SALHA MWINJUMA; MWAKILISHI WA VIJANA KUTOKA WILAYA YA KUSINI UNGUJA YAJUE USIYOYAJUA AMBAYO NI MUONGOZO KWA WENGINE WENYE NDOTO ZA KUFIKA ALIPOFIKA YEYE.


NA MASOUD JUMA, UNGUJA
SALHA Mohamed Mwinjuma ni mwakilishi wa Viti Maalumu  anayewakilisha vijana kwenye Baraza hilo, ambapo safari yake ya siasa ameianzia akiwa na umri wa miaka 18.

 Mwaka 2020 alimaliza masomo yake ya shahada ya kwanza ya Uhusiano wa Kimataifa. Mnamo mwaka 2015 Salha aliwania viti maalumu na hatimaye kufanikiwa kuingia kwenye Baraza hilo akiwakilisha vijana kutoka Mkoa wa Kusini Unguja.

Kijana huyo anasema kuwa ameanza harakati zake kwenye umoja wa vijana wa CCM mwaka 2012 kabla ya kujitosa rasmi mwaka 2015 baada ya kuona anaweza kusimama na kutetea vijana wenzake.

Anasema amepata wakati mgumu kueleweka na jamii, lakini vijana na wanawake baadhi walimuelewa na sasa wanamuelewa zaidi kwani amekuwa akifanya kazi kwa ushirikiano wa hali ya juu na matokeo yake yamekuwa yakionekana siku hadi siku.

“Haikuwa kazi rahisi kwa wakati ule nilikuwa mdogo nina miaka 18 tu, nimejikita kwenye siasa nikiwa sina utani hata kidogo, kwa kweli wengi hawakunielewa wachache waliielewa kazi ninayofanya ambao walizidi kunipa moyo wa kusonga mbele,”anasema Salha.

Anazitaja changamoto alizokutana nazo katika hatua za awali alipowania nafasi ya uwakilishi ni pamoja na kukatishwa tamaa hususani na wanaume ambao wamekuwa wakifanya siasa kwa muda mrefu.

“Sikupata shida kukabiliana nazo kwa sababu zinaanzia ngazi ya chini na tangu nawania uwakilishi nilijua nitakutana nazo” anasema.

“Ninachofanya ni kuhakikisha najifunza kila siku, kwa wanaosema ya kujenga na kubomoa lengo ni kuwajua wote na kwenda nao sambasamba kwa sababu mimi ni kiongozi sasa siwezi kukwepa changamoto,” anasema.

Anasema wanawake wengi wanafeli kwa sababu wanaume wameshawapima na kujua udhaifu wao kwa miaka mingi wakikatishwa tamaa kidogo wanarudi nyuma.

Mwinjuma anasema hatarajii kugombea jimbo kwenye uchaguzi wa 2025 kwa sababu anataka kujifunza zaidi.

“Nitagombea tena nafasi hii niliyonayo sasa, nataka kujifunza zaidi kabla sijaingia kwenye mikikimikiki ya kuwania jimbo, ”anasema.

Anayataja malengo kuwa ni kuhakikisha anaowaongoza au aliochukua dhamana yao wanamuelewa na kujenga imani nao, ikiwa ni pamoja na kutekeleza anachowaahidi kwa kuyapeleka bungeni malalamiko yao ya kiserikali.

“Sababu kubwa ya mimi kuwa Barazani ni wao, hivyo nafanya kazi yao". anasema.

Salha anasema majukumu yake ya kazi hayaingiliani na familia kwa sababu wanafahamu anafanya nini na atakuwa wapi kwa wakati gani.

“Mume wangu na familia yangu yenye watoto wawili wanafahamu ratiba ya kazi zangu, kuna wakati nachelewa kurudi nyumbani kutokana na majukumu na wapo wananielewa, ”anasema.

Anasema licha ya uwakilishi wake kuorodhesha anawakilisha vijana, lakini hajawaacha nyuma wanawake pia ambapo amekuwa akiwasaidia katika shughuli zao mbalimbali.

Anasema huwa anakutana nao na kuangalia namna ya kuwapa mafunzo kwa ajili ya kujiendeleza kiuchumi na wapo waliofanikiwa kupitia vikundi hivyo.

“Nasimamia kuhakikisha wanapata mitaji, ambapo niliwahi kukutana na wafugaji wa nyuki wa eneo la Jambiani na Makunduchi nikiangalia miradi hiyo ambayo tuliwapa mafunzo na wamefanikiwa sana kupata asali ya kutosha, ”anasema.
Anasema mafanikio ya vikundi ndiyo kitu anachojivunia kwa sababu watu waliokupa dhamana wanapofanikiwa unapata nguvu ya kusonga mbele.

Salha anajinasibu kuwa bado yupo sana kwenye siasa, 
“Ninaweza kusema ndiyo kwanza naanza, wananchi watarajie makubwa kutoka kwangu.
Salha anamalizia kwa kutoa wito kwa vijana wenziwe khasa wa kike kuwa wanapopata nafasi wazitendee haki ili ionekane kama wao kweli wanaweza na wamedhamiria maendeleo.

Comments

Popular posts from this blog

BAJAJI WAMLILIA RAIS DK MWINYI PEMBA ,WAOMBA MSAADA KWAKWE WASEMA WAMECHOSHWA NA HILI KUTOKA MAWASILIANO

Masheha wanawake wa Wilaya ya Magharib B walivyoleta mabadiliko na maendeleo kwenye shehia zao.

MPANG0 MKAKATI JUMUISHI WA JINSIA KATIKA MICHEZO UTEKELEZAJI WAKE UZINGATIWE.