MWANAMKE ANAESIMAMIA NA KUIMARISHA SEKTA YA UCHUMI WA BULUU
.
NA ASIA MWALIM
UBORESHWAJI wa Miuondombinu ya baharini ni moja wapo ya kigezo cha kuongezeka thamani ya bidhaa za baharini ikiwemo biashara ya samaki na mazao mengine ya baharini
Kuwepo miundombinu pekee haitoshelezi ikiwa hakuna kiongozi mzuri na imara wa kuonesha njia sahihi ya kutumia fursa za hizo na kupata mafanikio.
Miongoni mwa malengo ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kusimamia kwa ufanisi fursa za bahari na mazingira yake ili kuchangia ustawi wa uchumi kwa mtu mmoja mmoja wakiwemo wanawake na taifa kiujumla .
Hii ni pamoja na kutekeleza malengo ya ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2025 na kuhamasisha wanawake katika harakati za kiuchumi, kijamii na demokrasia ili kukuza fursa za uchumi wa buluu.
Mwaka 2021, wananchi wa jimbo la Malindi walimchagua bibi Khadija Saleh Ali, kuongoza nafasi ya udiwani jimbo la Malindi, ambae hadi sasa anasimamia na kuimarisha shughuli za uchumi wa buluu.
Mwanamke huyo alipewa ridhaa na wananchi, jambo ambalo limedhihirisha kuwa maendeleo hayachagui jinsia na kuonesha wanawake ni watu muhimu katika siasa, uchumi na maendeleo ya jamii nchini kote.
Mfano wa miundombinu ya baharini iliyoimarishwa nchini ni diko la samaki Malindi, mkoa wa mjini Magharibi Unguja, jimbo la Malindi kichama wilaya ya Mjini.
Mama huyo, ametekeleza kwa vitendo dhana ya uchumi wa buluu kwa kusimamia ujenzi wa soko la samaki Malindi ili wananchi kukidhi matakwa ya soko la ndani na nje ya nchi.
Kazi anazofanya mwanamke huyo imethibitisha kuwa wanawake wana uwezo mkubwa wa kutumikia nafasi mbali mbali za uongozi na maamuzi ndani ya serikali, chama, familia na jamii kiujumla.
Bibi Khadija alionesha nia yake mapema ya kutaka kuongoza kwa kuanza kujipima kwa kugombea nafasi mbali mbali kuanzia tawi, wilaya, jimbo, Mkoa hatimae kuona ni wakati mzuri wa kuingia ngazi ya taifa kupitia nafasi ya udiwani.
Licha ya kuwa kiongozi mwanamke anahakikisha anasimamia sekta ya uchumi wa buluu ambao umekua na kufikia takriban asilimia 80 ndani ya jimbo hilo.
Kwa kua yeye ni mwanamke jasiri anahakikisha Wanawake wanapata fursa kwenye sekta tofauti ikiwemo biashara katika eneo hilo la diko la malindi kwa lengo la kuimarisha uchumi wa buluu.
Diko la samaki Malindi lina wafanyabiasha wasiopungua 263 waliosajiliwa kati yao wanawake 17 na wanaume 246.
Akizungumzia kuhusu kuengeza ushiriki wa wanawake katika diko hilo alisema kwa sasa wanawake wengi wameimarika na kujishughulisha na kazi mbali mbali hivyo matarajio yake ni kuona wanawake wanaengezeka eneo hilo.
Alisema baadhi ya tabia zilizomjenga hadi kufikia nafasi hiyo ya uongozi ni malezi ya wazazi wake na kuipenda siasa tangu akiwa mtoto mdogo na msukumo zaidi aliupata kwa mama yake ambaye wakati huo alikua Mwenyekiti wa tawi la CCM Kiponda.
Tabia nyengine ni mashirikiano mazuri baina yake na wanajamii na ndio anapofanikiwa kupata ari ya kuongoza na nguvu ya kukabiliana na changamoto zinazojitokeza.
Kabla ya nafasi hiyo aliwahi kuwa na nafasi tofauti ikiwemo Mwenyekiti tawi, Katibu tawi Kiponda ,Mwenyekiti wa vijna Jimbo la Malindi, Mjumbe baraza kuu taifa, Mjumbe Mkutano mkuu UWT Mkoa na Mjumbe kamati ya siasa.
