Wananchi wapewa wito Kuhusu VVU
Fatma Abrhman
JAMII nchini imetakiwa kutokupuuzia kuhusu gonjwa la
Ukimwi, kwani bado upo na unaendelea kuwa tishio kwa maisha ya watu katika makundi na rika zote Ulimwenguni .
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Othman Masoud Othman, ametoa kauli hiyo huko Viwanja vya Skuli ya Msingi Jadida Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani .
Amesema ni vyema kila mmoja kuwa ni askari wa kupinga vita tatizo la Ukimwi na kwa pamoja kukemea vitendo vinavyosababisha maambukizi ya makusudi au hata ya bahati mbaya sambamba na kulaani udhalilishaji wa aina zote na kuepuka kuwanyanyapaa wagonjwa wa maradhi ya Ukimwi.
Akizungumzia hali halisi ya Ugonjwa huo hapa Zanzibar Makamu Othman amesema jitihada zinafanyika katika kuyafikia malengo kupambana na maradhi ya Ukimwi na hadi kufikia Disemba 2021 idadi ya maambukizo mapya imepungua kwa asilimia 32 ingawa lengo ilikuwa ni kuzuia maambukizi hayo kwa asilimia 83.
Aidha amesema kiwango cha maambukizo mapya kwa vijana wa kike kimeongezeka kwa mara tano zaidi ya malengo yam waka 2025, huku utumiaji wa kinga kwa makundi maaulum nao ukipungua na kufikia baina ya asilimia 27 hadi 53 ikiwa ni asilimia ndogo ya kuweza kuyafikia malengo yaliyowekwa ya kuondosha tatizo hilo nchini ifikapo 2030.
Kutokana na hali hiyo Mhe. Othman amezitaka Tume za Ukimwi , Wizara ya Afya pamoja na wadau wengine kushirikiana na kuzifanyia tathmini takwimu za tatizo hilo zilizopo ili kubaini vyema makundi ya jamii ambayo hayafikiwi na huduma hizo pamoja na kuongeza ufanisi katika kuzifikia shabaha na maelengo ya kuondoa Ukimwi kabisa Zanzibar ifikapo 2030.
Kwa upande wake waziri wa nchi Afisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Harous Said Suleiman, amesema serikali kupitia Tume ya Ukimwi na kwa mashirikiano na wadau mbali mbali wamekuwa wakifanya jitihada kubwa za kutoa elimu ikiwa ni jitihada za kupambana vyema na maradhi hayo sambamba na kuzuia maambukizi mapya ya Ukimwi.
Nae Mwenyekiti wa Tume ya Ukimwi Zanzibar Dk. Ali Salim amesema ukosefu wa usawa katika upatikanaji wa huduma za maradhi ya ukimwi ni changamoto hasa katika kuyafikia makundi maalum ambayo yanaathirika zaidi na maradhi hayo.
Naye Mwakilishi kutoka Mahirika ya Umoja wa Mataifa George Loy amesema katika kupambana na maradhi hayo ni vyema kwenda na mpango wa vipaumbele zaidi ikiwemo kongeza jitihada ya kutafutwa fedha ambayo ni changamoto kubwa katika kukuza ufanisi wa kuyakabili maradhi hayo sehemu mbali mbali duniani.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kaskaszini Pemba Salama Mbarok Khatib amewataka wanaume na wanawake kubadili mtazamo ili kuhakikisha wanaepukana na ushawishi wa kuwepo maambukizi mapya ya maradhi ya ukimwi Zanzibar.
Amesema mkoa wake utaendelea na jitihada mbali mbali zitakazoasaidia kuongeza uelewa kwa jamii na hasa vijana kuachana na ,masuala yote yanayoweza kusababisha maradhi ya ukimwi ikiwemo kuachana na tabia ya kuwa na wapenzi wengi jambo ambalo ni hatari zaidi kwa maambukizi mapya ya maradhi hayo.
Comments
Post a Comment