MPANG0 MKAKATI JUMUISHI WA JINSIA KATIKA MICHEZO UTEKELEZAJI WAKE UZINGATIWE.
NA ASIA MWALIM
MARA nyingi tumeshuhudia uzinduzi wa mipango mikakati kwenye masuala mbali mbali ikizinduliwa, lakini ukifatilia kwa karibu utabaini utekelezaji wake haufikii lengo husika.
Kwa kuwa utekelezaji wake hauzingatiwi, huo huwa wakati kwa baadhi ya watu kutokujali kutekeleza yalioelezwa kutokana kutochukuliwa hatua yoyote.
“Huwezi kumwambia mgeni apite wakati mlango wa nyumba yako umeufunga” huu ni wakati sasa serikali, wadau mbali mbali wa michezo na jamii kushirikiana katika utekelezaji wa mpango mkatati jumuishi wa michezo ili kufikia dhana ya kuanzishwa kwake na kila mmoja kunufaika na fursa za michezo.
Kwa muda mrefu kundi kubwa la wanawake na wasichana walishindwa kushiriki michezo ipasavyo kutokana na changamoto kadhaa ambazo hazina usalama kwao kushiriki michezo.
Hali hiyo ni miongoni mwa vikwazo vinavyowakabili baadhi ya wanawake wanaojitokeza kushiriki michezo, hatimae kuvunja ndoto zao ya kuibua vipaji kwa kutokuwepo uasawa wa kijinsia katika michezo.
MPANGO MKAKATI
Disemba 5/ 2024 wadau wa michezo na serikali zimeshiriki katika uzinduzi wa Mpango Mkakati Jumuishi wa Jinsia katika Michezo Zanzibar wa 2024/2025 hadi 2028/2029 ambao unatekelezwa na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ), Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar (BTMZ), Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na Mradi wa Kanda wa Michezo kwa Maendeleo Afrika ambapo pia umejumuisha Utambulisho wa Muongozo wa Ulinzi katika Michezo.
WACHEZAJI
Zuhura Soud Othman ni mchezaji timu ya Yellow Queens anasema licha ya uzinduzi wa mpango jumuishi wa michezo jambo la msingi ni ufatiliaji ili kuhakikisha malengo husika yanafikiwa.“serikali ishirikiane na wadau wa michezo kufuatilia utekelezaji wa mpango huo ambao ni mpya unahitaji kupewa kipaumbele”anasema.
Mwajuma Abdalla Mchezaji wa kike anasema, uzinduzi wa mpango mkakati huo ni ishara ya kuengeza hamasa kwa wanawake katika michezo jambo ambalo Zanzibar bado liko nyuma ikilinganishwa na maeneo mengine kama Tanzania bara.
Mohammed Yahya mchezaji wa Timu ya KMKM, anasema baadhi ya wanawake wanaona aibu kushiriki mchezo wa mpira mara nyingi hujihusisha michezo midogo midogo ikiwemo mchezo wa nage.
JAMII
Baadhi ya wazazi ikiwemo Maryam Hamdani, Leluu Jumanne, na Khalid Mwinyi wanasema Mpango huo utasaidia kutoa fursa sawa kwa Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu sambamaba na kuleta mabadiliko ya usawa wa kinsia katika michezo jambo ambalo litaongeza vipaji na kupata idadi kubwa ya wachezaji wakike Zanzibar.“Zanzibar inasifika kwa kuwa na viapaji tunahisi huu ni wakati wa wazazi kuwaruhusu watoto wao kushiriki michezo ili kuibua viapji vyao ambavyo vitaonekana”.
WADAU WA MICHEZO
Luisa Scheuber kutoka ubalozi wa Ujerumani, anasema watahakikisha wanashirikiana na wizara husika ili mpango huo ufanikiwe katika utekelezaji wake kwa faida ya wananchi hasa wanawake.
Anasema amefurahishwa na ujenzi wa viwanja vizuri na vya kisasa katika maeneo mengi ya Zanzibar ikiwemo vijijini hatua ambayo itaibua vibaji michezo maeneo mengi na kushirikisha jinsia zote.
WANAHARAKATI.
Mkurugenzi Chama Cha Wanasheria Wanawake Zanzibar, (ZAFELA) Jamila Mahmoud, anasema muongozo huo ni mkombozi kwa wanawake na watu wenye ulemavu ili kuwa na mazingira mazuri kila mmoja katika kushiriki michezo.
Mratibu kutoka Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) Rufea Juma, anasema muongozo wa kupinga ukatili wa kijinsia katika michezo utasaidia kuondoa ukatili unaotokea kwa wanamichezo.
