KIPATO DUNI KWA WANAWAKE KINAZUIA USHIRIKI WAO KATIKA MICHEZO.
NA ASIA MWALIM
NCHI nyingi duniani zina mabadiliko makubwa katika soka la wanawake ambapo wachezaji wanapata malipo mazuri na kuwafanya kuwa miongoni mwa wachezaji wanaolipwa vizuri katika soka.
Katika nchi kama marekani kupitia ligi kuu ya soka la wanawake (NWSL) wachezaji wengi wanawake wanapata mishahara inayofikia hadi dola milioni 1 kwa mwaka, lakini kwa soka la wanawake hususan visiwani Zanzibar hali ni tofauti kabisa kwenye suala la malipo.
Hali ya kipato kwa wachezaji wanawake nchini Zanzibar ni mbaya sana huku wengi wakikosa mikataba rasmi na kulipwa kiasi kidogo cha fedha, ingawa Tanzania bara inaonekana kuwa bora kidogo kutokana na uwepo wa ligi kuu ya wanawake inayotoa fursa za kifedha.
Zanzibar ina historia ndefu ya soka lakini soka la wanawake limeanza kupata umaarufu zaidi katika miaka ya hivi karibuni, hivyo kufanya baadhi yao kukosa mishahara na wengine kulipwa kiwango cha chini kabisa.
Kwa mfano wachezaji wengi Zanzibar wanapata kati ya shilingi elfu tatu (30,00) hadi elfu tano (50,00) na hawana posho wala mishahara na wakati mwengine hukosa mechi kwa miezi kadhaa.
WACHEZAJI WANAWAKE ZANZIBAR
Mchezaji wa Green Queen ya Zanzibar Annastazia Desmon, anasema soka la wanawake Zanzibar linahitaji kujitolea Zaidi kama mwanasoka hana shughuli nyengine ya kufanya anaweza kujikuta anashindwa hata kufanya mazoezi.
Anasema mchezo wa mpira kwa wanawake umekua ni tofauti na wanaume ambao mpira ndio kazi yao kuu na ikitokea kama mwanasoka anajishughulisha na kazi nyengine hiyo ni ziada tu. “kwa soka la wanawake husussan visiwani Zanzibar mambo ni tofauti kabisa”anasema.
wanalazimika kuugawa muda wao kati ya kufanya kitu wanachokipenda, yaani mpira wa miguu, na kufanya biashara ndogondogo zinazoweza kuwaingizia kipato na kuwawezesha kujikimu wao na familia zao.
Kidawa Kheri Hamad, 32, mchezaji wa Green Queens, anasema soka la wanawake visiwani Zanzibar wanapata shida zinazofanana vipaji vyao vimeshindwa kuwawezesha kuziishi ndoto zao kwa furaha na majivuno kutokana na uwepo wa uwekezaji hafifu kwenye soka la wanawake Zanzibar.
Licha ya kuutumikia mchezo huo kwa muda wa miaka nane sasa, Kidawa anakiri kwamba kipato alichokitengeneza kwa muda wote huo hakimpi ari ya kuendelea kuutumikia mchezo wa soka, mchezo anaoupenda sana.
“Natamani maisha yangeweza kunipatia nafasi nyingine ya kupata kipato, ikiwa nitapata kazi ya kufanya, yenye maslahi, itakayonisadia kuingiza kipato kizuri naweza kuacha mpira.”anasema.
Zuhura Soud Othman ni mchezaji wa timu ya Yellow Queens aliyeanza kucheza mpira wa miguu wakati akiwa mwanafunzi wa darasa la nne, mwaka 2018, anasema“Zanzibar mpira wa miguu kwa wanawake haulipi, tofauti na wanaume kwa sababu hapa Zanzibar hakuna mwendelezo wa ligi, hivyo hatuna fursa”anasema.
WACHEZAJI WA KIUME
Samir Abdillah Haji anacheza daraja la pili timu ya mtani katika kijiji cha Makunduchi, anasema mchezo wa mpira Zaznibar haulipi anacheza kwa mapenzi na kujenga uwezo,”sitegemei kulipwa badala yake napata posho ambalo halina uhakika uhakika wa malipo ni kwa timu za serikali au zinazojiweza.anasema
“malipo yanategemea na timu kuanzia shilingi elfu 1, 2,3, 5, na timu ikifungwa ndo munapewa nauliya shilingi elfu moja ya kupanda daladala unafuu ni kwa wale walioajiriwa”anasema.
