JINSI TAMWA ZNZ INAVOANDAA JESHI LA WANAWAKE 2025


NA - MASOUD JUMA- Unguja


 KWA KIPINDIkirefu kilichopita dunia ilikua na mtazamo hasi kuhusiana na ushiriki wa wanawake katika ngazi na vyombo mbalimbali vya Maamuzi.

Katika mitazamo hiyo wapo waliomchukulia mwanamke kuwa ni mtu wa kubaki nyumbani na kulea familia tu, halikadhalika mwanamke alionekana ni mtu wa kumtunza mume na kumpa utulivu ili mwanamme apate nafasi kubwa na nzuri ya kushiriki katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo ikiwemo kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Lakini sasa dunia imefumbua macho na kukubali na kuthamini jitihada za mwanamke katika masuala ya maendeleo, kwa kipindi hichi hali imebadilika sana kutokana na jitihada kubwa iliyofanyika kwa wanawake wenyewe kuonesha uwezo wao na hivyo kufanikiwa kubadilisha mitazamo mibaya juu yao.

Kazi hiii ya kubadilisha mitazamo imefanywa na inaendelea kufanywa na wanaharakati mbalimbali wakiwemo wanaume wa mabadiliko wanaotamani kumuona mwanamke anashika nafasi za uongozi katika Nyanja za kisiasa hata kijamii.

Harakati hizi pia hufanywa na jumuiya na asasi mbalimbali za kiraia ikiwemo TAMWA ZANZIBAR.

TAMWA ZANZIBAR  ni Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania kwa upande wa Zanzibar, hii ni jumuiya ya kupigiwa mfano kwa harakati zake za kumkomboa mwanamke na kuleta mapinduzi ya kifikra kwa jamii ya kizanzibari kuwa wanawake wanaweza kushika nafasi na dhamana mbalimbali za uongozi.

Mwaka 2020 TAMWA ZNZ ilifanikiwa kupata mradi maalum wa kuwatetea wanawake ili kubadili mitazamo hasi kwa jamii juu ya uwezo wa mwanamke na pia kumpa moyo mwanamke ili apambane katika kushika nafasi kwenye masuala ya maendeleo.

Mradi huo unajulikana kwa jina la SWIL  ambapo kwa kiiengereza ni Strengthen Women In Leadership ambao tafsiri yake ni kuongeza nguvu kwa wanawake kushiriki katika nafasi za uongozi na unafadhiliwa na ubalozi wa Norway.

Kupitia mradi huo, hadi sasa zaidi ya wanawake 160 wa Unguja na Pemba wameshapatiwa mafunzo kuhusiana na masuala ya uongozi na mbinu mbalimbali za kuwasaidia kuweza kufika nafasi hiyo.

Washiriki wa mafunzo hayo walikua ni kutoka vyama tofauti vya siasa ikiwemo CCM, CHADEMA, CUF, ADA TADEA, ACT WAZALENDO, NCCR MAGEUZI, ADC, UMD, UPDPO na wengine walikua ni viongozi kutoka vyuo vikuu vilivyopo hapa Zanzibar.

Miongoni mwa changamoto kubwa iliyotajwa na washiriki wa mafunzo hayo ni kuwepo kwa tatizo la rushwa ambao miongoni mwa washiriki walokua washawahi kujitosa kwenye kugombea walisema hicho ni kikwazo kikubwa.

Kutokana na changamoto hiyo TAMWA ZNZ iliamua kwa makusudi kumualika ofisa habari wa mamlaka ya kuzuia rushwa na uhujumu uchumi bi Mwansaid Suleiman ambae aliwaasa na kuwapa mbinu washiriki hao jinsi ya kukwepa mitego mbalimbali yenye viashiria vya rushwa.

Aidha aliongeza kuwa rushwa pia hutumika kuwarubuni wao wanawake ili wawaachie nafasi hizo wanaume kwa kisingizio kuwa bado hawajakua na uwezo, wengi huwaahidi wanawake fedha nyingi ama vitu vya thamani ili wakae pembeni katika kinyang’anyiro hicho.