Anasema muongozo huo una walenga wana michezo na wadau wanaopinga ukatili wa kijinsia katika jamii ambao utaonesha ni kwa namna gani wataweza kutengeneza sera za ndani ili kujikinga na vitendo vya udhalilishaji kwa wanawake na wanaume.
“Tunataka kuona usawa wa kijinsia ukiongozeka katika michezo kwani wanaume ni wengi sana ukilinganisha na wanawake wanamichezo, yote haya yanakuja kutokana na kukosekana mazingira yasiyo rafiki na salama kwa wanawake kushiriki michezo” anasema.
Rufea anasema Uzinduzi wa mpango mkakati huo sio kikomo badala yake wataandaa mafunzo kwa makocha, wanamichezo ili kuona namna ya kuufanyia kazi hasa katika maeneo muhimu kwa lengo la kutengeneza mazingira salama, usawa wa kijinsia na kutekelezeka kwa urahisi zaidi.
Afisa Programu Chama Cha Waandishi wa habari wanawake Tanzania (TAMWA-ZNZ) Asya Hakimu Makame anasema, Mpango mkakati huo jumuishi utasaidia TAMWA kwa kiasi kikubwa kwani ni miongoni mwa wadau wa kuleta ujumuishi wa kijinsia katika michezo kwa kuwatumia waandishi wa habari na vyombo mbali mbali vya habari, na namna ya kutumia mpango huo.
Anasema pia utasaidia kuwashirikisha wasichana, wanawake na watu wenye ulemavu jambo ambalo litasaidia kukuza maendeleo na ujuzi wa kijamii kwa watoto unaohusisha ajira na vijana kupitia michezo.
WIZARA YA HABARI, VIJANA UTAMADUNI NA MICHEZO.
Afisa Mdhamini wizara hiyo, Mfamau Lali Mfamau, anasema wizara inaandaa fursa kuhakikisha kila mmoja anashiriki michezo na kupata nafasi ya kushiriki michezo na kupata ulinzi wakati wa wote wa michezo ili kuwa na michezo salama hasa kwa wanawake.
Aliwataka wanamichezo kuusoma muongozo huo kwa makini na kuuelewa ili kujua lengo halisi lililokusudiwa kwa kuhakikisha wanapata fursa ya kushiriki michezo wakiwa salama.
WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII JINSIA, WAZEE NA WATOTO.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Riziki Pembe Juma, anasema dhamira ya serikali ni kuhakikisha michezo inakua jukwaa salama, jumuishi na lenye usawa wa kijinsia kwa kila mshiriki.
Anasema mpango mkakati jumuishi wa jinsia katika michezo Zanzibar wa mwaka 2024/2025 hadi 2028/2029 na muongozo wa ulinzi na uslama katika michezo.
Anasema dhamira ya kufanya hivyo ni kukuza maendeleo ya michezo jumuishi na yeye usawa wa kijinsia hapa zanzibar kwani hiyo ni historia inayojumuisha juhudi za kuimarisha mazingira ya michezo kwa wote.
Maandalizi ya mpango mkakati jumuishi wa jinsia katika michezo ni hatua ya kimkakati inayolenga kuimarisha nafasi ya usawa wa kijinsia katika michezo Zanzibar.
“Mpango huu unajumuisha malengo na mikakati ya kufanikisha kauli mbiu ya sera ya michezo ya mwaka 2018 ambayo inasema ‘michezo kwa wote’, kupitia mpango huu tunaweka dira na hatua madhubuti za kufanikisha maendeleo ya sekta ya michezo kwa kuwa jumuishi yenye kuzingatia usawa wa kijinsia na kuleta mabadiliko chanya hapa nchini” anasema.
Mpango mkakati huo ni nyezo muhimu ya kuhakikisha wanawake na wanaume wanapata fursa sawa ya kushiriki kuongoza na kufanikisha maendeleo ya sekta ya michezo Zanzibar, kuondoa vizuizi vya kiutamaduni na miundo mbinu vinavyowazuia wanawake kushiriki kikamilifu kwenye michezo kuanzia ngazi za jamii hadi kitaifa.
Aliongeza kuwa katika michezo vitendo vya ukatili wa kijinsia unyanyasaji wa kihisia na mwili pamoja na mazingira hatarishi vimekua vikijitokeza mara kwa mara hapa nchini, hivyo muongozo huo utasaidia kupiga vita changamoto hizo kutokana na mikakati madhubuti iliyowekwa.
Comments
Post a Comment