RC KASKAZINI PEMBA " NAAPA WAZAZI MTALALA RUMANDE " TUNATAKA MABADILIKO KWA WANAFUNZI WA SKULI HII HARAKA.
MKUU wa mkoa Kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib amewataka wazazi na waalimu wa wanafunzi skuli ya Sekondari Mchanga mdogo kusimamia na kutoa mashirikiano katika kuziondosha changamoto zinazokwamisha ufaulu mzuri kwa wanafunzi wa kidato cha nne ndani ya skuli hiyo.
Akizungumza katika mkutano maalum wa waalimu wazazi,kamati ya ulinzi na usalama, pamoja wanafunzi mkuu huyo amesema kuwa bado kuna changamoto kwa wazazi na waalimu ikiwemo suala la ufuatiliaji wa mienendo ya watoto ,ukosefu wa maadili na nidhamu kwa wanafunzi wanaosoma katika skuli hiyo ambazo zinapelekea kukosa utayari wa kuongeza bidii katika masomo yao jambo ambalo husababisha matokeo mabaya kwa wanafunzi wa kudato cha 4.
Amesema uongozi wa mkoa utaendelea kufuatilia kwa ukaribu mahudhurio ya wanafunzi wa skuli hiyo na kuchukua hatua ikiwemo kuwalaza rumande wazazi wa wanafunzi watoro,pamoja na watakaofanya vibaya katika mitihani ya majaribio itakayofanywa ili kuleta mabadiliko na matokeo chanya kwa wanafunzi kwa wanafunzi wa kidato cha 4 .
Aidha mkuu huyo ameagiza uongozi wa skuli hiyo kusimamia na kuchukua hatua za kinidhamu kwa wanafunzi watakaovaa mavazi yasiostahiki ikiwemo suruali za kubana , kukata mikato isiyo rasmi kufuga ndevu,kutoingia madarasani,kusuka misuko , hina pamoja na kuvaa mapambo huku akiwataka wanafunzi wote wa kiume kukata kipara kuanzia kesho.
Katika hatua nyengine mkuu huyo ameliagiza jeshi la polisi Mchanga mdogo pamoja na uongozi wa shehia kuzifuatailia na kuzifungia tv za usiku zinazooneshwa katika vibanda mbali mbali ndani ya shehia hiyo .
Sambamba na hayo Salama amewataka wazazi kuacha tabia ya kuwatumikisha watoto shughuli za kuuza biashara katika mitaa na maeneo mbali mbali na kuwakosesha muda wa masomo.
Nao baadhi ya wazazi na waalimu wa wanafunzi wa skuli hiyo wameushukuru uongozi wa mkoa huo kwa kufanya mkutano wa kujadili maendeleo ya wanafunzi ambapo wameahidi kutoa mashirikiano katika suala hilo litakalosaidia kuleta mabadiliko kwa watoto wao.
Kwa upande wao baadhi ya wanafunzi wameuomba uongozi wa wizara ya elimu Pemba kuwasaidia kuwawekea bweni litakalowasaidia kujisomea kwa pamoja muda wote wote
Mwisho.
Comments
Post a Comment