MPIRA WA MIGUU KWA WANAWAKE ISIWE SABABU KUACHA MILA NA DESTURI ZA KIZANZIBAR.
NA ASIA MWALIM
WANAWAKE na wasichana wanaocheza soka hapa nchini wamekua wakitafsiriwa tofauti kutokana na muonekano wao wakiwa viwanjani kwenye mazoezi na hata wanapokua wakitetea ubingwa wao viwanjani.
Muonekano huo unajumuisha mavazi, mwendo, sauti, aina za mikato ya nywele na wengine kufika mbali zaidi pale wanapojaribu kujifanya wanahitaji kuwa na mahusiano na wanawake wenzao.
Binti anapojihusisha na mpira wa miguu ni vyema abaki kwenye haiba yake ya kike, bila ya kujali aina ya mchezo anaocheza ili kuweka mitazamo mizuri kwa jamii ambao wana nafasi kubwa ya kushajihisha michezo kwa wanawake.
Agosti 22, mwaka 2021, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan alizungumza kuhusu muonekano wa wachezaji wa kike wa mchezo wa mpira wa miguu ambao wanajaribu kutaka kuondoka kwenye uasili wao na kutaka kujifananisha na wanaume.
Wachezaji wanajaribu kujifananisha na wanaume, jambo ambalo linapoteza heshima yao na kujenga taswira mbaya kwa jamii yao jambo ambalo huchangia kuwapa wasiwasi wazazi kuwaruhusu watoto wa kike kushiriki michezo.
Baadhi ya wachezaji wa kike limeanza kuwaingia akili suala hilo na kusema kuwa Mpira wa miguu kwa wanawake usiwe sababu ya kuacha mila na desturi za kizanzibar.
WACHEZAJI
Halima Ibrahim kutoka Timu ya Mpira wa miguu Jangombe, alisema ameamua kubaki kwenye uhalisia wake na kujikubalisha kuwa na mvuto wake halisi na kvaa hijabu kichwani kwani mpira wa wa miguu ni mchezo wa baadhi ya masaa na sio muda wote.
“Nimeamua kubaki kwenye uhalisia wangu, na nina muonekano mzuri licha ya kuwa mpira wa miguu unahitaji mwili mkakamavu” alisema.
Mavazi ya mchezaji huyu yanamtambulisha wazi jinsia yake, na hataki kuwa na tabia ya kuvalia nguo za kiume licha ya kuwa ni shabiki na mpenzi mkubwa wa mchezo wa soka.
“Napenda urembo ingawa nilivyojiingiza kwenye soka sikupata ushawishi wakunifanya niendelee kuupenda badala yake nimejikuta natembea kwa ukakamavu, na mazungumzo yangu yalifanana na wachezaji wa kike” alisema.
Alisema anaamini kipaji chake kwani kubadili mavazi au muonekano sio sababu ya mtu kufanya vizuri uwanjani na kuwataka watoto wa kike kubaki kwenye misimamo yao ili kufikia malengo wanayotarajia bila ya kuiga tabia za wengine.
Ingawa yupo kwenye soka lakini mchezo huo haujamfanya awahi kufikiria kubadili muonekano ili aonekane kama mwanamme kwa sababu anjiamini jinsi alivyo.
“Napenda muonekano wangu wa kike na sijawahi kufikiria kubadilisha muonekano huu kwani nimeweka ahadi hii kwa wazazi wangu na wao wameweka matumaini makubwa kwangu hasa wanapotizama muonekano wangu” alisema.
Mrembo huyo alisema amevutiwa na mshambuliaji wa kimataifa wa soka la wanawake Tanzania, Opah Clement anaecheza kwenye klabu ya Besiktas ya Uturuki ambae ameingia katika orodha ya mabinti walioamua kufanya muonekano wao kuwa wakike japo ni mchezaji wa mpira wa miguu.
“Opah amepost picha zake kwenye mitandao ya kijamii akiwa katika mavazi ya nguo za kike (gauni) akiwa amerembwa uso wake na kuwavutia mashabiki wengi wa kike kujiweka kwenye asili hiyo.
Nae, Sabahi Salum alisema, awali wakati anajiunga na mchezo huo ndoto zake ni kutafuta kipaji na kuimarisha afya ingawa suala la mavazi ya kiume ametokea kulipenda kadiri siku zinavyozidi akiwa mchezaji.
Sabahi alisema aliamua kugawa magauni yote ya kike kwa wadogo zake na baadae kununua nguo za kiume jambo ambalo limepoteza asili ya muonekano wake wa awali.
“Imefika wakati hata vazi la nguo aina ya kike nakalichukia na kuona haliendani na mimi kutokana na mazingira tofauti niliyokutana na yo viwanjani na kunifanya mimi kuathiwa na tabia za walionitangulia kwenye soka” alisema.
JAMII
Maryam Kheir Juma, alisema hakuna mzazi anaefurahia mtoto wake kuharibika wala kuhusishwa na tabia chafu kwa sababu ya michezo, ingawa wapo watoto wa kike wanaobadilisha mwendo, sauti na mikato ya nywele wakati utamaduni wa Zanzibar ni kuvaa ushungi kwa watoto wa kike.
Alisema tabia hiyo ni mfumo wa kuigwa kutoka kwa wachezaji wa kongwe ammao watoto wameukuta na kuendeleza.
“Mimi nahisi hawa wachezaji wadogo wadogo kwenye soka wanaiga tabia hii kwa zile timu kubwa za kitaifa au wanatizama timu za nje ya nchi ambazo wengi wao hawajisitir vya kutosha kulingana na tamaduni zetu” alisema.
