KASI YA WANAWAKE AWAMU YA NANE IMEONGEZA MAENDELEO.


NA ASIA MWALIM 
JUHUDI za mwanamke katika safu ya uongozi zilionekana mapema tangu wakati wa kupigania uhuru wa Visiwa vya Unguja na Pemba na hadi sasa zinaendelezwa.

Mfano mzuri wa mwanamke aliyejitoa wakati wa Mapinduzi ya Zanzibar ni Bibi Fatma Karume, mke wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, marehemu sheikh Abeid Amani Karume.

Licha ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 kuzaa matunda kutokana na ushiriki wa wanawake katika harakati mbali mbali za uongozi hadi sasa wanawake wameonesha uwezo wao kwenye nafasi za uongozi wanazopata.

Wakati huu hatua kubwa iliofanyika ni kuona usukani wa kuiongoza Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania sasa unashikwa na mwanamke, Mama Samia Suluhu Hassan.

Kubwa zaidi ni kwamba Mama Samia sio tu anaimudu kazi ya kuliongoza taifa, bali mwenye uwezo, hekima, busara na jasiri wa kufanya maamuzi magumu ambayo yanabidi yafanyike ili taifa lisonge mbele kujitafutia maendeleo.

Zanzibar nayo kwa mara ya kwanza imepata Muhandisi mwanamke, Zena Ahmed Said, ambae ni Katibu Mkuu kiongozi Katibu wa Baraza la Mapinduzi kupitia serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Hilo limedhihirika kutokana na nchi hizo kusaini mikataba ya kikanda na Kimataifa kwamba itazingatia usawa wa kijinsia kati ya wanawake na wanaume katika uongozi na ngazi za maamuzi.

Hata hivyo serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, awamu ya nane na zilizotangulia zinatambua na kuthamini mchango wa wanawake kwa kuwapatia nafasi mbali mbali ikiwemo Mawaziri, Naibu Waziri , Makatibu wakuu, Wakurugenzi na nyenginezo.

Katika Baraza la Mawaziri awamu ya tano liloanza Oktoba 25 mwaka 1990 hadi Oktoba 2000 chini ya Rais Salmin Amour Juma lilitambua umuhimu wa wanawake na kuwapa nafasi katika baraza hilo.

Ndani ya baraza lenye viongozi 18 kati yao wanawake walikua wanne, katika nafasi ya Mawaziri na Manaibu waziri ambao walitumikia nafasi hizo kwa uweledi wa hali ya juu.

Kwa upande wa Mawaziri wanawake awamu hiyo ni Amina Salum Ali, Msimu A. Hassan na Rufea J. Mbarouk huku Naibu Waziri akiwa ni Asha Bakari Makame wakiwa katika sekta tofauti.

Aidha Baraza la Mawaziri awamu ya sita liloongozwa na Rais Amani Abeid Karume, kuanzia mwaka 2001 hadi 2010 lilikua na viongozi  22 ambapo kati yao wanawake walikua wanne 4.

Wanawake waliopata nafasi za Mawaziri katika baraza hilo ni Zainab Omar Mohammed, Samia Suluhu Hassan, Asha Abdallah Juma na Naibu Waziri ni Shawana Bukheti Hassan.

Wakati awamu ya saba 7 ilianza mwaka 2011 hadi 2020, baraza la Mawaziri lililo ongozwa na Rais mstaafu Dk. Ali Mohammed Shein Mawaziri wanawake waliopata nafasi ni Amina Salum Ali, Maudline Castico, Riziki Pembe Juma, Fatma Abdulhabib Fereji, Salama Aboud Talib, Dkt Sira Ubwa Mamboya na Zainab Omar Mohammed.

Aidha Manaibu Waziri waliobahatika awamu ya nane ni Chumu Kombo Khamis, Harusi Said Suleiman, Lulu Msham Abdallah, Shadya Muhamed Suleiman, Zahra Ali Hamad, Bi Hindu Hamad na Thuwaiba Edigton Kisasi.

Wakati huu wa Awamu ya Nane inayoongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi iliyoanza mwaka 2021 mpaka sasa akiwa madarakani baraza lake la Mawaziri limejumuisha Mawaziri wanawake 9 na wanaume 12. 

Ndani ya baraza hilo idadi ya wanawake Mawaziri waliopata nafasi ni sita, nao ni Tabia Maulid Mwita, Leila Muhamed Mussa, Rahma Kassim Ali, Saada Mkuya Salum, Riziki Pembe Juma na Harous Said Suleiman.

Pia Manaibu Mawaziri wanawake ni watatu kati ya saba ambao ni Anna Atunas Paul, Salha Mohamed Mwinjuma na Zawadi Amour Nassor.

