MIKAKATI YA KUDHIBITI UTORO YAZAA MATUNDA.
HII HAPA MIKAKATI YA UFAULU NA KUDHIBITI UTORO SKULI ZA MSINGI MICHEWENI
Na Amina Ahmed
Mohamed
MIKAKATI iliyobuniwa na uongozi wa wilaya
ya Micheweni kudhibiti utoro skuli za msingi wilaya ya Micheweni imewezesha
wilaya hiyo kuongoza kitaifa kwa ufaulu kwa miaka minne mfululizo.
Mkuu wa wilaya
ya Michewemi Mgeni Khatib Yahya amesema mikakati hiyo ni pamoja na kupiga marufuku ajira za watoto maeneo
yote na wananchi katika shehiza zote kwenye wilaya hiyo wameelimishwa
kuzingatia umuhimu wa elimu na malezi bora,
Kadhalika wilaya ya Micheweni imeunda kamati maalum katika kila
shehia kufuatilia suala la suala la utoro skuli na imepepiga marufuku watoto wa
skuli kushiriki dufu la usiku na kuzunguka hovyo usiku kuangalia televisheni.
Tatizo la dufu
linathibitishwa na mkazi wa shehia ya Majenzi Hassan Omar ambaye anasema "zamani
watoto walikuwa wanachelewa kulala wanazifuata ngoma popote zinapopigwa
hawakataziki lakini aliekuwa mkuu wa wilaya alipotoa marufuku waliogopa
wakaanza kutulia majumbani kusoma”.
Kwa mujibu
wa mkuu wa wilaya ya Micheweni alipoanza kazi katika wilaya hii mwaka 2020 kulikuwa na jumla
ya wanafunzi watoro 7,609 ambao walikuwa
nje ya skuli ambapo 3,000 kati yao ni wanafunzi wa skuli za msingi .
Amesema hata
hivyo wanafunzi 1,240 wakiwepo wanawake 892 na wanaume 348 wamesharudishwa
skuli rasmi na wanaendelea vema na masomo.
Afisa Elimu msingi wilaya
ya Micheweni Asya Msellem Hassan amesema utoro
uliobaki wilaya ya Micheweni kwa sasa sio ule wa moja kwa
moja unatofautiana na ule wa miaka iliyopita huku zaidi
ukibaki katika maeneo ya ukanda wa pwani.
"Upo
ule utoro wa siku mbili siku moja bhasi na zaidi ni skuli ambazo zipo maeneo ya
bahari Makangale, Tumbe, Shumba Maziwa ng'ombe na hivyo sio ule wa mtoto
kukatisha moja kwa moja mkuu wa wilaya anatusaidia kazi hii ya
kumaliza utoro Micheweni".
SHEHA WAFUNGUKA
Ili kupata
kufahamu kinachoendelea kwenye shehia kuhusu mikakati ya kudhibiti utoro skuli
mwandishi alifunga safari hadi Sheha wa Makangale na kuzungumza ana kwa
ana na sheha wa shehiya hiyo Said Kombo Said ambaye amesema;
"Utoro
ulikuwepo kutokana na suala la maji wanafunzi walikuwa wanatumia kisingizio cha
kufuata maji ya bomba na kutoroka
skuli na kushuka baharini kwenda
kufanya kazi za kupara samaki, kuokota Mwani na au kwenda ucheza badala
ya kwenda skuli.
Sheha huyo amesema
kwa sasa ‘’mashirikiano ya kamati iliyoundwa shehiani petu na
wanakijiji hasubutu mwanafunzi kutoroka wanagopa wakionekana watachukuliwa
hatua’’.
Amema tatizo
limepungua sana na kwamba mkuu wa wilaya anapita pita na anatoa
maelekezo wanashirikiana bega kwa bega kutekeleza maelekezo hayo. .
Sheha huyo wa
shehia ya Makangale amesema katika shehia hiyo imeweka sheria ambapo mzazi
atakaeonekana anamtumikisha mtoto atachukuliwa hatua.
Kwa upande wake,
Rahila Ramadhan Juma Sheha wa shehia ya Shumba Mjini ameeleza hali ilivyokuwa
awali kuhusu utoro skuli na mikakati ya kudhibiti tatizo hilo
ilivyofanikiwa.
”Suala la
utoro ilikuwa ni uelewa mdogo wazazi juu ya umuhimu wa elimu ndio husababisha
wanafunzi washindwe kudhibitiwa wanakuwa wapo majumbani mwao”, anaeleza sheha
Rahila.
Amesema kwa
mfano awali wazazi walikuwa hawako tayari kutoa mashirikiano kumaliza
tatizo la utoro wala kusimamia wanafunzi wasome.
Hata hivyo amesema
utoro pia ulikuwa unachangiwa na tatizo la uchache wa waalimu walimu mashuleni.
