MAJUKWAA YA SIASA YAHUSISHWA NA RUSHWA YA NGONO KWA WANAWAKE WANAOTAKA UONGOZI.


NA ASIA MWALIM 
MAJUKWAA ya kisiasa yanatajwa kuwa ni mojawapo ya vikwazo vinavyosababisha wanawake wasifikie malengo yao ya kupata nafasi za uongozi, kama udiwani, uwakilishi, ubunge hata urais.

Hayo yameelezwa na wanawake tofauti waliojitokeza kugombea nafasi za uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 katika nafasi mbali mbali kupitia vyama vyao.

Walisema Rushwa ya ngono ni miongoni mwa vikwazo vinavyowakabili baadhi ya wanawake wanapojitokeza kugombea nafasi za uongozi na hatimaye kuvunja ndoto yao ya kuitumikia jamii, ambayo ipo kikatiba.

Aidha walisema sio kitu rahisi kuliweka hilo hadharani kwa vile sio sera ya vyama vyao, bali ya mtu mmoja mmoja, mwenendo huo umeathiri matokeo ya wao kusonga mbele.

Thuwaiba Jeni Pandu (32) Mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) alisema rushwa ya ngono bado ni kikwazo  kikubwa kinachowakuta baadhi ya wanawake wanaotaka nafasi za uongozi Zanzibar. 

"Nikiri kuwa changamoto hiyo ipo na binafsi imenikuta katika harakati za uchaguzi wa mwaka 2020 nilipogombea uwakilishi kupitia kundi la vijana” alisema.
 
Lakini licha ya kukabiliwa na tatizo hilo hakuripoti popote na badala yake kwa mshangao mkubwa wapo watu wake wa karibu waliomshawishi kukubali, lakini akawaambia ila hilo.
 
Alisema aliyachukulia madai ya ngono kama changamoto katika harakati za kugombea uongozi na kuona umuhimu wa kuwa imara na kuendelea kupambana.

"Wanawake wanapopata tatizo waichukue hali hio kama angalizo la umuhimu wa kuwa mkakamavu na sio kukata tamaa au kuacha kugombea kwani kigezo cha uongozi sio ngono, bali uwezo wa wa kuongoza" alisema.

Bahati Khamis, kutoka Chama Cha CUF, alisema rushwa ya ngono ipo katika uchaguzi na miongoni mwa wanaotengeneza mazingira hayo ni baadhi ya viongozi ambao hawataki kutambua umuhimu wa uwakilishi wa nusu kwa nusu katika vyama na taifa.
 
"Kinacho turudisha nyuma wanawake ndani ya vyama, pale ukikataa kutoa rushwa ya ngono wapo viongozi wanaochukulia kama sababu ya kutokuunga mkono na kukupa sifa mbaya ambazo huna ukaribu nazo" alisema.
 
Alisema mwanamke anapojitokeza kuwania uongozi wananchi wanamkubali, lakini tatizo la rushwa ya ngono linasababaisha safari ya kugombea kuishia ngazi za chini na ndio maana wapo wanaochukua fomu na hawazirejeshi.

Mratibu wa Mradi wa Kuinua Wanawake Katika Uongozi (SWIL) kutoka Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, TAMWA Zanzibar, Maryam Ame Chumu, alisema  wanatoa elimu kwa wanawake kuhusiana na uongozi, kuonyesha changamoto zinazojitokeza na njia nzuri za kuzikabili.
 
Alisema rushwa ya ngono inatajwa na wanawake waliojitokeza kuwania uongozi, lakini changamoto ni kushindwa kuripoti kutokana na aibu au hofu ya kukosa nafasi.
 
Alisema wanawake wengi hawajatambua nafasi za uongozi kuwa ni haki yao ya kikatiba na wanastahiki kuzipata bila ya kuwepo uhusiano wa ngono au rushwa nyengine.
 
Mkurugenzi wa Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Jamila Mahmoud Mussa, alisema Jumuiya imepokea ksesi za aina hio kwenye mikutano ya kijamii, lakini hakuna muamko wa kuripotiwa sehemu husika.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo, Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Abeda Rashid Abdallah, alisema tetesi za rushwa ya ngono kwa wanawake zipo na hilo limethibitishwa na wawanawake wa vyama tofauti.

