BIDII YAMUWEZESHA KUONGOZA HOTELI KUBWA
NA, THUWAIBA HABIBU, UNGUJA
TUNAAMBIWA mwenye kujitahidi hufaulu na hili limeonekana kwa mwnamke, Sylvia Godleven Moshi ambaye sasa anaongoza hoteli ya Golden Tulip Stone Town Boutique iliyopo Malindi, Unguja.
Hoteli hii iliopo karibu na bandari mbali ya kupokea watalii kutoka nchi mbali mbali ni kituo maarufu cha mikutano.
Mwanamke huyu ana miaka 25, lakini bidii zake za kujifunza ,kujiamini na ujasiri zimepelekea licha ya kuwa na umri mdogo kuaminiwa na kupewa dhamana hii kubwa ya kuwangoza wanaume na wanawake zaidi ya 80.
Kumbuka kuwa hawa wafanyakazi ni watu wa rika, tabia na mtazamo wa maisha tafauti.
Kama utafanya upelelezi wa kupitia hoteli nyengine za aina hii utaona uongozi wa hoteli wa nafasi hii amepewa mtu mwenye umri mkubwa kidogo, uzoefu wa muda mrefu wa kazi ya hoteli na wengi wao ni mwanamume.
Lakini mwana dada huyu amefanikiwa kuwa kiongozi wa hii hoteli kutokana na bidii ya kujituma na kujenga maelewano mazuri na wafanyakazi na wateja wanaofika hapo kupata huduma mbali mbali. .
Katika orodha ndefu ya majukumu yake ni pamoja na kusimamia wafanya kazi wote kwa shughuli walizopangiwa kufanya, kuajiri watu, kupanga mapumziko na likizo za wafanyakazi.
Alisema wakati wote huwa anajaribu kuhakikisha kila mfanyakazi anawajibika ili huduma za hoteli zibakie kuwa za kiwango cha juu kama wateja wanavyozitarajia kuwa.
Unapokuwa katika eneo lako la kazi na hasa kiongozi hutakiwi kuogopa au kumuonea mtu, bali kutumia sheria na taratibu za kazi’’, alieleza.
Binti huyu alipata elimu katika Chuo Kikuu cha Iringa ambako alisomea fani ya usimamizi rasilimali watu mnamo mwaka 2021.
Baadaye alipata mazoezi ya vitendo kwa miezi mitatu katika Tanzania Investment Bank ambapo ndipo alipoanza kupata ujuzi wa kazi anayoifanya hivi sasa.
Katika mwaka 2022 alipata ajira katika Hotel ya Golden tulip na kushika nafasi aliyokuwa nayo hivi sasa..
Nashukuru, sijahangaika sana kutafuta kazi na naaamini bidii yangu ndio ilionisaidia kuonekana kuwa nina uwezo wa kuongoza’’, aliongeza.
Dada huyu aliwataka wanawake wenziwe kuwania nafasi za uongozi zilizopo katika sekta mbali mbali kwa kuonesha utayari na uwezo wa kuongoza na kwa kufanya hivyo tu ndio watafikia malengo waliojiwekea.
Alisema kikubwa cha kufanya mbali ya kujiamini ni kuhakikisha unatekeleza na kutimiza majukumu yako kwa usahihi na vizuri unapokwama ukataka ushauri
Mwendo huu utawafaya wakubwa na wadogo waelewe uwepo wako katika eneo hilo.
Aliwataka wanawake wasiogope kuwa viongozi na kwa kufanya bidii na kushika nafasi za uongozi ndio patapatikana usawa wa kijinsia katika uongozi.
‘’Ukiwa mtaani unapata maneno mengi yanayovunja moyo ya kuwa hutoweza kuongoza muhimu ni kushikilia malengo yako tu’’, aliongeza.
Alisema katika safari yake ya uongozi alikumbana na changamoto ya kiumri na kimuonekano, lakini yote hayo hayakumrejesha nyuma ,bali yalimshajiisha kufanya juhudi zaidi ili waliokuwa na mashaka wabadili mtazamo wao.
‘’Nashukuru sikufikiwa na matatizo kwa sababu ya usichana wangu, lakini kidogo nilikumbana na shida mdogo na umbo langu. Nilitumia zaidi hekima kwa sababu naongoza watu walionozidi miaka na wengine wenye rika na wazazi wangu’’, alieleza
Kilichosaidia zaidi ni kuzitumia sheria na taratibu za kazi kama muongozo wa kufanya kazi yake na kwa vile sheria ni msumeno basi hakuchelea kuhakikisha unamkata kila aliefanya makosa.
Alisema changamoto ziko kila sekta na sehemu zote ujasiri ndio ngao pekee ya kupata suluhisho, lakini kuwa tayari kujifunza zaidi na kupata mawazo mapya ili kuwa kiongozi bora
Msimamizi mkuu wa ghala ya hio hoteli, Masoud Juma kitwana, alielezea kufurahishwa na uongozi wa huyu dada na zaidi kwa kuonyesha mashirikiano na wafanyakazi.
Kubwa zaidi ni kwamba anawatendea wafanyakazi wote haki.
"Ni binti mwenye hekma na busara na hana majivuno au dharau kwa kuwa anashika nafasi ya uongozi’’, aliongeza.
Mfanyakazi mwengine wa hoteli, Shaibu Magoma alisema uongozi wa huyu dada ni mzuri na wanatamani wabakie kuwa naye kwani ana roho ya kibiadamu ni muelewa wakati mtu akipata matatizo.
Vile vile anapokea mawazo yanayotolewa na wafanyakazi na watu wengine na husaidia kutatua shida za wafanya kazi.
Kwa ujumla, uongozi wa hoteli wa dada huyu mwenye umri mdogo ni kielelezo chengine katika jamii yetu kwamba sifa ya uongozi sio umri au jinsia, bali wa jitihada za mtu na namna anayoweza kushirikiana na wenzake katika kazi.
Comments
Post a Comment