezaji wa soka wakike yawe sawa na wakiume.
Utamaduni wa wanawake kucheza mpira wa miguu umeanza kueleweka kwa wengine, ingawa bado kuna kundi kubwa halijaelewa jambo hilo.
Hali hiyo imefanya wanawake na wasichana hapa Zanzibar kujiuliza kwa nini wanaokosa usawa wa kijinsia katika michezo hali hiyo inatokana na nini? Je kuna umuhimu kwa wazazi kutoa fursa kwa watoto wa kike kushiriki michezo.
WATOTO WA KIKE
Sharifa Ali Maulid, 17 alisema alipokua mtoto alishiriki nyimbo na michezo wa nage sio mpira wa miguu lakini alipofika darasa la sita tu alisitisha michezo.
Alisema anajisikia kuumwa mara tu anapomaliza kucheza nage anahisi ni kutokana na kuengezeka uzito wa mwili wake.
Shaymaa Hassan Mwinyi alisema, hajawahi kushiriki mchezo wa mpira wa miguu ingawa anaupenda sana mchezo huo anapoona wanaume wanacheza.
Alisema anaishi na mama yake pekee lakini hajawahi kumshajihisha suala la michezo badala yake mdogo wake wa kiume ndio huambiwa mara kwa mara acheze mpira.
"Mara nyingi mama yangu humwambia mdogo wangu wa kiume mwenye miaka 6 akacheze mpira muda mwengine humlazimisha hasa lakini mimi hanihimizi kwenye michezo" alisema.
Zainab Abdallah Suleiman, mwanafunzi wa kidato cha tatu alisema ni vyema serikali kuweka somo la michezo katika skuli zote na sio kuwekwa skuli maalumu kwani wanafunzi wote wanahitaji fursa ya michezo.
WAZAZI
Talhiya Khamis Mwinyi, alisema Ligi ya soka la wanawake imeibua vipaji kadhaa ambavyo vimeonekana na kuonesha ishara ya mafanikio katika soka hilo kwa siku za usoni.
Alisema michezo haibaki kama kucheza tu pia kuimarisha afya kwani husaidia kujikinga na maradhi mbali mbali mbilini.
Aidha alisema mbali na kuwa watoto wanapenda michezo jitihada za wazazi zinahitajika kuhamasisha michezo kwa wanawake kwani si jambo walilozoeshwa katika tamaduni zao.
JAMII
Mustafa Khamis Khamis, alisema mila na desturi walizolelewa katika familia yao ndio kikwazo kikubwa cha wanawake kushiriki michezo.
Alisema baba yake mzazi alimshuhudia akimkataza dada yake kucheza mpira wa mikono jambo ambalo limewafanya
Fatma Ali Chanzi, alisema wazazi wawaruhusu watoto wakike kwani nao wanatamani kuibua vipaji vyao, ili siku moja kuwakilisha timu za kitaifa na Kimataifa kupeperusha bendera ya Tanzania.
WALIMU WA MICHEZO
Kocha mkuu wa KMKM, Ame Msim alisema michezo kwa watoto inaongeza ufahamu kwenye masomo yao kwani hutulizanisha akili na kuipa uwezo mkubwa wa kufikiri masomo.
Alisema wanawake wengi wanaobahatika kupata fursa ya kushiriki michezo wanafanya vizuri viwanjani ingawa baadhi yao huishia njiani bila ya kujua sababu zinazowasitisha kucheza.
WANAHARAKATI
Haura Shamte Muandishi wa Habari mongwe na mtaalamu wa masuala ya kijinsia, alisema imefika wakati jamii kubadili mitazamo hasi juu ya suala la ushiriki wa wanawake katika michezo mbalimbali ili nao waweze kupata haki yao ya msingi ya kuchangamana kupitia michezo hiyo.
Alisema wasichana wengi wanashindwa kufikia ndoto zao kutokana na vikwazo mbalimbali ikiwemo vitendo vya ukatili katika michezo ambavyo hupelekea wazazi na jamii kuona michezo sio sehemu salama kwa wanawake.
Bi Haura alisema bado wazazi hawatoi nafasi sawa kwa wanawake na wasichana kushiriki katika fursa za michezo kutokana na hofu na mitazamo hasi iliyojengeka jambo linalopelekea kuwakosesha fursa mbalimbali zinazotokana na michezo ikiwemo afya, ajira na kipato.
Alieleza wasichana wengi wanashindwa kufikia ndoto zao kutokana na vikwazo mbalimbali ikiwemo vitendo vya ukatili katika michezo ambavyo hupelekea wazazi na jamii kuona michezo sio sehemu salama kwa wanawake.
“Bado hakuna idadi sawia ya wanawake wanaopata mamlaka katika tasnia ya michezo, ukatili na ujira mdogo kwa wanawake wanamichezo ni miongoni mwa sababu zinazoshusha hamasa kwa wasichana wengi kujihusisha na michezo.” alisema.
IDARA YA MICHEZO
Kamishna Idara ya Michezo Zanzibar, Ameir, alisema bado jamii haina muamko wa kuhamasisha michezo kwa mtoto wa kike kwani wanahisi ni kitendo kinachokwenda kinyume na maadili yao.
Alisema Idara hiyo imekua ikitoa fursa nyingi kupitia michezo, umefika wakati kushirikiana na watoto wao wa kike kwenye michezo ili wafaidike kwenye fursa hizo.
Alisema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kupitia Idara yake ya Michezo imekua iktoa fursa mbali mbali za kimaendeleo ikiwemo ajira, kushiriki mabonanza ndani na nje ya Zanzibar.
Sambamba na hayo alisema ipo haja kwa serikali kushirikiana na wadau mbali mbali kuelimisha jamii, wazazi umuhimu wa michezo ili kila mmoja kumruhusu mtoto wake bila ya kipingamizi chochote.
VIONGOZI WA SERIKALI
Katika hotuba zake za hivi karibuni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi DK.Huusein Ali Mwinyi alisemaserikali ya awamu ya nane imeelekeza nguvu zake katika michezo kwa kujenga viwanja vya michezo ili kila mmoja apate fursa ya kushiriki bila ya kujali jinsia zao.
Alibainisha kuwa anatambua michezo ni ajira, afyana ndio maana imeamua kujenga viwanja katika wilaya zote za Unguja na Pemba kwa lengo la kutoa fursa sawa kwa wanawake na wanaume kwenye sekta hiyo.
Katika uongozi wa Dk.Mwinyi michezo ni miongoni mwa vipaumbele vyake akiamini michezo inaongeza ufahamu kwa wanafunzi kufanya vizuri kwenye masomo yao pia kuimarisha afya ili kuondosha maradhi mbali mbali.
SHERIA
Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kifungu cha 12(1) kinaeleza kuwa watu ni sawa mbele ya sheria na wana haki ya kushiriki na kushirikishwa bila ya ubaguzi wowote, kulindwa na kupatiwa haki sawa.
Comments
Post a Comment