WANAWAKE WAUNGANA KUIMARISHA NAFASI ZAO ZA UONGOZI KATIKA JAMII: WASEMA HAWATENGANISHWI NA TOFAUTI ZAO ZA VYAMA VYA SIASA.
NA MASUOD JUMA, UNGUJA
Wanawake kutoka katika vyama mbalimbali vya siasa Zanzibar, ambao wamekutanishwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake TAMWA ZNZ kwa ajili ya kupatiwa mafunzo mbali mbali kuhusiana na uongozi na namna ya kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazomkumba mwanamke wakati wa kuitafuta nafasi ya uongozi katika jamii wamesema kwa sasa lengo lao kubwa ni kuona kuwa nafasi za viongozi wanawake zinaongezeka katika ngaz za maamuzi, hivyo tofauti za vyama vyao haziwezi kuwazuia kutimiza lengo lao hilo.
Wametoa kauli hiyo wakati wa kuwasilisha ushuhuda mbele ya balozi wa Norway nchini Tanzani Mhe Elisabeth Jacobsen huko katika ofisi za TAMWA ZNZ Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja, ili kuonesha ni kwa namna gani mradi wa kuwawezesha wanawake kushika nafasi za uongozi (SWIL) umewasaidia kuwajenga ili kufikia kuwa viongozi.
Naibu Katibu Mkuu wa Ngome ya Wanawake kwa upande wa Zanzibar Chama cha ACT Wazalendo Bi Halima Ibrahim alisema kuwa kwa sasa hali imebadilika sana kwao wanawake, wanashirikiana sana na wanawake wa vyama tofauti ili kuhakikisha kuwa wanawake wanakua mstari wa mbele katika nafasi za uongozi.
“Kwa kweli hali imebadilika sana, tofauti na zamani ambapo tulikua tunaonana ni maadui, tunaishukuru sana TAMWA kwa kutuweka pamoja na kutuonesha kuwa sote lengo letu ni moja, hivyo ni lazima tushirikiane kulifikia lengo hilo”.anasema Bi Halima
Nae Bahati Chum ambae aliwahi kugombea ubunge jimbo la Mahonda kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA anasema kuwa sasa chuki miongoni mwao imepungua sana hivyo imewapa nafasi ya kushauriana, kuulizana na hata kupeana moyo ili kuhakikisha hakuna anaekata tama.
“Tumefungua magrupu mbalimbali ya Whatsap, tupo wanawake wa vyama tofauti, na hatuangalii huyu katoka chama gani, tunaangalia sisi ni wanawake na tuna lengo moja la kushika nafasi za uongozi hivyo ni lazima tusaidiane”.
Bahati aliongeza kuwa wanawake ndio kundi kubwa la wapiga kura kipindi cha uchaguzi hivyo watakapoungana na kuwa kitu kimoja itakua ni rahisi kusimamisha nafasi nyingi za wanawake katika majimbo mbalimbali.
Kwa upande wake ndugu Hasina Hamad kutoka Chama cha Mapinduzi CCM alisema kuwa anashukuru sana TAMWA ZNZ kwa kumkutanisha na wanawake wengine kutoka vyama tofauti kwani imemsaidia kumjenga na kumtia ari zaidi katika kutimiza ndoto yake ya kuwa kiongozi.
“Tumekutanishwa hapa lakini tunasaidiana nje ya hapa pia bila ya kujali tofauti zetu za vyama kwa ivo hii itatusaidia kila mmoja kutimiza ndoto yake”. Alisema Hasina
Ndugu Hanifa Ramadhan kutoka Chama cha Mapinduzi CCM alisema kuwa yeye kama mwanamke anafurahi kukutana na wanawake wenzake ambao wana lengo moja hata kama wanatoka katika vyama tofauti, hiyo haiwazuii wao kujadiliana masuala yanayowahusu na kupeana njia ambazo zitawasidia kufanikiwa.
Nae afisa mradi huo wa kuwawezesha wanawake kushika nafasi za uongozi (SWIL) kutoka TAMWA ZNZ ndugu Maryam Ame amesema kuwa suala la wanawake kuungana ili kuongeza ushiriki wao katika nafasi za uongozi bila kujali tofauti za vyama vyao vya siasa ni jambo zuri kwani litasaidia sana kujenga na kuimarisha uongozi wa wanawake katika ngazi mbali mbali hapa nchini, hivyo amewaasa wanawake hao kuendelea kushirikiana na kuondosha chuki baina yao ili waweze kufanikiwa kwa kwa kiwango kikubwa zaidi.
Comments
Post a Comment