Alisema walipofuatilia tatizo waligundua changamoto kubwa iliyopo nikukosa takwimu za kutosha kwa sababu wanawake walishindwa kuripot ikutokana na kuona aibu na kudharaulika katika jamii.
 
Alisema hakuna muamko wa kuripoti kesi hizo, ni vizuri kuwepo mabadiliko kwa wanawake  kupaza sauti zao juu ya tatizo hilo na kuacha aibu ilikufikia usawa wa nafasi hizo bila ya vikwazo kutoka kwa wanaume wasiopenda maendeleo.
 
Aliwataka wanawake wasivunjike moyo na badala yake wajifunze na kuahidi kwamba wizara kwa kushirikiana na taasisi mbali mbal inatarajia kukuwatunisha wanawake wanaojikita katika harakati za uongozi ili kusikiliza changamoto zao na kuona vipi watazitatua wakati tunaelekea uchaguzi wa 2025.
 
Aliwataka wadau wa wa taasisi mbali mbali kushirikiana na serikali kupiga vita rushwa ya ngono nchini.

Ofisa uhusiano wa Mamlaka ya kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA), Mwanaidi Suleiman Ali, alisema ni vyema wanawake wanaojitokeza kuwania uongozi kuepuka vishawishi vya rushwa ya ngono ili kuwa imara na jasiri wanapotaka kugombea  uongozi.
 
Alisema ana imani wanawake wengi wanaweza kupambana na rushwa ya ngono na kuwataka wajizatiti kuhamasishana ili kila mmoja kuwa imara na uwezo wa kukabiliana na hali hiyo.
 
Alifahamisha kuwa wapo wanaume wanaoutumia mwanya huo ili kuwavunja moyo wanawake na  kusitiza ni vyema kukitokezea tatizo kujitathmini na kuwa imara kukataa ngono na kuwahamasiha wengi wasikubali kupoteza utu wao ili wawe viongozi.
 
“Uzoefu unaonesha wanawake ndio waathirika wakubwa wa matukio hayo na  sio katika masuala ya kisiasa hata kiuchumi na wamekuwa wakirudishwa nyuma na kushindwa kufikia malengo yao,”aliongeza.
 
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Kuzuia rushwa na uhujumu uchumi Zanzibar ZAECA waathirika wakubwa wa rushwa ya ngono katika uchaguzi ni wanawake na baadhi yao kushindwa kukabiliana nayo na kupata athari mbali mbali katika maisha.
 
Akizungumzia kesi zinazohusiana na rushwa ya ngono alisema ofisi haijapokea kesi zinazohusu uchaguzi 2020, hali hiyo ni kutokana na muhali wa wanawake na kuhofia aibu.
 
Mkurugenzi wa Uchaguzi Zanzibar, (ZEC)Thabit Idarous Faina, alisema Tume haijawahi kupokea tuhuma za rushwa ya ngono na kwamba kazi yake ni  kupokea maombi ya wagombe waliopitia mchakato katika vyama vyao.

Aidha tetesi hizo kama zipo kwa baadhi ya vyama basi, labda kutoka katika ngazi za teuzi ambapo teuzi hizo hufanyika ndani ya vyama vyao. 

Katika uchaguzi wa mwaka 2020 kati ya wagombea 32 nafasi ya Urais Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanawake watano tu walijitokeza na hata mmoja hakuwemo katika nafasi ya wagombea watano waliopitishwa.
Alibainisha kuwa wanawake wengi wana uwezo wa kuongoza na wanatamani kushika nafasi hizo, lakini rushwa ya ngono inawarudisha nyuma.
 
Nafasi nyingi zinashikwa na wanaume kwa sababu wanawake wengi hawapo tayari kujiingiza katika rushwa ya ngono na hii itapelekea kuwa kazi ngumu kufikia usawa wa nafasi za uongozi kati ya wanaume na wanawake. (yaani asilimia 50 kwa 50)
 
MWISHO

Comments

Popular posts from this blog

BAJAJI WAMLILIA RAIS DK MWINYI PEMBA ,WAOMBA MSAADA KWAKWE WASEMA WAMECHOSHWA NA HILI KUTOKA MAWASILIANO

Masheha wanawake wa Wilaya ya Magharib B walivyoleta mabadiliko na maendeleo kwenye shehia zao.

MPANG0 MKAKATI JUMUISHI WA JINSIA KATIKA MICHEZO UTEKELEZAJI WAKE UZINGATIWE.