MFUMO WA KUTOA MSAADA WA HUDUMA ZA KISHERIA UBORESHWE KUPUNGUZA CHANGAMOTO ZA UDHALILISHAJI.
NA ASIA MWALIM
WADAU na wanaharakati wa masuala ya wanawake na watoto wamesema ipo haja ya kuboreshwa mifumo ya utoaji misaada ya kisheria ili kuondoa vikwazo vinavyokwamisha wanawake na watoto kupata haki zao.
Imebainikia kuwa, wapo baadhi ya watendaji wa serikali wanatumia nafasi hiyo, vibaya kwa kuwatolesha fedha wanawake wanaofika Mahakamani kutafuta matunzo ya watoto waliotelekezwa na baba zao.
Aidha, walisema kutokana na changamoto hiyo, baadhi ya familia zinashindwa kusimamia kesi hizo baada ya kuvunjika moyo, kutokana na malipo wanayotakiwa kulipa ukizingatia wana hali duni za kimaisha.
TAMWA-ZNZ ni miongoni mwa taasisi inayopigania haki za wanawake na watoto , imekiriki kupokea malalamiko hayo kwa baadhi ya wanawake waliofika katika vyombo vya sheria kwa lengo la kutafuta matunzo ya watoto.
Kwa mujibu wa sheria ya mtoto no.6 ya mwaka 2011, kifungu namba 5(1) (C) kinaeleza haki ya matunzo na malezi anayotakiwa kupewa mtoto.inaeleza wazi kuwa baba au mzazi wa kiume ana haki na wajibu aa kusimamia familia yake kupata matunzo na huduma nyengine stahiki ikiwemo chakula, mavazi elimu, na mahala salama pa kuishi ili kuepusha vitendo vya udhalilishaji kuendelea.
Akizungumza na muandishi wa Makala haya, Zaina Salum Abdallah, Afisa Kitengo cha kupinga ukatili na Udhalilishaji wa Kijinsia kutoka Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA-ZNZ) alisema bado kesi nyinyi za wanawake na watoto wanaodai matunzo zinapelekwa mahakani, sehemu ambayo hakuna huduma ya msaada wakisheria.
Aidha alisema taasisi hiyo imekua ikipokea kesi mbali mbali zinazohusiana na ukatili na udhalilishaji wa wanawake na watoto kukoseshwa haki zao ikiwemo matunzo.
Hati za madai(Legal draft) imetajwa kuwa ni moja ya kikwazo kinachokwamisha wanawake na watoto kuendelea kukosa matunzo kutoka kwa baba watoto, hali ambayo inaweza kuwaweka hatarini kukabiliwa na vitendo vya udhalilishaji.
Katika kukabiliana na tatizo hilo, wameamua kuwekeza nguvu zaidi kwa kuendelea kutoa elimu kwa jamii, kupata uelewa wa kuzitumia taasisi zinazotoa msaada wa kisheria ikiwemo kupata hati za madai ya matunzo (legal draft).
Haura Shamte, alisema miongoni mwa mikakati ya kupinga ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto ni kuhakikisha huduma za msaada wa kisheria zinapatikana kwa urahisi kwa wahanga wa vitendo vya udhalilishaji.
Wakizungumza na makala haya wanawake wanaokosa matunzo ya watoto, walisema hati za madai ya kusimamia kesi hizo bado ni changamoto kuzipata kutokana na kutoleshwa kiasi cha fedha na baadhi ya watendaji wa serikali.
Bimkubwa Khamis Haji, mkaazi wa Mpendae (30) amebarikiwa watoto 3, alisema kwa mara ya kwanza alifika Mahakama ya Kadhi Mwanakwerekwe Zanzibar, kudai matunzo ya watoto, lakini alichokikuta kwa watendaji hakutegemea.
Alisema, aliambiwa atoe kiasi cha fedha (20000) ili apatiwe hati za madai ya kusimamia kesi yake ya kupata matunzo anayotaka kutoka kwa mtalaka wake.
Mama mwengine (46) alisema mume wake hakumpa talaka badala yake alimkimbia kwenda Tanzania bara kwa miaka minne na kumuachia watoto watano (5) bila ya huduma yoyote wala mawasiliano.
Aliwalea watoto hao katika mazingira magumu na mara nyingi watoto wake waliranda ovyo mitaani na kushindwa kuhudhuria masomo, na alipofika Mahakamani kudai matunzo ya watoto, alilazimishwa kutoa shilingi laki moja (100000)kwa ajili ya kumsafirishia mumewe ili arejeshwe kutoka Tanzania bara hadi Zanzibar.
Ikiwa hali ya kutoleshwa fedha itaendelea wanawake wengi watashindwa kufungua kesi za matuzo Mahakamani kutokana na gharama wanazotakiwa kulipa na baadhi ya watendaji wa Mahakama hiyo.
VITUO VYA HUDUMA ZA SHERIA
Fatma Khamis Ali, Paraligo kutoka Zanzibar Paraligo Organization (ZAPAO) alisema kawaida wanatoa huduma ya msaada wa kisheria bure kwa kesi za udhalilishaji, utelekezwaji na hata kudai matunzo.
