KAZI 162 ZINAZOHUSU SHERIA YA HABARI NA UHURU WA KUJIELEZA ZIMECHAPISHWA.
NA ASIA MWALIM
JUMLA ya kazi 161 zinazohusu sheria ya habari na uhuru wa kujieleza zimechapishwa na waandishi wa habari 25 wa Unguja na Pemba waliopatiwa mafunzo kupitia mradi wa miaka 2 wa majaribio wa mapitio ya sheria za habari Zanzibar.
Afisa Programu wa mradi wa majaribio wa mapitio ya sheria za habari Zanzibar kutoka TAMWA Zaina Abdalla Mzee, aliyasema hayo wakati akiwasilisha ripoti ya tathmini ya utekelezaji wa mradi kwa kipindi cha mwaka mmoja 2023/2024 kwa waandishi wa habari, wadau wa serikali na binafsi wakiwemo ZAMECO na tume ya Utangazaji Zanzibar.
Alisema kazi zilizowasilishwa zilionyesha mapungufu yaliyojitokeza katika sheria mbali mbali za habari ikiwemo sheria namba 5 ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magaazeti na Vitabu ya mwaka 1988 na marekebisho yake namba 8 ya mwaka 1997 ambayo ni ya muda mrefu.
Na sheria namba 7 ya mwaka 1997 ya Tume ya Utangazaji Zanzibar, na marekebisho yake namba moja ya mwaka 2010 ambazo bado zina wakwaza waandishi wa habari katika uyendaji wao.
Aidha alisema lengo la kuanzishwa mradi wa kutetea masuala ya uhuru wa habari ni kupatikana kwa sheria huru na rafiki kwa vyombo vya habari ili kufanya kazi zao kwa weledi na kufanya habari za uchunguzi.
Akielezea mambo yaliyofanyika kwa kipindi cha mwaka mmoja wa utekelezaji wa mradi huo Zaina alisema jumla la vikao 5 vilifanyika kwa ajili ya kuzungumzia umuhimu wa sheria mpya ya habari pamoja kuzichambua sheria 8.
"Sheria hizo 8 tulizipitia na kuangalia mapungufu yake na kufanikiwa zikawasilishwa kwa waandishi wa habari na baadhi ya viongozi wa serikalini" .
Aidha alifahamisha kuwa katika kipindi cha miaka 2 cha utekelezaji wa mradi huo wanatarajia uhuru wa habari Zanzibar ukue na uheshimiwe kupitia sheria rafiki za habari hivyo aliwasisitiza waandishi wa habari na wadau mbalimbali kuongeza kasi ya kuandika umuhimu wa uwepo wa sheria ya habari kwa kipindi kilichobaki hadi kukamilika kwa mradi huo.
Akifungua kikao hicho Mjumbe wa Bodi ya TAMWA Zanzibar Hawra Shamte aliwahimiza waandishi wa habari kuzitumia kalamu zao kwa ajili ya kufanya uchechemuzi juu ya upatikanaji wa sheria mpya na rafiki ya habari ili vyombo vya habari viweze kufanya kazi zao vizuri.
Alisema zipo sheria mbalimbali ikiwemo sheria ya adhabu, sheria ya Takwimu na sheria ya Uchaguzi zinawabana waandishi wa habari katika kutekeleza majukumu yao hivyo ipo haja ya kuongeza bidii ya kufanyiwa uchechemuzi.
Alisema kila mwaandishi wa habari anapaswa kujitolea kulisema hili kuhakikisha sheria hizo zinazonyima uhuru wa habari na kujieleza zinafanyiwa marekebisho ili kuwalinda waandishi wa habari katika majukumu ya kazi zao za kila siku.
Nae Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa habari Wanawake Tanzania TAMWA Zanzibar Dk Mzuri Issa ameviomba vyombo vya habari visichoke kuzungumzia masuala ya upatikanaji wa sheria mpya ya habari kwani jambo hilo linahitaji nguvu ya pamoja.
Mradi wa mapitio ya sheria za habari Zanzibar umeanza Agosti mwaka 2023 na unakamilika julai mwaka 2025 unatekeleza na TAMWA Zanzibar kwa mashirikiano ya Coman Welth Foundation.
Comments
Post a Comment