WANAWAKE WENYE ULEMAVU WATAKA NAFASI ZA MAJIMBO.
NA ASIA MWALIM
WANAWAKE wenye ulemavu wa aina tofauti wameeleza namna wanavyotamani kuipata haki yao ya kuwa viongozi kupitia nafasi za majimbo, jambo ambalo bado ni changamoto kwao.
Jamila Borafya, Mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) alisema kundi hilo lina uwezo wa kuogoza nafasi yoyote ile ikiwemo ya uwakilishi au ubunge huko majimboni, sio tu nafasi za viti maalumu.
"Nafasi tunazozitaka za majimboni, sio za viti maalumu pekee, tunataka kuongoza kwani uwezo na uzoefu tunao wakutosha" alisema.
Alisema ifike wakati wagombea wenye ulemavu wanapojitokeza na kufikia asilimia sawa na makundi mengine, basi wapewe kipaumbele wanawake na zaidi kuzingatia watu wenye ulemavu.
Alisema changamoto kubwa ni kutoka kwa vyama vya siasa ambavyo havijaona umuhimu wa kundi hilo kuwasimamisha majimboni ili kuchaguliwa na wananchi.
"Vyama vya siasa bado havijaona umuhimu wa kusimaisha watu wenye ulemavu majimboni, hili linatuumiza sana tunataka usawa wenye hadhi sawa ndani ya vyama vyetu kupitia nafasi za kuchaguliwa na wananchi" alisema.
Aisha Ali Abdallah, kutoka Jumuiya Wasioona Zanzibar (ZANAB) wilaya ya Chake chake Pemba, alisema ushiriki wao katika kugombea nafasi za uongozi ni mzuri, wanajitolea lakini bado vyama vya siasa vinawabana kuwapa nafasi.
"Binafsi nilishiriki kugombea nafasi ya uwakilishi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, sikupata hiyo nafasi wala hakuna linalotendeka" alisema.
Kikwazo kimoja wapo ni vyama vya siasa kushindwa kuona umuhimu wa kundi hilo na kuwapa kipaumbele hadi sasa, hakuna kiongozi mwenye ulemavu upande wa Pemba, hivyo kuwapa changamoto ya kutatua matatizo yao kwa wakati.
Adil Mohammed Ally, Mratibu Jumuiya ya Wasioona Zanzibar (ZANAB), alisema watu wenye ulemavu wana himili kuongoza nafasi za majimbo, ipo haja kwa vyama vya siasa kuzingatia watu wenye ulemavu kugombea nafasi hizo, ili nao kupata haki yao ya kikatiba.
Aliomba Tume ya uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kuweka sheria madhubuti na msisitizo maalumu kwa vyama vya siasa ili kupewa kipaumbele kundi hilo pale watakapojitokeza kwenye majimbo.
Hata hivyo aliwataka watu wenye ulemavu kujitokeza kwa wingi majimboni 2025, kwani jamii imebadilika na baadhi ya maeneo tayari yamerekebishwa ikiwemo mifumo wa kupiga kura kwa watu wenye ulemavu.
Mwantatu Mbarouk Khamis, Kiongozi mwenye ulemavu Baraza la wawakilishi, alieleza haja ya viongozi wa vyama vya siasa kuwaunga mkono watu wenye ulemavu kwa kuwapatia nafasi za majimboni ili kuengeza idadi yao ndani ya vyombo vya kutolea maamuzi.
Aliongeza kuwa Katika baraza la wawakilishi kuna viongozi watatu tu, ambao wote wamepata nafasi za viti maalumu na sio kupitia uchaguzi wa majimbo, jambo ambalo linawakosesha fursa sawa.
Alisema nafasi zote tatu zimetoka kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM, ni jambo la kuigwa na vyama vyengine ili kuunga mkono kundi hilo kuonesha uwezo wao.
"Mwanamke hasa mwenyewe ulemavu anauchungu wa kusaidia jamii yake kupata maendeleo, hakuna sababu ya kuweka matabaka kupata nafasi za majimbo kati yetu, sote ni viumbe hatujakamilika, kila mtu ni mlemevu mtarajiwa" alisema.
Kwa mujibu wa ripoti ya viashiria muhimu vya kijamii, uchumi na mazingira kutokana na matokeo ya, sensa ya watu na makaazi mwaka 2022, ngazi ya mkoa inaonesha kuwa Zanzibar, watu wenye ulemavu kuanzia umri wa miaka 7 na kuendelea, ni watu 114 kwa kila 1000 .
Ripoti hiyo inaonesha idadi ya watu wenye ulemavu imeongezeka kwa watu 39 kwa kila 1,000 kati ya sensa ya mwaka 2012 na sensa ya 2022.
Sheria zilizopo zinaeleza kuwa watu wenye ulemavu wanahaki ya kuchagua na kuchaguliwa kama watu wengine, hakuna sababu ya kunyimwa nafasi kwenye nafasi za maamuzi na uongozi.
Kwa mfano katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, katika kifungu 21(2) kila mzanzibari anayo haki na uhuru wa kushiriki kwa ukamilifu katika kufikia uamuzi juu ya mambo yanayomuhusu na yanayohusu taifa lake na kupata nafasi.
Katiba hiyo katika marekebisho ya 2010 imeeleza wazi kuwa katika kifungu nambari 67 (1) kuwa kutakuwa na wajumbe wa baraza la wawakilishi wanawake kwa idadi ya asilimia 40 wa wajumbe wote wa kuchaguliwa katika majimbo.
Takwimu za umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa takriban asilimia 15 ya watu wote duniani ambao ni zaidi ya watu Bilioni moja ni wenye ulemavu, wengi wao wakiwa ni wanawake.
MWISHO
Comments
Post a Comment