“Utakuta mwalimu mmoja anashghulikia darasa moja lenye wanafunzi pengine 70
wale atawadhibiti lakini madarasa mengine huku hayana mwalimu hayasimamiwi
wanatoroka kwa vile vipindi zaidi ya vitatu darasa halijaingia mwalimu",
amesema
"Hali
ya ufaulu mfano awali skuli yaa msingi iliyopo Shehiani mwangu Skuli
ya Karume ilikuwa haitoi wanafunzi waliofaulu michipuo lakini mwaka
jana 2021 ilitoa ni jambo la faraja".
Kwa upande wake
Sheha wa shehia ya Micheweni Khadija Abdi Haji Kuhusi alipofikiwa
na kuhojiwa alisema "nikiri
utoro kwa wanafunzi wa skuli za msingi limefanikiwa kudhibitiwa na ni
kutokana na kamati maalum ya kusimamia utoro wa wanafunzi na
tumefanikiwa juu ya hilo na leo hii limepungua kabisa".
WANAFUNZI WATORO WALIORUDISHWA SKULI
Baadhi ya
wanafunzi ambao uongozi wa wilaya walifanikiwa kuwarudisha skuli wametoa duku
duku lao walipokuwa nje ya skuli ambapo wamedai sababu ya kutoroka skuli ni kutokana na
kukosa sare, kuumwa pamoja na kukosa ufahamu katika masomo yao.
Heri Omar amesema
"nilijiona sifahamu masomo ya skuli nikawa nje ya skuli lakini kwa sasa nimesharudi
nawaambia wanafunzi wengine ambao wametoroka warudi skuli tuje tusome’’.
Mwanafunzi
mwingine Time Makame amesema “nilikuwa sina sare kwa sasa nishapata naawambia
wanafunzi wenzangu warudi skuli waje tuje tusome elimu ni ufunguo wa maisha’’.
Kwa
upande wake mwanafunzi Fatma Juma Ali anasema alikuwa anaumwa na kifua
kwa sababu alikuwa anabanja mawe ya kokoto na ndiyo sababu akawa haende skuli lakini kwa sasa ‘’nisharudi nawaambia
wanafunzi wenzangu wasikae utoro waje skuli tusome tupate
kufanikiwa" .
WALIMU WAELEZA MIKAKATI YAO
Walimu
kwa upande wao WAELEZA kuwa kufanikiwa kwa jitihada za kudhibiti utoro
kwa wanafunzi kumetokana na vikao vya walimu wakuu wa skuli
zilizomo ndani ya wilaya kupanga mikakati ya pamoja ili kuona tuna ufaulu
haushuki.
"Mikakati
ikiwemo ya walimu wakuu kuanzisha kambi za kusoma muda wa ziada, kamati maalum
za skuli kufuatilia watoro jambo ambalo tumefanikiwa kupunguza taatizo la utoro
lakini kuongeza ufaulu", amedokeza Salum Mkadam Hamad
mwalimu mkuu Skuli ya Mkanagale Msingi.
Kai Omar
Haji kutoka skuli ya Micheweni B msingi amesema kambi za kimasomo zina
mchango mkubwa na kuwa chachu ya maendeleo ya elimu na silaha ya kudhibiti
utoro. Amesisitiza kuwa ‘’lazima walimu tujue mwenendo wa
mwanafunzi tunakuwa nao muda wote hilo linasababisha utoro
usijitokeze kwa sana" .
ONGEZEKO LA UFAULU
‘’Kuna
msemo usemao penye nia pana njia’’ Msemo huu umethibitika katika Wilaya ya
Micheweni kufuatia takwimu zilizotolewa na Afisa Elimu msingi wilaya ya
Micheweni Asya Msellem Hassan zinazoonyesha kwamba mwaka 2019 jumla
ya wanafunzi 107 walifaulu kati ya wanafunzi 1632 ambao walifanya mitihani
ya darasa la sita wilayani humo.
Amesema ufaulu uliongezeka zaidi
mwaka 2020 ambapo jumla ya wanafunzi 1919 waliofanya mitihani
167 kati yao walifaulu jambo ambalo kabla halijawahi
kutokea.
Ameongeza Mwaka
2021 wanafunzi 257 walifaulu kati ya wanafunzi 3255 waliofanya
mitihani skuli za msingi wilaya hiyo.
Wilaya ya Micheweni iliyoko katika Mkoa wa kaskazini ndani ya kisiwa cha Pemba ambayo ni moja ya wilaya kumi zilizoko Zanzibar inaongoza kwa matokeo ya darasa la nne sambamba na kuvuuka lengo liliowekwa na wizara ya Elimu juu ya kudhibiti tatizo la utoro na kuwarejesha skuli wanafunzi wa skuli za msingi waliotoroka kwa sababu mbali mbali.
mwisho
Comments
Post a Comment