FURSA NA CHANGAMOTO ZINAZOWAKABILI VIJANA KATIKA KUFIKIA MAENDELEO YA KUJIKOMBOA KIUCHUMI WAOMBA SERIKALI KUENDELEA KUWASAIDIA KUZIPATIA UFUMBUZI ILI KUZIDISHA KASI YA KUZIFIKIA FURSA MBALI MBALI KATIKA SIASA UCHUMI NA UONGOZI .
- Get link
- X
- Other Apps
‘’KIJANA ni mtu yeyote mwenye umri wa miaka 15 hadi miaka 35,’’ndivyo sera na sheria ya vijana Zanzibar inavyofafanua.
Lakini kwa upande mwengine kijana ametafsiriwa kuwa ni mwanamke au mwanamme yeyote mwenye miaka katia ya 15 hadi 24, kama sera ya taifa ya Maendeleo na vijana ya mwaka 1996, na kama ilivyorekebishwa mwaka 2007.
Kijana ni mtu muhimu kwa taifa lolote ulimwenguni, kwani ndio nguvu kazi ya taifa, ndio taifa la kesho kama wasemavyo baadhi yao.
Lakini kijana ndio tumaini la taifa na ndio mtu anayetazamiwa kwa mapana ya nchi, katika kuongoza, kukuza uchumi na kuzima majaribio ya kihalifu.
Vijana wanakumbana na changamoto mbali mbali katika maisha yao, na mwisho wa siku taifa linamchukulia kama mtu aliyeshindwa na asiye na msaada wowote kwa taifa lake.
Lakini katika umri huo wa ujana, inampasa kijana kujitambua ili aweze kuwa na muonekano halisi, sio kwa umri tu bali matendo zaidi.
Ni lazima awe na ushawishi katika masuala muhimu na kwa manufaa ya jamii kwa ujumla, hasa kwa vijana wenzake, katika kushawishi ndio tunaona nguvu ya kijana na kuanza kutengeneza taifa imara.
Hata serikalini, vijana wengi wameaminiwa na kuonesha ushawishi mkubwa, kuwa wana uwezo wa kufanya kazi kwa kuaminiwa na pale wanapopewa nafasi za uongozi.
Serikali imeahidi kuendelea kuweka mazingira bora ya kuwawezesha vijana, kuzitumia fursa zinazopatikana katika sekta ya uchumi wa buluu, kuibua fursa za ajira na kuwainua kiuchumi.
Serikali ya awamu ya nane, inathamini juhudi mbali mbali zinazofanywa na vijana, hivyo ipo tayari kuendelea kuwashirikisha katika kuzitumia fursa zitakazosaidia kuwainua kiuchumi.
IDARA YA MAENDELEO YA VIJANA
Idara ya maendeleo ya vijana, ni miongoni mwa taasisi za serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, iliyoanzishwa mwaka 1992 kwa lengo la kuratibu na kusimamia maendeleo ya vijana Zanzibar.
Idara hii inatekeleza kazi zake kwa mujibu wa sera ya maendeleo ya vijana Zanzibar, mipango na miongozo ya Serikali.
Dhamira yake ni kukuza ustawi na maendeleo ya vijana, kuwajengea mazingira mazuri na endelevu yatakayowawezesha kushiriki kikamilifu katika sekta za kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Mkurugenzi wa Idara hiyo Zanzibar Shaibu Ibrahim Mohamed anasema, juhudi mbali mbali zinachukuliwa na serikali kuhakikisha shughuli za vijana vinatekelezwa.
"Vikao hivyo pia tunapata kujua changamoto na tunapashana habari mpya, zilizopo katika sekta ya vijana, kwani kuna miradi mingi ambayo inaibuka siku hadi siku,’’anasema.
Akitaja malengo ya Idara hiyo moja wapo ni kuandaa, kusimamia na kuratibu utekelezaji wa sera, mipango ya maendeleo nchini.
Jengine ni kuimarisha ushiriki na ushirikishwaji wa vijana katika nyanja za kiuchumi na kijamii, ili wawe mfano bora wa taifa lao.
Kuratibu taasisi na asasi za maendeleo ya vijana Zanzibar, kusimamia mipango ya malezi na makuzi ya vijana na kuimarisha ushirikiano, baina ya taasisi za vijana ndani na nje ya nchi.
‘’Jengine ni kuhakikisha masuala ya vijana yanazingatiwa na kuingizwa katika sera, mipango, miradi ya kitaifa, na kusimamia mipango ya uwezeshaji wa vijana kiuchumi,’’anafafanua.
OFISI YA RAIS KAZI, UCHUMI NA UWEKEZAJI
Mratibu wa Idara ya Ajira Pemba Said Salum Othman anasema, idara yao, inatekeleza mipango maalumu ya kuhakikisha vijana wanawapatia mafunzo ya ujuzi.
