MAMLAKA YA MAPATO ZANZIBAR ZRA YAFUNGUA JENGO JIPYA LA OFISI MKOA WA KASKAZINI PEMBA, IKIWA NI MUENDELEZO WA SHAMRA SHAMRA ZA MIAKA 3 YA UONGOZI WA DK MWINYI.
NA AMINA AHMED MOH’D- PEMBA.
WANANCHI Mkoa wa Kaskazini Pemba wametakiwa kuzidisha uzalendo katika ulipaji wa kodi mbali mbali ili kuisaidia serikali kupanga mipango mbali mbali ya maendeleo ya nchi.
Ameyasema hayo mkuu wa wilaya ya Micheweni Mgeni Khatib Yahya alipokuwa akizungumza na wananchi wa Wete kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Sada Mkuya Salum katika ghafla ya Ufunguzi wa Jengo la Mamlaka ya Mapato Zanzibar ZRA Mkoa wa kikodi Kaskazini Pemba .
Amesema wapo baadhi ya wananchi hususan ni wafanya biashara wamekuwa wakiidanganya serikali na kufanya malipo yasiostahili wakati wa uuzaji na utowaji wa risiti jambo huku baadhi yao wakishindwa kuzitoa kwa wateja wao , hivyo ni vyema kuwacha tabia hiyo na kushirikiana na serikali kupitia mamlaka hiyo katika kuongeza mapato yatakayosaidia kutumika katika uletaji wa maendeleo.
Aidha Mkuu huyo amesema kuwa Serikali ya mkoa itaendelea kuinga mkono mamlaka ya mapato Zanzibar ZRA katika kuhamasisha ulipaji wa kodi ikiwa ni pamoja na wafanya biashara kutoa na wanunuzi kudai risiti za kielectronic kwa wanaonunua bidhaa mbali mbali sambamba na kutowafumbia macho wale wenye dhamira ya kuihujumu serikali kwa kukwepa kodi.
Akizungumza Mwenyekiti bodi ya wakurugenzi kutoka mamlaka hiyo Pr. Rashid Hemed Hikman amesema mafanikio hayo ya kuongeza ofisi katika mkoa huo ni katika kusaidia kufanyika kwa ufanisi kazi za ukusanyaji wa kodi mbali mbali kisiwani Pemba .
Akizungumza Kamishna mkuu wa Mamlaka ya Mapato Zanzibar ZRA Yussuf Juma Mwenda Amesema ufunguzi wa ofisi hiyo ni muendelezo wa kusherehekea miaka mitatu ya uongozi wa Rais wa Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi katika kujenga mfumo wa kodi ambao ni rahisi kwa walipa kodi wake.
Aidha amesema mamlaka hiyo itaendelea kutoa huduma bora kwa wananchi sambamba na kuimarisha wafanya biashara ili ziendelee kukua na kuongeza mapato yatakayosaidia kufikia malengo ya serikali kuimarisha maendeleo ya nchi.
kwa Upande wake Mkurugenzi wa ZRA Pemba Jamal Hassan Jamal amesema kufunguliwa kwa jengo kutasaidia kuwaondoshea usumbufu waliokuwa wanaupata walipa kodi mkoa wa kikodi kaskazini kwa muda mrefu kutokana na kukosekana kwa ofisi hiyo ambapo amewataka wananchi wa mkoa huo kuitumia ofisi hiyo ili kujipatia huduma zote za kikodi .
Uzinduzi wa ofisi hiyo umeambatana na shamra shamra mbali mbali ikiwemo ukatajai keki, ngoma, utenzi maigizo ambapo inatarajiwa kuanza rasmi kazi zake kuanzia leo hii kwa kutoa huduma mbali mbali ikiwemo huduma za ulipaji wa ushuru wa stamp, mashine za kielectronic, Ulipaji wa kodi za majengo, Leseni, pamoja na kodi nyengine mbali mbali.
Mwisho
Comments
Post a Comment