Alisema kesi nyingi za matunzo ya watoto zinakaa takriban miaka miwili hadi kukamilika, jambo ambalo huleta athari zaidi kwa watoto na kukosa mahitaji ya lazima, mara nyengine kuingia kwenye hatari ya vitendo vya udhalilishaji. Pia baadhi ya wanawake wanakatisha njiani, kesi hizo kutokana na kukaa muda mrefu bila ya mafanikio.
ZAPAO kwa mwezi moja hupokea malalamiko 9 hadi 11 kwa upande wa utelekezwaji na matunzo, changamoto ni kwamba wananchi bado wananchi wengi hawajui utaratibu wa kupata hati za madai .
Alisema changamoto inayojitokeza kwa wanawake wengi na jamii kukosa uelewa kuwa mchakato wa kudai matunzo, sio rahisi kama wanavyofikiria na hauwezi kukamilishiwa ndani ya siku moja.
Akizungumzia kuhusu kutoleshwa fedha kwa ajili ya hati za madai, alikiri kuwa waliwahi kupata malalamiko kwa baadhi ya wanawake wanaofika hapo kutoleshwa fedha na makarani kutoka Mahakama ambao wanatumia nafasi hiyo vibaya.
JUMUIYA YA WANASHERIA WANAWAKE ZAFELA
Mkurugenzi Chama Cha Wanasheria Wanawake Zanzibar ZAFELA, Jamila Mahmoud alisema, kulingana na kazi wanazofanya inaonesha kuwa wanawake wengi Zanzibar wanakabiliwa na tatizo la kutelekezwa na kukosa matunzo.
Alisema ZAFELA inatoa huduma ya msaada wa kisheria kwa wanawake na watoto sambamba na kutoa hati za madai bure, kwa lengo la kusaidia jamii hasa ya wanawake na watoto kupata haki zao.
Kupitia msaada wa kisheria wanaotoa alithibitisha kuwa, baadhi ya familia zinendelea vizuri bada ya kupewa elimu juu ya malezi na matunzo ya familia zao, pia wapo wanapeleka matunzo hapo ili kufikishwiwa familia zao.
IDARA YA MAENDELEO YA JAMII
Mkurugenzi Idara ya Maendeo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Siti Abasi Ali, alisema katika kuhakikisha wanawake na watoto wanapata matunzo na huduma nyengine stahiki, wizara inatumia Maafisa wilaya kupitia shehia zote 388 kutoa elimu, ili wanawake na jamii kuwa na uelewa wa kudai matunzo na namna ya kupata kwa njia sahihi.
Alisema serikali imejipanga kupigania haki za makundi yote ikiwemo wanawake na watoto ili kuhakikisha wanapata haki zao kwa mujibu wa sheria za nchi.
Rasilimali kubwa ya Tanzania na Zanzibar ipo kwa watoto, pia imewekeza mambo mengi na kuwathamini kwa kuwaangalia na kuwajali ili kupata haki zinazostahiki.
Sheria ya mtoto nambari 6 ya mwaka 2011, imeeleza haki za mtoto na namna ya kupatiwa matunzo, wazazi wanapaswa kutoa matunzo ya watoto wao.
Tathmini inaonesha kuwa kesi za utelekezwaji na kukosa matunzo ni nyingi kwa sababu asilimia kubwa ya wanawake walioachika hawapewi huduma ingawa mara nyengine hutokea kwa wanandoa.
MAHAKAMA YA KADHI
Kadhi Dhamana Wilaya ya Mwanakwerekwe Omar Shekha Khamis alisema, wakati huu Mahakama haina utaratibu wa kutoa hati za madai, badala yake hufungua jalada la mashitaka baada ya mdai kupeleka hati hiyo.
Alisema kawaida huwaelekeza wanawake wanaodai matunzo kwenda ZAFELA au, kituo chengine kinachotoa huduma za sheria kwa ajili ya kupatiwa hati hizo ili kufungua kesi.
Akizungumzia muda wa kukamilika kesi hizo alisema, zipo kesi zinazomalizika kwa muda mfupi (siku moja) na nyengine zinazohitaji upelelezi na taarifa za kidaktari kuchukua takriban miezi 2.
Akizungumzia kuhusu malalamiko ya kesi hizo kuchelewa alisema utaratibu unaotumika unazingatia ukubwa wa tatizo na namna ya uhudhuriaji wa wahusika wa kesi, Mahakama haiwezi kutoa adhabu kinyume na taratibu.
Alisema kawaida husikiliza kesi 3 hadi 4 kwa siku, ambapo kwa mwezi September 2023, Mhakama imepokea kesi 4 za malezi ya watoto na kesi 12 za matunzo.
Pia kwa mwezi October 2023, kesi za malezi zilikua 5 na upande wa matunzo kesi 7.
Kaadhi dhama alisema, kwa sasa mahakama hiyo ina kesi zisizopungua elfu moja na miatatu kwa makosa mbali mbali ya mdai yanayofikishwa.