“Mafunzo haya ni ya miezi sita kwa vijana wa rika tofauti kuanzia miaka 15 hadi 24 kwa wenye elimu ya msingi, sekondari na ambao hawana elimu kabisa, ili kuhakikisha vijana wanapatiwa fursa na kuweza kujiajiri na kuajirika,” anasema.
Mafunzo hayo ya ujuzi yanatolewa, na mwaka jana wilaya ya Wete walichukuliwa vijana wawili, Chake watatu, Mkoani wawili na Micheweni wawili kupelekwa Unguja kwa ajili ya kusoma utalii.
“Mwezi Novemba mwaka 2021, tulichukua vijana wa wilaya ya Wete, tunawaangalia ambao wanafaa kwa mchujo maalumu badala yake, tunawapeleka katika vyuo maalumu vya mafunzo ya ujuzi wa kujiajiri au kuajirika,” anasema.
Mwaka huu mwezi Machi walichukuliwa vijana wengine kwa ajili ya kupatiwa mafunzo ya kutengeneza mafriji, viyoyozi, ushoni pamoja na uchongaji.
Hivyo sasa inafahamika kuwa, vijana 339 wa wilaya ya Chake chake, wamenufaika wakiwemo wanawake 14 na wanaume 325 na ajira kupitia kampuni za ujenzi wa miradi saba ya ahuweni wa COVID 19.
Mkoani jumla ya vijana 117 wakiwemo wanaume 72 na wanawake 45, huku Wete ikiwa na vijana 158 wanaume 141 na wanawake 17 na Micheweni vijana 772 wanaume 688 na wanawake 84 kupitia miradi hiyo.
Afisa TEHAMA kutoka mfuko wa uwezeshaji wananchi kiuchumi Pemba, Farid Hamuni Juma, anasema serikali ya awamu ya nane, imetenga zaidi ya shilingi bilioni 80 kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali.
Ambapo tayari kwa kisiwa cha Pemba pekee, zimeshatolewa zaidi ya bilioni 2 kwa vikundi 228.
Lakini hata wilaya ya Wete nako kuna vikundi 38, vimeshapatiwa zaidi ya shilingi milioni 300 na wilaya ya Micheweni ina vikundi 38 vilivopatiwa zaidi ya shilingi milioni 400.
Anasema, kati ya bilioni hizo 80 kuna mgawanyiko ambao umewekwa asilimia 45 ni vijana, asilimia 35 ni wanawake, asilimia 12 watu wenye mahitaji maalumu, huku asilimu 5 wakiwa ni wastaafu na asilimia 3 watu ambao wameachana na dawa ya kulevya.
WIZARA YA UCHUMI WA BULUU NA UVUVI
Ali Rashid Hamad, kutoka ziara hiyo Pemba anasema, jamii bado uwelewa wa jamii kuhusu masuala ya uchumi wa buluu uko chini, hivyo wameona kuna haja ya kutoa elimu ili wafahamu.
“Tumetoa elimu hii ya uchumi wa buluu katika shehia 25 za Pemba na ndani yake asilimia 48 ya tuliowafikia ni vijana, tumetoa mafunzo ya kusarifu wa mwani kati ya hao vijana walikua 26 na kutoa vifaa vya uvuvi ambapo wanufaika walikua 16 kati ya hao asilimia 60 ni vijana,” anaeleza.
Wizara ilitoa mafunzo ya ufugaji wa majongoo bahari, ambapo waliwafikia watu 80 asilimia 50 kati ya hao walikua ni vijana na baada ya kuwapa mafunzo waliwajengea vizimba vitano vya kufugia.
“Lazima tuwajengee mabanda maalumu kwa kushirikiana na watu wa ‘FIO’ tayari wameshatenga zaidi ya shilingi milioni 120 kwa ajili ya banda la kukaushia mwani kwa wakulima wetu wakiwemo vijana,” anasema.
Anasema, sasa hivi kuna zaidi ya shilingi bilioni 49 ambazo zimepangwa kutolewa kwa kukopeshwa wanufaika wakiwemo wavuvi, wafugaji wa mazao ya baharini, wakulima wa mwani wakiwemo vijana.
IDARA YA KILIMO
Afisa Kilimo Wilaya ya Chake chake Rashid Mohamed Wema, anasema idara hiyo inafanya kazi kwa kushirikiana na shirika la kilimo ulimwenguni ‘FAO’.
Ambalo limewawezesha vijana 23 wa vikundi viwili vya ushika kwa wilaya ya Wete na Mkoani.
