MAHAFALI YA PILI WAANDISHI CHIPUKIZI (YMF) YAMEFANYIKA LEO WAASWA KUENDELEZA HAYA
AMINA AHMED MOH'D.
SHEREHE ya mahafali ya pili kwa waandishi wa habari chipukizi Young media fellowship (YMF) imefanyika leo katika ukumbi wa Bima Kisiwani Unguja ambapo jumla ya wahitimu 24 waliopatiwa mafunzo kwa muda wa mwaka mmoja kupitia mradi wa kuandika habari zenye kuimarisha uongozi kwa wanawake kupitia vyombo vya habari wamepatiwa vyeti maalum .
Akizungumza na wahitimu hao kupitia Sherehe hiyo iliyoandaliwa na chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania Tamwa Zanzibar kwa ufadhili wa shirika la National endowment for democracy ( NED) mkurugenzi wa chama hicho Dk Mzuri Issa Ali amewataka waandishi hao kuendelea kushirikiana na chama hicho katika kutetea haki za wanawake ili kuweza kupata haki wanazostahiki ikiwemo masuala ya uongozi
Awali akizungumza Mjumbe wa bodi kutoka Tamwa Hawra Shamte kwa niaba ya mwenyekiti wa Chama hicho amewapongeza wahitimu hao kwa kufikia malengo ya mradi huo ambapo amewataka wahitimu hao kuendelea kutumia vyema kalamu zao katika kuwasaidia wanawake kuondokana na changamoto mbali na kuwaonesha wanawake kupitia vyombo mbali mbali vya habari .
Aidha amewataka wahitimu hao kujiwekea malengo ya kuwa waandishi wa habari ambao watakuwa wawakilishi wa wananchi wasio na sauti katika kupata haki zao mbali mbali badala yake kuendeleza kupaza sauti kwa uadilifu katika kutetea maslahi ya wanawake na makundi ya pembezoni.
Akizungumza kwa niaba ya wakufunzi wa wahitimu hao Shifaa Said amewataka wahitimu hao kuendeleza uandishi wa habari wenye maslahi ya jamii na kuondokana na uandishi wa habari wa matukio ambao hauleti tija kwa jamii.
Aidha amewataka wahitimu hao kudhibiti kufanya uandishi wa habari kwa kufanya mahojiano marefu kutoka kwa vyanzo vya habari ili kupatikana habari zenye kueleweka kwa uharaka zaidi.
Akisoma taarifa ya mradi huo wa kuimarisha uongozi kwa wanawake kupitia vyombo vya habari kaimu Afisa mradi huo Hairat Haji amesema kuwa wahitimu hao wamefikia kwa asilimia 99.9 malengo ya mradi huo ambapo jumla ya habari 347 kati ya 348 zilizohitajika zimeandikwa na kutumwa katika vyombo mbali mbali vya habari tofauti ikiwemo mitandao ya kijamii radio na magazeti habari ambazo zimefanyiwa utafiti.
Akitoa neno la shukurani kwa niaba wahitimu hao 24 ambao ni waandishi wa habari vijana Khadija Rashid Nassor amesema kuwa mafunzo hayo ya mwaka mmoja kupitia mradi huo yamekuwa chachu ya mabadiliko katika kuandika habari za maendeleo ambapo ameutaka uongozi wa tamwa kuendelea kuwatumia wahitimu hao katika kazi zao mbali mbali za habari katika kuibua na kuandika habari mbali mbali kwa lengo la kuleta maendeleo kwa taifa.
Nao baadhi ya wahariri ambao ni wadau wa habari za maendeleo kwa wanawake akiwemo Said Omar Said kutoka radio jamii mkoani ameushukuru uongozi wa Tamwa zanzibar katika kuwafundisha vyema waandishi wa habari vijana kuandika habari zenye tija na mabadiliko katika jamii
Katika Sherehe hiyo Wahitimu watatu kati ya 24 waliofanya vizuri katika kazi za habari hizo wametunukiwa zawadi maalum ambazo ni Laptop pamoja na vyeti maalum.
Mwisho.
Comments
Post a Comment