WAJASIRIAMALI NGALAWA WALIA NA UDOGO WA ENEO.
Na Yusra Said - Unguja.
WAJASIRIAMALI Wanawake wanaojishughulisha na biashara ya kuanika na kukausha dagaa eneo la Bububu Ngalawa Wilaya ya Magharib A wameeleza kushindwa kufikia malengo yao kutokana na changamoto kadhaa zinazowakabili.
Wakizungumza na muandishi wa habari hii ambae alitembelea eneo hilo wajasiriamali hao walisema kwa sasa biashara yao imekuwa tofauti na mwanzo kutokana na kupungua kwa kiwango cha uzalishaji.
Kwa mujibu wa takwimu kutoka Kampuni ya uvuvi Zanzibar ZAFICO eneo la Ngalawa lina jumla ya wajasiriamali 506 ambapo kati yao wabebaji dagaa ni 167,wapishi 70,waanikaji 114 na wanunuzi 155.
Bahati Shaaban ni miongoni mwa wajasiriamali katiaka eneo hilo alisema tatizo kubwa linalowapa usumbufu ni udogo wa eneo wanaloanikia dagaa lililopo Ngalawa ambapo husababisha dagaa kubaki na hukaribika hasa kipindi cha mvua inaponyesha.
Alisema awalia kabla ya Serikali kuwaamuru wahame katika eneo hilo walikuwa eneo la Maruhubi ambapo walikuwa na uwezo wa kuanika dagaa ndoo hadi 200 kwa siku lakini kwa sasa wanaanika wastani wa ndoo ishirini tu kwa siku jambo ambalo linawarudisha nyuma kimaendeleo.
Hata hivyo aliiomba serikali kupitia wizara ya ya uchumi wa bluu na uvuvi kuwatengenezea miundo mbinu rafiki itakayowawezesha kufanya biashara yao kwa weledi ili rasilimali hiyo iuzwe katika masoko ya kimataifa.
“Sehemu ya kuanikia dagaa ni ndogo sana ambapo sehemu ya mwanzo mimi kama mimi nilikuwa nikianika ndoo 200 kwa siku lakini leo hii ndoo ishirini tu zinanisumbua”alisema.
Mwanaisha Ali ambae pia ni mjasiriamali wa eneo hilo alisema cha kusikitisha Zaidi katika eneo hilo hamna hata huduma ya choo jambo ambalo linawaumiza hususan wanawake wanapotaka kujisaidia hivyo hulazimika kwenda kujisaidia baharini.
“Sisi wanawake ndo tunadhalilika Zaidi maana hata vyoo hapa hamna tukiwa na haja twende baharini au msikitini na huko msikitini pia utakuta maji hayatoki miezi “alisema .
Nae Saidi Mkubwa Saidi ambae ni mjasiriamali wa uanikaji wa dagaa katika eneo hilo alisema pia wanakabiliwa na ukosefu wa vitendea kazi ikiwemo chanja za kuanikia dagaa na kusababisha dagaa lao kutokuwa na ubora kutokana na mazingira ya kuanika chini.
“Vitendea kazi hatuna nah ii inapelekea dagaa letu kutokuwa na ubora hivyo tunaiomba serikali itusaidie kwa hili” alisema.
Haji Makame amabe ni mnunuzi wa dagaa aliefika eneo la Ngalawa kwa ajili ya kununua bidhaa hiyo alisema wakati wa mvua dagaa huwa adimu kulipata na linalopatikana huwa halina ubora ,hivyo huwa wanapata usumbufu hata wao wanaonunua kutokana na changamoto zilizopo.
“Kweli kipindi cha mvua changamoto za kupatikana kwa dagaa zinazidi na ukilipata inabidi uchukue tulinakuwa halina ubora” alisema.
Kufuatia madai ya vyoo katika eneo hilo muandishi wa habari hii alimtafuta Afisa mipango Baraza la Manispaa Magharib A Makame Nyange Khamis alisema amekiri kuwepo kwa tatizo hilo na tayari limeshafikishwa katika uongozi husika kwa ajili ya kutafutiwa ufumbuzi.
Aidha alisema kuwa vyoo katika eneo hilo vipo lakini changamoto kubwa iliyokuwepo ni hitilafu ya umeme ambayo hivi karibuni itafanyiwa matengenezo.
Katibu mkuu wizara ya uchumi wa bluu na uvuvi Aboud Suleiman Jumbe alisema sekta ya dagaa ni muhimu sana na inahitaji uangalizi wa hali ya juu ambapo kwa mwaka 2021 Zanzibar ilisafirisha zaidi ya tani 3500 zenye thamani ya shilingi zaidi ya bilioni 12.
Alisema licha ya rasilimali hiyo kuchangia pato la taifa kwa kiasi kikubwa lakini imekuwa ikiachwa nyuma kwa sababu ya kutokuwepo kwa miundo mbinu mbali mbali ikiwemo huduma bora za kiusalama na kiafya za kufikia kusafirishwa nje ya nchi.
Alisema kwa sasa soko kubwa la dagaa wanalouza ni katika nchi ya Kongo,hivyo matarajio yao ni kuwa rasilimali hiyo inauzwa hadi nchi za nje ikiwemo china.
Alisema Serikali ya awamu ya nane tayari inatambua umuhimu wa dagaa na imeashaanza kufanya utaratibu wa kuimarisha miundo mbinu ya uanikaji dagaa na kuleta mapinduzi ya huduma bora za kuzalisha kwa kuwawezesha wajasiriamali nyenzo na vifaa vya kisasa vya kuvulia na kuanikia dagaa .
Alisema pia serikali inafanya matengenezo ya eneo la Kama ambalo litakuwa ni kitovu kikuu cha sekta ya dagaa na litakuwa na uwezo wa kuchukua wajasiriamali wasiopungua elfu kumi.
Mkurugenzi muendeshaji wa Kampuni ya uvuvi Zanzibar ZAFICO Ameir Haidar Mshenga Alisema wamewahamisha katika eneo la Maruhubi kutokana na eneo hilo ni lakihistoria ,hivyo kuondoka kwao kutapunguza usumbufu kwa wageni wanaokuja kutembelea sehemu hiyo.
Aidha amewataka wajasiriamali kuwa wavumilivu mpaka ujenzi wa eneo la Kama utakapokamilika ambao unatarajiwa kuharimu shilingi bilioni 5.9 kwa awamu ya kwanza na matarajio ifikapo febuari 2023 eneo hilo litaanza kutumika rasmi.
Alisema ili waweze kupata miundo mbinu bora ya kimaendeleo ni vyema kufanya ubunifu na kupata muda wa utekelezaji wake.
Alisema wamewahamisha katika eneo la Maruhubi kutokana nae neo hilo ni la kihistoria ,hivyo kuondoka kwao kumepunguza usumbufu kwa wageni wanaokuja kutembelea sehemu hiyo.
Comments
Post a Comment