Aliwashauri watoto wa kike kubaki kwenye haiba yao kwa sababu kuna maisha baada ya michezo pia nao wanatahitaji kuwa na wenza wao kwa ajili ya kuanzisha familia kwa maana ya kufunga ndoa.
WADAU WA MICHEZO
Adil Muhammed Ali, alisema wanawake wanakua na aibu ya kushiriki michezo kutokana na kuona baadhi ya wachezaji wakiwa na mavazi ya nusu uchi jambo ambalo liko kinyume na mila na tamaduni zilizozoeleka.
“Watoto wa kike wa hapa kwetu Kuvaa nguo fupi za michezo (jezi) na kucheza hasa watoto w kike wenye ulemavu kutokana na mila na tamaduni za wazanzibar hawawezi labda liangaliwe suala la mavazi kwanza” alisema.
Mkurugenzi wa TAMWA ZNZ, Dkt. Mzuri Issa, alisema jamii haipaswi kuchukua mabaya machache na kuyatolea hukumu kwa wengine kwani wapo baadhi ya wachezaji wanajisitiri na wanaendelea na michezo.
Aliwasisitiza watoto wa kike kuwa na heshima katika jamii ili kuwa mfano wa kuigwa na wengine jambo ambalo litahamisha wanawake wengi kujitokeza na kushiriki michezo mingi tofauti na ile ilyozoeleka na kupewa jina la michezo ya kike.
“Tuwe mifano mizuri ya kuwa na heshima katika jamii, kwasababu sisi tuna nafasi ya kupata mawaidha sehemu mbalimbali ya stadi za maisha.
Hivyo tuna kila sababu ya kuendeleza kuimarisha na kuhamasisha michezo kwa wote,” alisema Dk Mzuri.
VIONGOZI WA TIMU ZA MPIRA
Kocha wa timu ya Mamlaka ya Maji na Nishati Zanzibar ZURA Simai Mwinyi, alisema mabadilko ya mavazi kwa timu za wanawake yapo ingawa wamechukua jitihada mbali mbali za kuhakikisha wanawake wanacheza kwenye uhalisia.
Alisema amekua akiwahusia mara kwa mara namna ya kutobadilisha muonekano wao kwakua ni wachezaji wa soka bali wabaki katika uhalisia husika licha ya mchezo huo kuhitaji ukakamavu na nguvu nyingi ndani ya uwanja.
Nidhamu ni jambo la msingi katika timu za mpira kwa upande wa timu, kwa upande wa timu hiyo imekua mstari wa mbele kuweka nidhamu kwa wachezaji wake ingawa wapo baadhi ya wachache wanaonesha kutokubali jambo hilo moja kwa moaja.
Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu wilaya ya Mjini (UDFA) Mohammed Rashid Bwaksi alisema, wachezaji wengi wanawake wanabalika muonekano wao kutokana na hali halisi ya mchezo huo.
Aidha alisema mchezo huo unatumia nguvu kubwa na pia hautaki kubeba mizigo mingi mwilini ili kumpa ugumu na wepesi wakati wa mchezo.
WANASAIKOLOJIA
Mwanasaikolojia na mshauri nasahakutoka jumuiya ya wanasaikolojia na ushauri nasihi Zanzibar, Ramadhan Mohammed Hassan alisema jambo lolote ukiliamini na kudhani linawezekana kuna asilimia kubwa ya kufanikiwa, hivyo wanawake wanatakiwa kujiamini kutokana na maumbile yao.
"Si vizuri kubadilisha muonekano kwani mfumo wa akili yako pia utajengeka vile mawazo yako yanavyokuwa na unavyoamini" alisema.
Salhia Kombo Mwalim, Afisa ushauri nasaha Wizara ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, alisema si vyema watoto wa kike wanaoshiriki michezo kuvaa mavazi yenye stara itasaidia kulinda mila na desturi za nchi.
Aidha alisema wachezaji wanapaswa kuiga mambo muhimu kutoka kwa waliowatangulia ikiwemo namna ya kucheza na kupata njia nzuri za kuwa wachezaji bora sio vitu vya ajabu mfano kuiga mikato ya nywele ambayo haiendani na tamaduni zao.
VYAMA VYA MICHEZO ZANZIBAR.
Mrajisi wa Vyma Vya Micezo Zanzibar Abubakar Muhammed Lunda alisema idadi ya vyama vya michezo vilivyosajiliwa ni 42.
Alisema michezo kwa wanawake inakuwa kwa sasa ikilinganishwa na miaka ya nyuma ni vyema kuacha vitu visivyo na msingi ili kupata fursa zaidi ikwemo kujidtiri na kuvaa mavazi ya heshima.
Aliongeza kuwa mpira sio sababu ya kumfanya mtoto wa kike abadilishe muonekano kwani anaweza kucheza akiwa amejisitiri,
VIONGOZI WA SERIKALI
Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Othman Massoud Othman Julai 28 mwaka huu amevitaka vikundi vya mazoezi nchini kuweka kanuni na miongozo ya maadili ambayo itasaidia kuondoa mitizamo hasi kwa jamii juu ya ushiriki wa makundi yote katika vikundi vya mazoezi na michezo.
Alisema, kuwepo kwa kanuni zinazosimamia maadili katika mazoezi na michezo kutasaidia watu wengi hasa wanawake kuona eneo hilo ni salama kwao na kuondoa dhana potofu iliyojengeka katika jamii.
Comments
Post a Comment