GOMBANI FITNESS KUJA NA BONANZA MAALUM KUHAMASISHA USAWA WA KIJINSIA .
NA HANIFA SALIM, PEMBA
KLABU ya mazoezi Gombani (Gombani Fitness Club) katika kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 10 ya klabu hiyo, imeandaa bonanza la michezo kwa lengo la kuhamasisha masuala ya michezo kwa jamii kwa kuzingatia usawa wa kijinsia.
Akisoma taarifa kuhusu maadhimisho hayo katika mkutano wa waandishi wa habari Kisiwani Pemba, huko ukumbi wa (TAMWA) Mkanjuni Chake chake, Katibu wa Klabu hiyo Khalfan Amour Mohamed alisema, bonanza hilo litahamasisha ushiriki wa wanawake katika mazoezi.
"Bonanza hilo linatarajiwa kuchezwa michezo ya aina tatu ikiwemo mbio za magunia, mazoezi ya viungo na mchezo wa kuvuta kamba, kuanzia Julai 20 hadi Julai 28 mwaka huu, viongozi wa serikali na taasisi watashiriki matembezi kuanzia Madungu hadi uwanja wa michezo Gombani", alisema.
Alieleza, kuelekea shamra shamra za kilele cha maadhimisho hayo, waandaaji wa bonanza hilo watapita skuli na katika shehia mbali mbali kuhamasisha usawa wa kijinsia katika michezo pamoja na kuwafundisha wanafunzi kujikinga na ukatili wa kijinsia GBV.
Aidha alisema, kuanzishwa kwa klabu hiyo mafanikio mengi yamepatikana ikiwemo kuimarika kwa afya za wanaklabu, lakini wanakabiliwa na changamoto ikiwemo kutokuwepo miondombinu rafiki ya kufanyia mazoezi Kisiwani Pemba hususani kwa wanawake.
Kwa upande wake, Mratibu wa chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania (TAMWA) Pemba Mussa Said, aliwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya maadhimisho hayo kwa lengo la kuunga mkono taasisi hizo pamoja na kuacha dhana potofu ya kwamba michezo ni uhuni.
"(TAMWA) Zanzibar kwa kushirikiana na Gombani fitness Clabu pamoja na wenzetu wa shirika la Bima tumeandaa bonanza la michezo kwa lengo la kuhamasisha masuala ya michezo kwa kuzingatia usawa wa kijinsia", alisema.
Akizungumza kwa niaba ya Meneja wa shirika la Bima Zanzibar ofisi ya Pemba Khatib Bakar alisema, lengo la Bima ni kumrejesha mtu katika hali yake hivyo, aliwashauri wanamichezo kukata bima ambazo zitawarejesha pale ambapo walikua kabla ya kupata majanga.
Jumla ya washiriki 500 kutoka maeneo mbali mbali ikiwemo Pemba, Unguja na Tanga wanatarajiwa kushiriki katika maadhimisho hayo ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni "WEKEZA KATIKA MAZOEZI NA MICHEZO KWA JINSIA ZOTE".
MWISHO.
Comments
Post a Comment