MWANAMKE ALIEVUNJA VIKWAZO KATIKA TASNIA YA SANAA YA MUZIKI DJ, HIJAB


Na MASSOUD JUMA UNGUJA

JINA lake halisi ni Aisha Bakary lakini anajulikana sana kwa jina lake la kazi ambalo ni HIJAB DJ, binti ambae anatokea hapa visiwani Zanzibar na kazi yake kubwa ni kupiga muziki katika maeneo mbali mbali ya burudani na starehe na amekua mwanamke wa kwanza katika kazi hiyo ya kupiga na kuongoza muziki (DJ) hapa Zanzibar.


Aisha ameamua kuvunja mfumo dume ambao umetawala katika tasnia ya muziki, na anawashawishi vijana wenzake wa kike wasizuiwe kutimiza ndoto zao eti tu kwa kujali kuwa tasnia hiyo ni kwa ajili ya wanaume.

Aisha pia kwa kupitia kazi yake hiyo mwaka 2019 amejishindia tuzo ya mwanamke wa mwaka ambayo hutolewa na shirika la Women Future ambayo ina lengo la kupongeza, kukuza na kutangaza mafanikio ya wanawake.

Aisha anasema tofauti na ilivyozoeleka kwa mavazi ya wadau wa muziki, yeye anafanya kazi zake siku zote akiwa amevaa hijabu na anafanya hivyo ili kuiwelesha jamii kubwa ya kizanzibari kuwa  hakuna ubaya kwa mwanamke kujiajiri katika sekta ya Sanaa.

Aisha anasema aliamua kutafuta kazi baada ya kumaliza masomo yake ya stashahada ya sayansi ya kompyuta kwa ajili ya kuisaidia familia yake baada ya kuondokewa na baba yao ambae ndie aliyekua msimamizi wa familia.

“mara tu baada ya kumaliza diploma yangu, niliamua kutafuta kazi ili niisaidie familia yangu baada ya kifo cha babaangu ambae ndio alikua tegemeo letu”,

Aisha anasema mwaka 2017 alianza kazi kama mtangazaji wa redio katika vituo tofauti lakini changamoto ilikua ni kucheleweshewa malipo na muda mwengine kukosa malipo kabisa.

“nilifanya kazi katika vituo vinne vya redio na televisheni lakini sijawahi kupata mshahara ambao ulinisaidia katika kuendesha familia yangu. Niliishia tu kupata  uzoefu wa kazi”.

Aisha aliongeza kuwa yeye kama mzanzibari anauheshimu sana utamaduni wetu wa kizanzibari, lakini hiyo haimzuii yeye kufanya kazi hiyo ya u DJ. Anafanya kazi maeneo tofauti ikiwemo Fumba Town, Nafasi Art Space iliyoko Dar es Salam, hotel mbalimbali za kitalii na hata maharusini.

Anasema ni ngumu sana kwa jamii na familia kuielewa na kuikubali kazi yake, kwani kazi yake hiyo inamlazimu kurudi nyumbani usiku mkubwa.

“hii bado ni changamoto lakini nashukuru Mungu, kupata baadhi ya tuzo katika tasnia hii ya burudani na baadhi ya waandishi kuja kufanya mahojiano na mie hapa nyumbani imesaidia kwa kiasi familia kulichukulia hili kwa mtazamo chanya”.

Aisha anaendelea kusema kuwa, ili kuwa dj mzuri ni lazima kujifunza kutoka kwa wengine namna wanavyofanya na pia kuwa mpenzi wa aina zote za miziki ili kuweza kukidhi mahitaji ya wateja wote.

Aisha anawaomba wazazi pamoja na jamii ya wazanzibari kwa ujumla kutumia vizuri vipaji walivyonavyo watoto wa kike kwa kuwafungulia milango katika sekta mbalimbali ambazo wenyewe wasichana watachagua kufanyia kazi.

“wanawake wengi wa kizanzibari wameekewa mipaka, yani ukishazaliwa unasoma elimu ya lazima ile, unaolewa na kulea familia, hii sio sawa kwani wanawake wengi wanakufa na vipaji vyao bila ya kuvitumia pahala”. Aliongeza Asha.

Sitiamina ni mkurugenzi wa SITI AND THE BAND anasema anampongeza sana Aisha kwa kusimamia msimamo wa kutimiza ndoto zake kwa kutumia kipaji chake, na anamuona ni DJ bora hapa visiwani Zanzibar ambae pia anawashawishi vijana wengine wenye ndoto kama zake kutokukata tamaa ama kuogopa kunyooshewa vidole.

“Tasnia hii ya muziki inaangaliwa kwa jicho baya kidogo, lakini Aisha anajitahidi kuifanya ionekane kwa jicho zuri kutokana pia na mavazi anayovaa, na huu ndio utambulisho wake mkubwa na tunaamini utamkuza zaidi ya hapa”. Anasema Sitiamina.

Khamis Haji ambae ni mdau wa masuala ya burudani hapa visiwani Zanzibar anasema kwa upande wake anamuona Aisha kama mwanamapinduzi katika sekta ya muziki hasa u DJ kwa upande wa wasichana, kwani anawawakilisha vizuri na kuonesha kuwa hakuna kazi maalum kwa ajili ya wanawake au wanaume tu.

“ukiwa pahala ambapo dj ni HIJAB DJ, huwezi kutofautisha ukasema kama hapa anapiga mwanamke, ladha na mizuka ni ile ile inayopatikana kutoka kwa ma DJ wanaume, kwa kweli anajitahidi sana.

Aisha anawaasa vijana hasa wa kike wapambanie ndoto zao mpaka pale zitakapokamilika, wasikubali kuwekewa vizingiti kutokana na jinsia zao ama mavazi yao, muhimu ni kuwa na heshma, kuweka bidii na kuonesha kazi iliyobora.

Comments

Popular posts from this blog

BAJAJI WAMLILIA RAIS DK MWINYI PEMBA ,WAOMBA MSAADA KWAKWE WASEMA WAMECHOSHWA NA HILI KUTOKA MAWASILIANO

Masheha wanawake wa Wilaya ya Magharib B walivyoleta mabadiliko na maendeleo kwenye shehia zao.

MPANG0 MKAKATI JUMUISHI WA JINSIA KATIKA MICHEZO UTEKELEZAJI WAKE UZINGATIWE.