MWENYEKITI UVCCM JIMBO LA MALINDI, KIJANA MDOGO MWENYE NIA YA KUSAIDIA WANAWAKE WENZAKE KUPITIA MAJUKWAA YA KISIASA
Na- Massoud Juma, Unguja
KHAYAM Musatafa Yakuti bado anaendelea kuwashangaza na kuwastaajabisha wengi kutokana na kuwa na umri mdogo lakini kwa kuwa na uelewa, uthubutu na uhodari wa kujenga hoja katika mada tofauti za kimaendeleo hususani katika masuala ya siasa hapa Zanzibar.
Kwa sasa Khayam ana umri wa miaka 23 tu, lakini tayari ameshapata uzoefu wa uongozi tokea ana umri wa miaka nane, mwenyewe anasema alianza kuingia katika mabaraza ya watoto ndani ya shehia, baadae wilaya na hatimae kushika nafasi ya makamu mwenyekiti wa baraza la watoto la Tanzania.
Kama yalivyo malengo ya mabaraza hayo, kumjenga mtoto kuwa na uthubutu na kujiamini, hilo lilifanikiwa sana kwa Khayam, kwani katika harakati za baraza hili za kulinda na kutetea haki za watoto yeye alijifunza mengi na hatimae kuingia katika siasa ili aweze kutumia majukwaa ya siasa kutetea na kulinda haki za wanawake, vijana na watoto.
Kwa sasa Khayam ni mwenyekiti wa UVCCM katika jimbo la Mlindi, na uongozi wake unasifiwa sana kama amesaidia kuonekana nguvu ya vijana na chama katika jimbo hilo.
Ndugu Abdulhamid Mvita ni Mwenyekiti UVCCM wadi ya Kwaalinatu anamzungumzia Khayam kama kijana wa kike shupavu na mwenye maono makubwa katika kukiletea chama chao maendeleo, maendelo ya vijana lakini Zanzibar kwa ujumla, na anasema anafurahishwa sana na uongozi wake kwani unaonekana kukiletea faida chama chao cha cha CCM.
Aidha Mvita aliongeza kuwa yeye amemfahamu khayam tangu alivokua mwenyekiti wa baraza la watoto , na anakumbuka tangu enzi hizo Khayam alikua ni mtu mwenye uthubutu na anaeweza kujenga hoja.
Mwaka 2020, Khayam alishangaza jamii, kwani akiwa kijana wa miaka 20 tu alijitosa kuchukua fomu ya kugombea udiwani wa viti maalum ndani ya UWT, huu ulikua ni uthubutu mkubwa sana, wengi walimsifia na kumpa moyo wa kumsaidia ili aweze kufanikisha malengo yake, kwa kipindi hicho bahati haikua upande wake lakini alipata nafasi nzuri tu katika kinyang’anyiro hicho kwa kushika nafasi ya pili katika uchaguzi wa ndani ya chama chake.
Hiyo ilikua ni hatua nzuri sana iliyomfanya ajulikane na hivyo kupata fursa nyingi za ndani na nje ya chama kwani alijijengea heshima na kuaminiwa kuwa ni kijana mwenye uwezo na anaweza kuipeperusha bendera ya chama chake kwa uzuri kabisa.
Katibu wa UVCCM wilaya ya mjini anamzungumzia Khayam kama ni kijana anaewaunganisha vijana wenzake na kukipa nguvu Chama Cha Mapinduzi ili kiendelee kushika dola hapa Zanzibar, pia anasema ni mtu hodari na yuko haraka katika kupokea na kutekeleza maelekezo anayopewa na uongozi ulioko juu yake.
Sambamba na hayo, ndugu katibu anasema yeye binafsi anampa thamani sana mtoto wa kike na huwa anawashauri sana wajielewe, waongeze juhudi lakini pia kujiendeleza kimasomo kila wanapopata fursa ya kufanya hivyo.
Pia ametoa wito kwa wazazi kuacha fikra mgando kama siasa ni uhuni, hivyo wawape fursa na uhuru vijana wao wa kike ili kutimiza ndoto zao na hatimae wafikie malengo yao ya kuwa viongozi bora.
Khayam ametumia fursa ya mahojiano haya kuishukuru sana familia yake kwa kumpa mashirikiano makubwa katika masuala yake haya ya siasa anayoshughulika nayo.
Na anaeleza kuwa anafurahi kukuza heshma yake, kujenga mahusiano na watu wa rika, hadhi na vyeo tofauti na zaidi ni kupata fursa mbali mbali za kujifunza katika maeneo mbalimbali kupitia shughuli hizi za siasa.
Khayam pia amekishukuru sana Chama Cha Mapinduzi kwa kumpatia fursa na vile vile ameitaja uvccm kama ni tanuri la kuwajenga vijana na kuwakuza ili kuja kuwa viongozi bora hapa nchini akitolea mfano kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dokta Samia Suluhu Hassan.
Katika nafasi yake hiyo ya mwenyekiti wa UVCCM katika jimbo la Malindi, Khayam anajivunia sana kufanya mapinduzi ya kimtandao na kuufanya umoja wa vijana katika jimbo la malindi kuonekana zaidi kupitia mitandao ya kijamii kama instagram, facebook na nyenginezo.
Mwisho alimalizia kwa kuwapa moyo wasichana wenzake kuwa wanaweza hivyo waendelee kujituma na kuwa wasikivu kwa familia zao, la muhimu zaidi amewataka kujielewa na kuwa na msimamo ili waweze kufikia malengo yao.
Mwisho
Comments
Post a Comment