KWA MARA NYENGINE SERIKALI YAAHIDI SHERIA KUPELKWA BARAZANI
NA ASIA MWALIM
KATIBU Mtendaji wa Tume ya Utangazaji Zanzibar, Suleiman Abdallah Salim, amesema licha ya mchakato mrefu wa sheria namba 5 ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magaazeti na Vitabu ya mwaka 1988 na marekebisho yake namba 8 ya mwaka 1997, inatarajiwa kufikishwa baraza la wawakilishi.
Alisema tayari sheria hiyo imewasilishwa kwa mwanasheria Mkuu na inategemewa kuwasilishwa katika baraza la wawakilishi katika kikao kinachokuja.
Aidha alisema baada ya kumaliza kikao cha bajeti katika baraza la wawakilishi sheria hiyo itasomwa kwa mara ya kwanza barazani hapo kwani hatua iliyofikia inaridhisha.
"Ni vyema wadau kuendelea kuwa na subira ili kuona mchakato wa sheria hiyo unamalizika kwa mafanikio, licha ya kuchukua muda mrefu kwani sheria hiyo imeshapita katika hatua mbali mbali na sasa inaridhisha" alisema.
Akizungumza sheria namba 7 ya mwaka 1997 ya Tume ya Utangazaji Zanzibar, na marekebisho yake namba moja ya mwaka 2010, alisema sheria hiyo imeanza kufanyiwa mchakato na tayari ipo katika kamati tendaji na kamati ya viongozi wa wizara.
"Tumeshakutana na wadau mbali mbali kutoa maoni na tayari mchakato huo umewasilishwa katika kamati tekelezaji na hatua nyengine zitafuata ili kukamilisha" alisema.
Akizungumzia kuhusu sera ya Utangazaji, alisema sera hiyo ipo kwa makatibu wakuu na ikitoka hapo itapelekwa kwa wadau ili kukamilisha hatua zinazoendelea.
Katika maadhimisho hayo Mratibu wa Baraza la Habari Tanzania upande wa Zanzibar Shifaa Said, aliomba ufafanuzi kwa viongozi wa wizara hiyo, juu ya kupatikana sheria mpya za habari ambazo waliahidiwa kuwa ziko njiani katika vikao mbali mbali walivyowahi kufanya ikizingatiwa imekuwa ni muda mrefu.
Shifaa alisema, muda mrefu umepita na hakuna matumaini yoyote ya mabadiliko ya sheria zilizopo ambazo zinakwaza uhuru wa habari na kuathiri tasnia hiyo ni vyema kufanyiwa marekebisho ya haraka kwa maslahi ya umma.
Aliomba serikali kutoa ufafanuzi wake juu ya suala hilo kwani mara kwa mara wamekuwa wakikumbushia serikali namna gani sheria zilizopo zinavyo athiri uhuru wa kutoa na kupata maoni hapa nchini.
Maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari duiani, yameshirikisha wadau na waandishi wa habari mbali mbali, ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni "Uandishi wa Habari na Changamoto za mabadiliko ya tabia nchi"
Itakumbukwa kuwa, mwaka jana Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi alisema kilio cha Waandishi wa Habari amekisikia na kwamba karibuni sheria hiyo mpya itawasilishwa katika baraza la wawakilishi.
Rais Mwinyi alisema, serikali inafahamu umuhimu mkubwa wa vyombo vya habari vilivyopo nchini katika kuhamasisha mambo mbali mbali, hivyo kilio cha Waandishi wa Habari amekisikia na kwamba karibuni sheria hiyo mpya itawasilishwa katika baraza la wawakilishi.
Aidha alisema serikali ipo njiani kuzirekebisha sheria zenye mapungufu ikiwemo sheria ya habari ili waandishi watekeleze majikumu yao kwa uhuru na kwamba sheria hiyo mpa itatokana na upande wa serikali na maoni ya wadau wa habari.
Comments
Post a Comment