Alieleza kuwa, licha ya Ujenzi wa diko la samaki malindi, wilaya hiyo pia imefanikiwa kujenga soko la kibanda Maiti, na kulifanya soko la darajani kuwa lenye hadhi ya kisasa.
Ndani ya miaka mitatu, tangu kushika nafasi hiyo, serikali imefanikiwa kujenga hospitali kubwa eneo la Lumumba, ujenzi wa barabara, na kuboresha usafi wa mazingira hasa maeneo ya mjini.
Alitaja maendeleo mengine ni ujenzi wa skuli mbali mbali, mikopo kwa wajasiriamali, na kusimamia upachikwaji wa taa za sola 40 katika maeneo ya mjini, ambapo mara nyingi wageni hufika eneo hilo.
Hata hivyo aliwapongeza viongozi wakuu wa nchi kwa hatua wanazochukua, na kualiwataka wa Tanzania, kumuunga mkono Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan katika suala la mkataba wa bandari, ambao umelenga kuleta maendeleo nchini.
Khadija aliwaomba viongozi wa CCM na serikali, kumuunga mkono Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi, ili kukamilisha maendeleo aliyokusudia na ahadi zake kwa wananchi.
Msimamizi wa Diko na soko la Samaki Malindi, Daudi Haji Pandu, alisema Diko hilo limejengwa kwa muonekano wa kisas na kuweka sehemu ya ujenzi wa gati, Ujenzi wa jengo jipya la biashara ya Samaki, ofisi na mkahawa na Ukarabati wa soko la zamani kuwa la kuhifadhia Samaki.
Alitaja huduma zinazopatikana kwa siku ni maeneo 6 ya shughuli za mnada, meza ndogo 141 vibaraza kwa wauzaji wadogo wadogo, maeneo 13 ya kuchakatia samaki, eneo la maegesho ya vyombo vya uvuvi zaidi ya 390, huduma za vyoo kwa wanawake na wanaume.
Alisema Matarajio yao ni kufikia wafanyabiashara wapatao 6500 watakao tumia eneo salama kwa ajili ya biashara zao kwa lengo la luluza sekta ya uchumi wa buluu nchi.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania, (UWT)wilaya ya mjini, Buluu Saleh, aliwataka viongozi na wanachama wa wa CCM kusema mazuri na maendeleo yanayofanywa na viongozi.
Alimpongeza diwani huyo mwanamke kwa utekelezaji wake mzuri jambo ambalo litasaidia kuziba midomo ya wapinzani wasiopenda maendeleo .
Naibu Meya Baraza la Manispaa mjini Khadija Ame Haji, alisema kupitia diko samaki Malindi kuimarika Mapato yamengezeka, pia serikali imetenga takriban milioni miatano kwa ujenzi wa soko la kibanda Maiti, na kuwapeleka wafanyabiashara kwa kuweka utaratibu wa kulipia vitambulisho kwa mwaka elfu Thelathini.
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi jimbo la Malindi, Dk. Yomba Ali Juma, alisema utekelezaji wa viongozi wa jimbo hilo umefikia asilimia 80 na wanatarajia kupata maendeleo zaidi ya hapo kutokana na kuimarishwa sekta ya uchumi wa buluu.
Wafanyabiashara diko la samaki Malindi walisema uimarishwaji wa miundombinu hiyo na kupaya viongozi imara wanaowasimamia kuna chochea maendeleo katika sekta ya uchumi wa buluu ambao ni miongoni mwa vipaumbele vya serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Dk.Hussein Ali Mwinyi.
Dhamira ya mwanamke huyo ni kuwa mfano wa kuigwa kama wanawake wengine wanaofanya vizuri kweye nafasi za uongozi ikiwemo balozi Amina Salum Ali Mwenyekiti wa bodi ya Takwimu Zanzibar, Anna Makinda Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, hivi karibuni amepata kiti cha urais umoja wa mabunge duniani.
Kwa kuzingatia kazi anayofanya mwanamke huyo katika kipindi cha kushika nafasi ya udiwani ni wazi kwamba huu ni mfano mwengine wa kuuzingatia wa uongozi bora wa mwanamke.
MWISHO
Comments
Post a Comment