Alielezea aina nyengine ya rushwa kuwa ni ile ya kutumika kimapenzi na watu wenye mamlaka na uwezo wa maamuzi ndani ya vyama vyao, ili tu wawapitishe kugombea nafasi fulani.

“Watu hawa ni hatari na mafundi wa kulaghai wanawake kwa tamaa za kimwili, hujidai pia kuanzisha mahusiano lakini lengo ni lile wapate rushwa kwa ajili ya kukuwezesha, na  hii sio kweli kwani unaweza kujirahisha na usipate unachokitafuta”, alisema Mwanaidi.

Mwanaidi pia alitumia fursa hiyo kuwaasa wanawake kuacha kuona aibu na kuwaripoti wale wote wanaowadai rushwa katika ofisi za ZAECA ama kupiga namba 113 kwa ajili ya kuwasiliana na maofisa ili suala hilo liweze kushughulikiwa na mtuhumiwa kutiwa hatiani.

Wasiriki wa mafunzo hayo wanaishukuru sana TAMWA ZNZ kwa kuwaandalia mafunzo hayo kwani yanawajenga na kuwatayarisha kuwa viongozi bora.

“Mimi naishukuru sana TAMWA maana haya mafunzo yameniongezea ujasiri wa kuendelea kupambana na kushika nafasi ya uongozi” alisema Salama Jumas.

Nae Mtumwa AbdulRahman aliongeza kuwa wanashukuru mafunzo hayo yanawafumbua macho na kuwafanya kuzijua haki zao jambo ambalo linawazidishia wao kujiamini.

Nae mratibu wa mradi wa SWIL Maryam Ame amesema kuwa lengo la kuandaa mafunzo ni kuwaamsha wanawake na kuwaandaa kimbinu ili wanawake wengi waweze kuingia katika kinyang’anyiro cha uchaguzi mwaka 2025 na hatimae kufikia asilimia 50 kwa 50 katika maswala haya ya uongozi.

Maryam aliongeza kuwa matokeo ya sensa ya mwaka 2022 yameonesha wazi kuwa wanawake ni Jeshi kubwa kwani wamewazidi wanaume kwa kuwa ni asilimia 51 ya  watanzania wote, hivyo amewataka wanawake kujiamini na kujiandaa kwa mwaka 2025 huku wakiwa na kauli moja ya kukataa rushwa ya namna yoyote ile.

Mkurugenzi wa TAMWA ZNZ Dokta Mzuri Issa aliwaasa wanawake hao kuyatumia vizuri mafunzo hayo ili malengo ya mafunzo hayo yaweze kufikiwa kwa wanawake kushika nafasi nyingi za udiiwani, uwakilishi na ubunge ndani ya Zanzibar.

Mradi wa SWIL pia umewapa mafunzo waandishi wa habari zaidi ya 60 kwa ajili ya kuandika habari mbalimbali zinazohusu wanawake na namna bora ya utendaji kazi wao.

TAMWA ZNZ imejipanga na kujidhatiti kuhakikisha kuwa wanawake hawabaki nyuma katika nafasi za uongozi  na uwezo wa wanawake unaonekana katika kuleta maendeleo endelevu kwa wanawake wenyewe, watoto na jamii kwa ujumla.

Comments

Popular posts from this blog

BAJAJI WAMLILIA RAIS DK MWINYI PEMBA ,WAOMBA MSAADA KWAKWE WASEMA WAMECHOSHWA NA HILI KUTOKA MAWASILIANO

Masheha wanawake wa Wilaya ya Magharib B walivyoleta mabadiliko na maendeleo kwenye shehia zao.

MPANG0 MKAKATI JUMUISHI WA JINSIA KATIKA MICHEZO UTEKELEZAJI WAKE UZINGATIWE.