WAZAZI
Farashuu Khamis Khamis anasema mtoto wake amekua mchezi takriban miaka minne na hajaona maendeleo aliyopata wala faida ya msingi zidi ya kujenga afya. “kwenye suala la kuimarisha kipato na maslahi ya wachezaji wanawake Zanzibar hakuna labda kidogo kwa wanaume” anasema.
Mzazi Nassor Mikidadi Nassor anasema, kutokana na uhalisia wa mazingaira ya visiwani mzazi haoni haja ya mtoto wake kwenda kufanya kazi isiyo na malipo labda sekta ya michezo kwa watoto wa kike kuangaliwa upya,”ni vyema serikali kuangalia namna ya kuwapatia ajira, malipo na mikataba wachezaji wakike nao wanahitaji huduma” anasema.
VIONGOZI WA TIMU ZA MPIRA
Riziki Aboubakar Islah, mwalimu wa soka la wanawake, anaamini kwamba mpira wa miguu unatoa fursa kubwa sana ya kumkomboa mwanamke kiuchumi, alishauri wadau kusaidia kukuza soka la wanawake Zanzibar ili kukuza soka hilo.
Mwenyekiti wa Soka la Wanawake Zanzibar, Yahya Khamis Ali, mpaka sasa kuna timu kumi za soka la wanawake kutoka Unguja na Pemba, huku idadi ya wachezaji ikiwa ni zaidi ya 150, na kukiri kuwa soka la wanawake visiwani hapa limezorota kwa kiasi kikubwa, kwa kukosa ligi yenye mwendelezo pamoja na wadhamini.
“Changamoto kubwa ni wadhamini wa ligi za mpira wa miguu wa wanawake, sisi tunategemea ligi ikiwepo, pamoja na wadhamini, ndiyo vitawafanya wacheza soka wanawake visiwani hapa waonekane.” anasema.
VIONGOZI WA CHAMA CHA SOKA
Mwenyekiti wa Chama cha soka Mkoa wa Kusini Unguja, Abubakar Khatib Kisandu, anasema hakuna timu yoyote ya soka la wanawake inayolipwa hapa Zanzibar, “Wachezaji wa ligi kuu Zanzibar wanawake hakuna anaelipwa mshahara badala yake wanapewa posho dogo kulingana na mechi wanazocheza ambalo halitoshezi”anasema.
VIONGOZI WA SERIKALI
Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar (BTMZ), Said Marine, alisema Serikali inaliona suala hilo na iko mbioni kulitafutia ufumbuzi.”Serikali inajitahidi sana kukuza hili soka kwa kuweka ligi, mashindano mengine, na hata kutafuta wadhamini,”
Marine anasema kwenye jamii pia bado kuna changamoto ya mashabiki kutojitokeza kwenye michezo ya wanawake, na hii inatokana na fikra kwamba mwanamke wa Kizanzibari hatakiwi kujihusisha na mchezo wa soka.
Kwa mfano Stephane Aziz Ki ni mmoja wa wachezaji bora katika Ligi Kuu Tanzania Bara Timu ya Young africans (YANGA) inakadiriwa analipwa takribani shilingi 30,000,000, Clatous Chama Inakadiriwa analipwa shilingi 28,000,000 na Feisal Salum mzaliwa wa Zanzibar anajulikana kama mmoja wa wachezaji wenye talanta katika Ligi Kuu Tanzania Bara anaechezea Azam fc. inasemekana analipwa shilingi 23,000,000.
WANAHARAKI
Khairat Haji, Afisa Miradi kutoka TAMWA-ZNZ anasema ni vyema serikali iweke mikakati ya kuhakikisha wanawake walipwa kama ilivyo wachezaji wa kiume ili kutoa fursa sawa kwa wote. “Serikali itoe mchango wake, na sisi kama asasi za kiraia tunafanya nafasi yetu kuhakikisha wanawake wengi zaidi wanashiriki kwenye mchezo wa mpira wa miguu”anasema.
“Michezo ni kwa wote, na ikiwa timu za wanaume zinapewa kipaumbele na kukuzwa, basi Serikali ifanye hivyo hivyo kwa timu za wanawake ili kuleta usawa na sio kuwaambiwa wajitolee nao wanamajukumu,” alisema.
MWISHO
Comments
Post a Comment