Akizungumzia kuhusu malalamiko ya baadhi ya watu kutoleshwa fedha na makarani wa mahakama hiyo alisema, ofisi haijawahi kupokea wala kusikia malalamiko hayo hata mara moja.
Pia alisema sula la kutoa hati za madai limekatazwa na kupigwa marufuku Mahakamani hapo, kwani ni kinyume na utaratibu wa sheria.
Aidha aliwataka waumini wa kiislamu kusoma zaidi dini yao kwani imetoa mafundisho katika kila hatua ikiwemo malezi ya watoto, matunzo hali ambayo itasaidia kupunguza migogoro ya ndoa na familia kiujumla.
MAHAKAMA KUU
Kwa mujibu wa takwimu kutoka Mahakama Kuu Zanzibar, zilionesha kuwa kesi 420 za makosa mbali mbali zilifunguliwa kutoka julai hadi June 2022, kati ya hizo kesi 170 zimefutwa na kuachiwa huru 39 watuhumiwa wmefungwa.
Imeeleza kuwa matukio yalioshika kasi kwa sasa ni unyanyasaji wa wanawake katika ndoa na kukosa matunzo na mambo mengine.
IDARA YA KATIBA NA SHERIA
Afisa Sheria Idara ya Katiba na sheria Zanzibar, Salma Suleiman alisema, Idara inaridhishwa na utendaji wa kazi za paraligo na wasaidizi wa sheria katika kutoa huduma ya msaada wa kisheria kwa jamii.
Alisema kwa kiasi kikubwa Paraligo wanafanikisha usimamizi wa hati za madai kutokana na ushuhuda wa wananchi jinsi wanavyoeleza namna walivyofanikiwa.
Aliitaka jamii kitumia wasaidizi wa sheria ili kupata huduma hiyo inayotolewa bure kupitia jumuiya na taasisi mbali mbali zilizosajiliwa kila wilaya wilaya kwa upande wa Unguja na Pemba.
Alisema kazi kubwa ya Idara ni kuratibu, kusimamia, kuendesha na kutoa msaada wa kisheria na ushauri nasihi kwa wananchi mbali mbali ikiwemo waliofanyiwa vitendo vya udhalilishaji,
Idara kupitia wasaidizi wa kisheria, ambao wapo kila wilaya wanafatilia kwa kutoa msaada wa kisheria kwa wahanga wa vitendo vya udhalilishaji mpaka kufika Mahakamani.
Alisema idara imesjili, Jumuiya 14 zanazotoa msaada wa kisheria kwa Unguja na Pemba, ingawa bado shehia ya Fundo kisiwani Pemba hazijafikiwa ipasavyo na watu hao.
TUME YA KUREKEBISHA SHERIA
Katibu wa Tume ya Kurekebisha sheria Zanzibar, Mussa Kombo Bakari, alisema serikali na taasisi binafsi wana nafasi kubwa ya kusaidia watu wenye kuhitaji msaada wa kisheria ili wanyonge kupata haki za msingi.
Alisema baadhi ya wananchi wanashindwa kudai haki zao, kutokana na changamoto mbali mbali za kimaisha ikiwemo mazingira ya umasikini, ni vyema wadau wanaoshughulika na jamii kuwasaidia wanyonge.
Aidha alisema, sheria ya msaada wa kisheria ni sheria muhimu kwa utu na thamani ya mtu, tume imeona haja ya kufanya mapitio na kuweka mazingira mazuri kwa sheria hiyo ili kila mwananchi kupata huduma hizo kwa wakati.
Serikali imekusudia kuona kila mwanachi anapata haki yake ikiwa kwa uwezo wake au kwa msaada, kama Katiba ya Zanzibar ilivyoeleza katika kifungu cha 12.6 kuwa ni miongoni mwa haki za lazima kwa watu.
Sambamba na hayo, Katibu alipongeza Ofisi ya Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala bora kwa kusaidia mchakato wa kugharamia mapitio ya sheria hiyo sambamaba na shirika la UNDP, kufanikisha hatua muhimu za maendeleo ya nchi.
Akizungumza latika kikao cha wadau wa mswaada wa kisheria Zanzibar, aliekua, Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha sheria Zanzibar, Khadija Shamte Mzee, alisema wamefanya utafiti wa sheria ya mswaada wa kisheria kwa lengo la kusaidia wananchi wanyonge wenye uhitaji wa kisheria kupata msaada kwa utaratibu unaohitajika kupunguza wanyonge kuonewa.
Alisema utafiti uliofanyika umetizama mikataba ya kimataifa, sheria na uzoefu wa nchi mbali mbali, na kuzingatia maoni ya wadau kutoka taasisi tofauti za serikali na zisizo za kiserikali.
Wakili kutoka Tanzania bara, Utti Mwangamba, alisema ni vyema wadau wa mswaada wa kisheria wawe na utaratibu wa kukutana na taasisi za serikali zenye kutoa huduma za wananchi ili kupeleka changamoto zinazokwamisha utendaji.
Comments
Post a Comment