“Katika mradi wa ‘CFP’ ambao mabwana shamba wetu wameshirikiana kwenye kilimo cha mboga mboga na matunda kwa Wete vijana 184 wamewezeshwa kupitia vikundi 12.
Wilaya ya Chake vijana 195 wamewezeshwa kupitia mradi huo kwa kupatiwa taaluma pembejeo, mbegu na mbolea, Mkoani vijana 133 wamewezeshwa kupitia vikundi 13 na Micheweni vijana 21.
WIZARA YA UTALII NA MAMBO YA KALE
Afisa Utalii na Mambo ya Kale Pemba, Hafidh Omar Masoud anasema, wizara yao inapitia hatua mbali mbali katika kuwawezesha vijana.
Kwa mwaka huu wa fedha, wizara imekua ikitoa elimu bure kwa vijana ambayo inahusisha madarasa ya vijana yanayohusiana na utalii na lugha za kigeni.
“Tunatoa elimu hii kupitia mikoa yote miwili ya Pemba kwa upande wa kusini tuna wanafunzi 35 wakiwemo wanawake 10 na wanaume 20 na kaskazini ni wanafunzi zaidi ya 50 wa darasa la elimu ya kigeni,” anasema.
MAMLAKA YA MAFUNZO YA AMALI
Mwalimu Mkuu wa chuo cha mafunzo ya amali Vitongoji Juma Mussa Ali anasema kwa mwaka 2020, jumla ya wanafunzi 580 walipatiwa mafunzo ya ufundi, kupitia fani za uchongaji, ushoni na uchomaji wa mageti ‘uashi’.
Mwaka 2021/2022 walipata vijana 400 wa kike, ambao walijiunga na masuala ya upandaji na usarifu wa mwani, ambao walijitolea kuitumia fursa ya kilimo hicho.
Anasema, katika lengo la kuwaendeleza vijana mamlaka imeandaa mpango wa kutoa mafunzo kwa vijana watakaotoa huduma za kiufundi kwenye hoteli na sehemu nyengine za nje ya nchi kupitia fani ya umeme, mafriji, viyoyozi na mafundi bomba.
BARAZA LA VIJANA
Fahim Abdalla ni Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wilaya ya Chake chake, amepongeza kwa jitihada zake za kuwaunga mkono vijana, kupitia nyanja mbali mbali.
Anaona kazi iliyoko mbele yao sasa kwa vijana ni kukaza buti, ili fedha na miradi iliyopo kwa ajili yao ifikie lengo la kujiongezea kipato.
"Tunakosa haki zetu Ikiwemo kupata Mikopo ya kujiendeleza Kielimu Kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo kufeli na kukosa sifa za kupata Mikopo ya Serikali jambo ambalo limekuwa likirudisha nyuma Malengo ya kufika mbali kimaendeleo Alisema Hashil Fadhil Kijana Kichungwani Chake Chake.
" Familia Zetu hazimudu gharama za kutusomesha Elimu ya Juu , Mkopo wa Serikali wa kusomeshea ymekuwa na Masharti ambayo wengi tuna malengo ya kufika mbali lakini masharti yanatufanya tubaki hapo hapo tulipo bila kuongeza Elimu hata kama tunataka Kujiendeleza Alisema Rushda Khamis Kassim Kijana kutoka Baraza la Vijana.
" Changamoto zetu tunazisemea sana ikiwemo kupewa Fursa za uongozi lakini bado hazijafikiwa zaidi kwa umri huu wa vijana Ambao tunaushawishi mkubwa kwa rika la vijana kama wetu Umri miaka 25 na kuendelea lakini bado jamii Serikali bado haijatuamini kama tunaweza kufanya Makubwa ya kuleta Mabadiliko.
Changamoto za Kufikia Maendeleo katika harakati zetu mbali mbali moja ni Mitaji, Serikali inatuwezesha kwa kutupatia mikopo Lakini bado haijafikia malengo kutokana na Kuoata kwa Asilimia isiyozidi 50 jambo ambalo halitoshelezi kutunufaisha sote kujiendeleza katika harakati zetu Aliongeza Rushda.
JEE ! VIJANA WANA WITO GANI KWA SERIKALI JAMII NA ASASI ZA KIRAIA JUU YA CHANGAMOTO AMBAZO ZINAWAKABILI.
Rushda Khamis Kassim alisema kuwa " Vijana ndio Hazina ya Taifa lolote lile , Changamoto yeyote ambayo inatukwaza kufikia Maendeleo Tunaiomba Serikali na Wadau wa Maendeleo kwa vijana Watusaidie kuzipatia ufumbuzi ili tuweze kutimiza Maelengo ya kimaendeleo Ambayo yatasaidia Taifa.
MWISHO.
- Get link
- X
- Other Apps
Comments
Post a Comment