USAWA WENYE HADHI SAWA UNAOZINGATIA JINSIA KWENYE NAFASI ZA UONGOZI BADO KITENDAWILI TANZANIA.
NA ASIA MWALIM - UNGUJA.
INGAWA Tanzania imesaini mikataba ya Kikanda na Kimataifa kwamba itazingatia usawa wa kijinsia kati ya wanawake na wanaume katika uongozi bado safari ndefu katika kufikia azma hiyo.
Ili kufikia usawa wenye hadhi sawa ni lazima nchi iweke sheria ambazo inatoa fursa kwa wanawake na wanaume kuwa na nafasi zenye hadhi sawa kugombea nafasi za uongozi kwenye majimbo na nafasi nyengine.
Kwa hali ilivyo sasa Tanzania hakuna fursa sawa zenye hadhi sawa katika kugombea nafasi za uongozi nchini, kwa sababu nafasi za uteuzi wanazopewa wanawake hazina hadhi sawa kama ilivyo nafasi za kuchaguliwa.
Mfano uchaguzi mkuu uliofanyika 2020 unathibitisha ukweli huo, kutokana na idadi ya wanaume waliochaguliwa ni kubwa kuliko wanawake kwenye nafasi mbali mbali za uongozi, ikiwemo bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, baraza la wawakilishi, madiwani.
VIONGOZI WANAWAKE KUPITIA UCHAGUZI 2020.
Wabunge waliogombea nafasi hiyo wanaume 257 walioshinda 46, ambapo wanawake waliogombea nafasi hiyo 81, walioshinda 4.
Nafasi ya uwakilishi wanaume waliogombea nafasi hiyo ilikua 190, walioshinda 42 ambapo wanawake waliogombea 61 na walioshinda 8.
Wanaume waliogombea nafasi ya udiwani 276 walioshinda 85 ambapo wanawake waliogombea 74, walioshinda ni 25.
Asilimia ya ushiriki wa wanawake katika siasa na uchaguzi ni ndogo sana na hivyo kupelekea ushiriki wao kuwa mdogo na usio na hadhi sawa katika nyanja nzima ya uongozi.
Aidha kupitia utafiti uliofanywa na Chama Cha Waandishi wa habari wanawake Tanzania upande wa Zanzibar TAMWA zimeeleza kuwa, Takwimu za Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania (NEC) zinaonesha kuwa katika uchaguzi wa mwaka 2015, idadi ya wanawake waliopata nafasi za uongozi katika bunge la Tanzania kupitia majimbo, viti maalumu na uteuzi wa Rais ilikua 126 sawa na asilimia 32 ya wabunge 393 wote walioingia bungeni mwaka huo.
Pia idadi ya wanawake walioteuliwa kugombea viti maalumu ni ndogo sana, na hitoi hadhi sawa mfano katika chama cha CCM waliweka asilima tisa, Chadema asilimia sita, CUF asilimia 11, ACT Wazalendo asilimia 15.
Kwa Zanzibar wanawake walioingia katika Baraza la Wawakilishi mwaka mwaka 2015 kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ni asilimia 36 au Wawakilishi 28 kati ya 84 huku wanawake waliopata nafasi za udiwani ni 87, zikiwemo nafasi za viti maalumu ambapo haitoi usawa wenye hadhi sawa kwa jamii.
Akizungumza na Makala hayo Naibu Katibu Mkuu Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) upande wa Zanzibar, Tunu Juma Kondo, amekiri kutokuwepo sheria ya idadi ya uwiano wa uongozi sawa ndani ya CCM na kwamba kila mtu anapata nafasi kwa kuchaguliwa na wajumbe na sio kulazimisha nafasi maalumu kwa uwiano wa kijinsia.
Nae, Ismail Rajab, (sio jina lake sahihi) amesema ipo haja ya kuzingatia usawa wenye hadhi sawa kwa wanawake, kwani wanawake wa sasa wameelimika na kufahamu mambo mengi pia wanajifunza kutoka ndani na nje ya nchi.
Khamis Haji Khamis amesema wanawake wanaweza kutumikia nafasi hizo kwa usawa wenye hadhi sawa kutokana na uwezo wa kazi wanazofanya.
KWA NINI HALI IPO HIVYO.
Kutokana na taratibu za kisheria za kuwezesha na kuweka ulazima wa wanawake kuwa na fursa sawa zenye hadhi sawa kwa wanawake na wanaume kunaifanya nchi kutokutekeleza kwa ufanisi baadhi ya mikataba ya kikanda, kitaifa na kimataifa.