Ni wazi kuwa idadi ya wanawake kwenye nafasi za uongozi na maamuzi ndani ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  inaongezeka siku hadi siku hivyo kupata maendeleo zaidi.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi amethibitisha kuwa wanawake wana uwezo na mchango mkubwa katika kuimarisha maendeleo ya nchi. 

Kupitia risala yake wakati akiwaapisha baadhi ya viongozi wanawake wa Baraza la Mawaziri alisema, anajivunia utendaji wa viongozi wanawake aliowapa nafasi kufanya vizuri.

"Najivunia utendaji wa viongozi  wanawake katika serikali yangu, wakiwemo  mawaziri, makatibu wakuu, manaibu makatibu wakuu, wakuu wa mikoa na wilaya, wakurugenzi wa taasisi na mashirika ya umma’’.alisema.

Aliwapongeza wanawake aliowateua kushika nyadhifa mbali mbali za uongozi kwa kazi nzuri wanayofanya ambayo alisema ameridhika nayo.

Imani ya Dk. Mwinyi kwa wanawake kuonyesha uongozi bora ndio iliopelekea wanawake kuongoza wizara sita kati ya wizara 18 na manaibu mawaziri wanawake watatu kati ya saba.

Baraza hilo limefanyiwa mabadiliko mara mbili tokea lilipoundwa mara ya kwanza na Rais Mwinyi na katika mabadiliko hayo hakuna waziri mwanamke aliyemuwekwa pembeni hadi sasa.

Hapo awali Baraza lilikuwa na wizara 15 kati ya hizo wizara nne ziliongozwa na Wanawake, ni Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo iliongozwa na Tabia Mwita Maulid, Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi iliyoongozwa na Riziki Pembe Juma, Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale iliyoongozwa na Lela Mohammed Mussa na Rahma Kassim Ali aliteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi.

Mabadiliko yaliyofanywa mara ya kwanza na DK. Mwinyi ilikuwa ni faraja kwa wadau wanaopigania usawa wa kijinsia kwenye demokrasia na uongozi kwani licha ya kwamba hakuna Waziri mwanamke aliyewekwa pembeni.

Baadaye Mawaziri wawili wanawake wakaongezeka ambao, Dk. Saada Mkuya Salum aliyeshika Wizaza ya Nchi, Ofisi ya Rais Fedha na Mipango na Harous Said Suleiman aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais.

Mnamo tarehe 27 Januari, mwaka huu, Rais Mwinyi  alifanya mabadiliko ya baraza la mawaziri na kuwateua wanawake wawili kushika nafasi za Manaibu waziri.

Baadhi ya viongozi wanawake waliopata nafasi baraza la Mawaziri awamu ya nane walisema, wanashukuru kupatiwa nafasi mbali mbali za uongozi na maamuzi ndani ya serikali.

Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi, Salha Mohammed Mwinjuma, alisema anaamini uteuzi wa wanawake zaidi kushika nafasi za uongozi unatokana na kuthibitika uwezo na uweledi wa kuongoza.

Aliwataka wanawake wengine wajifunze kutoka kwa viongozi waliowatangulia na mfano mzuri ni wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mama Samia Suluhu Hassan na wanawake wengine waliowahi kuwa mawaziri au kushika nyadhifa nyengine za juu za uongozi.

Waziri wa Elimu na Mafunzoya Amali Zanzibar, Lela Muhamed Mussa, alisema hali halisi inaonesha kuwa kila mwanamke anaepata nafasi ya kuongoza anafanya vizuri ukilinganisha na makundi mengine hali ambayo inaongeza ujasiri kwa wanawake kutaka nafasi za kuongoza zaidi.

Aidha alisema kwa mara ya kwanza Tanzania imepata kiongozi mwanamke, ambae amekuwa mfano wa kuigwa ndani na nchi nyengine duniani, hivyo ni vyema kupatiwa nafasi wanawake wengi zaidi.

Aidha amezishauri taasisi mbali mbali kuwachagua na kuwapa zaidi nafasi za uongozi wanawake kutokana na juhudi zao za kazi pia kupitia sense ya watu na makaazi ya mwaka 2022, imethibitisha idadi ya wanawake ni 974,281, sawa na asilimia 51.6.  

MWISHO

Comments

Popular posts from this blog

BAJAJI WAMLILIA RAIS DK MWINYI PEMBA ,WAOMBA MSAADA KWAKWE WASEMA WAMECHOSHWA NA HILI KUTOKA MAWASILIANO

Masheha wanawake wa Wilaya ya Magharib B walivyoleta mabadiliko na maendeleo kwenye shehia zao.

MPANG0 MKAKATI JUMUISHI WA JINSIA KATIKA MICHEZO UTEKELEZAJI WAKE UZINGATIWE.