DIWANI VITI MAALUM FATMA MNGWALI ATOA NENO KWA JAMII YA KASKAZINI A KUHUSU WATU WWNYW ULEMAVU.
Na RAIFFA ABDALLAH
DIWANI wa Viti Maluum Wilaya ya Kaskazini A Fatma Mngwali Khamis , ameiasa Jamii kuongeza Uelewa pamoja na Mashirikiano kwa Watu wenye Ulemavu katika kuwasaidia husasani katika ngazi Uongozi, kwani ni watu wenye Mawazo pamoja na Uwezo wa kufanya mambo Mazuri kama watu wa kawaida.
Hayo Aliyasema wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi katika Afisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini A, Gamba Zanzibar.
FATMA MNGWALI KHAMIS - DIWANI VITI MAALUM K/NI A UNGUJA.Alisema, aliamua kuingia katika kugombania nafasi hiyo ya udiwani kwa ajili ya kuwasaidia watu wenye ulemavu, na kuwatetea watu wenye ulemavu waweze kupata haki zao.
“kwa ukweli kitu kilichonipelekea kuweza kugombania ni kuona jinsi sisi watu wenye ulemavu tulivoekwa katika jamii na kuonekana kama hatuko sawa, lakini kwa mtazamo wangu Toka niingie katika Uongozi nimeona kuwa jamii imekosa uelewa juu ya watu wenye ulemavu na wanaona kama maajabu kwa mtu mwenye ulemavu kuwa kiongozi” alisema.
Amesema kuwa , Watu Wenye Ulemavu ni watu wenye kujiamini na wachapa kazi na Wanamawazo Mazuri wakati mwengine kumshinda hata mtu wa kawaida katika kuhakikisha jamii inazidi kupata maendeleo
Akieleza Mafanikio aliyoyapata ni kuandaa Makongamano mbali mbali ya watu wenye ulemavu ambayo yamefanyika sehemu tofauti ikiwemo Nungwi, lengo la makombano hayo ni kutoa muamko kwa watu wenye ulemavu na kuonesha kuwa wanaweza katika kushirika kwenye huduma za jamii.
" Ninatumia fursa yangu katika kupita Maskulini kwa ajili ya kusikiliza Changamoto tofauti zikiwemo za watu wenye Ilemavu, pia kuwapa Elimu walimu wanaowasimesha watoto wenye ulemavu juu ya namna bora ya kuweza kuwasomesha ili waweze kufahamu na kufaulu vizuri”
Akizungumzia Changamoto anazozipata ni kutokupata mashirikiano katika kutekeleza majukumu yake ya udiwani, na kuongeza kuwa mashirikiano ni madogo anayoyapata kutokana hali yake ulemavu wa kutokuona.
“Wakati mwengine nashindwa kusoma kabrasha ambazo zimeandikwa kwa lugha ya kawaida, licha ya kuwa nina katibu ambaye ananisaidia lakini wakati mwengine katibu anakuwa na mambo yake binafsi siyo wakati wote ndio atakuwa na mimi kwa ajili ya kulisoma kabrasha hilo, hivyo huwa nakosa kujibu maswali vizuri wakati wa kikao cha baraza” alisema
Aidha alisema kuwa anaomba kuzidi kupata mashirikiano baina ya madiwani wenzake, wawakilishi pamoja na wabunge ili kuhakikisha wanazitatua Changamoto hizo kwa pamoja, kwani miongoni mwa watu wanaopata shida na maumivu ni watu wenye ulemavu.
Kwa upande wake Khamis Rashid Khamis Afisa aneshughulikia watu wenye ulemavu wilaya ya Kaskazini A , ameleza kuwakuwa, tangu Diwani Fatma aweze kupata Uongozi amekuwa akitoa mashirikiano kwa watu wote bila kuweka ubaguzi wakiwemo watu wenye ulemavu .
Akizungumzia Serikali namna ilivyo shiriki katika kuhakikisha Diwani Fatma anapata nafasi hiyo ili aweze kuisaidia jamii na walemavu kwa ujumla alisema,
“Kabla ya kugombania alinifata na nikampa Changamoto ya Uongozi ili kumuepusha kuja kuathirika Kisaikolojia, kutokana na watu tofauti wanaweza kuja kumkwaza katika ongozi wake”
Alitoa wito kwa wananchi kuwa, jamii imuunge mkono Diwani Fatma pamoja na kuwa nae bega kwa bega katika harakati zake zote ili kusudi kwamba azidi kufanya mambo ya kimaendeleo ambayo yataweza kuimarisha jamii na kuifanya kuwa bora .
Nao wanakijiji wa fukuchani Ali Haji na Mwanajuma Khamisi , wamesema kuwa, kupitia Uongozi wa Diwani Fatma wameweza kutatuliwa shida mbali mbali ambazo zilikuwa zikiwakabili Kijijini hapo, kama vile ukosefu wa maji jambo ambalo ndilo lilokuwa likiwakosesha raha.
Tulikuwa tukilazimika kuyafata maji masafa ya mbali na wakati mwengine tukilazimika kununua huduma maji jambo ambalo lilitukosesha usingizi”
Ndani ya Wilaya ya Kaskazini A Unguja kuna jumla ya Viongizi Wanawake Wenye Ulemavu Watatu . Wawili ni viongozi wa Jumuiya wa watu wenye ulemavu wilaya ya Kaskazini A Unguja na moja ni BI Fatma Ngwali kiongozi wa kisiasa.
Comments
Post a Comment