Mikataba mbali mbali ya Kikanda, Kitaifa, na Kimataifa imeeleza suala la haki sawa wa jinsia kwa wanawake na wanaume katika uongozi ili kupata hadhi sawa kwa wote.
ITIFAKI YA SADC
SADC ambayo ni Jumuiya ya maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika, ambapo mkataba wake wa kikanda uliotiwa saini mwaka 2008 wenye vifungu 43 unaeleza kuondoa utafauti na kuwatenga wanawake katika Nyanja mbalimbali za maendeleo na kuwasaidia katika usawa wa kijinsia nchi wanachama.
Ambapo katika kifungu cha nambari 12 kinasisitiza ushiriki sawa wanawake kufikia asilimia 50/50 kwenye Nyanja za maamuzi, serikalini na taasisi binafsi.
JUKWAA LA UTENDAJI KAZI LA BEIJING
Mpango wa utekelezaji wa Beijing katika maelezo ya dhamira nambari 7 ya mpango huo imeeleza kuhusu uwezeshaji wa wanawake na ushiriki katika vyombo vya maamuzi kwa kuangalia uwiano wa kijinsia kwenye ngazi zote za uongozi.
ITIFAKI YA MAPUTO
Haya ni makubaliano yaliyofanyika tarehe 11, Julai 2003 nchini Msumbiji katika mji wa Maputo, katika kipengele nambari 9 cha makubaliano hayo imeonesha haki ya kushiriki wanawake katika siasa sambamba na kushiriki katika mchakato wa vyombo vya kutoia maamuzi.
MKATABA WA CEDAW
Huu ni mkataba wa CEDAW wa kimataifa ambao unapinga aina zote za udhalilishaji, mkataba huu umeasisiwa mwaka 1979, katika mkataba huu kwenye kifungu chake cha 7 kimeeeleza wazi wanawake kushiriki katika siasa na maisha ya kijamii.
Pia umeeleza kuweko kwa usawa baina ya mwanamke na mwanamme katika uchaguzi na mchakato mzima wa upigaji kura sambamba na nafasi za kushika madaraka, kwa mantiki hiyo basi CEDAW ni mkombozi kwa wanawake katika Nyanja za kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Kwa mukhtadha huo basi ni wazi kuwa katiba, mikataba ya kimataifa haikuzingatiwa ipasavyo katika kutoa fursa sawa ya uongozi.
NINI KIFANYIKE.
Ananileya Nkya, mwanaharakati ambae pia ni Muandishi muandamizi ameshauri, Serikali ya Tanzania kupitia sharia zake za uchaguzi na kuweka kipengele kinachowataka vyama vya siasa kueka idadi sawa ya wanawake na wanaume kugombea kwenye majimbo.
Aidha amesema nafasi za viti maalumu lisiwe kwa wanawake badala yake liwe kwa kwa watu wenye mahitaji maalumu kwani wanawake uwezo wao ni mkubwa katika uongozi.
"Chama cha Mapinduzi kimetibitisha kuwa wanawake wanaweza kuongoza nafasi za bunge la jamuhuri ya muungano wa Tanzania, nafasi za wawakilishi, madiwani, hivyo kupitia sharia hiyo pia vyama vya siasa vitalazimika kufuata sharia" alisema .
Hata hivyo Dk. Nkya ameshauri wanawake kuelekea uchaguzi wa Taifa wa 2025, wajiandae kugombea nafasi mbali mbali za uchaguzi kwenye maeneo yao ikiwemo ubunge, uwakilishi, na udiwani na sio kusubiri nafasi za uteuzi ili kupata hadhi sawa.
Mkurugenzi wa Chama Cha Waandishi wa habari wanawake Tanzania upande wa Zanzibar, Dk Mzuri Issa Ali, amesema umefika wakati kuondoa vikwazo vyote vinavyo kwamisha usawa wenye hadhi sawa kwa wanawake ili kwenda sambamba na mikataba hiyo.
DK MZURI ISSA ALI- MKURUGENZ TAMWA-ZNZ
Amesema sheria zilizopo hazitoi fursa sawa kwa wanawake na wanaume hivyo kukiuka baadhi ya vipengele vya mikataba hiyo.
Aidha aliomba viongozi wa vyama vya siasa kuweka sheria rafiki zitakazo toa muongozo wa bayana wa nafasi za uongozi sio kuwapa nafasi za uteuzi ambapo zinakuwa kama ziada.
Hata hivyo amesema mara nyingi TAMWA, inatoa mafunzo mbali mbali ya uongozi kwa wanawake ili kuhakikisha wanawake wanapata haki sawa katika nafasi mbali mbali.
Comments
Post a Comment