NJIA WANAZOTUMIA VIJANA WA KIKE KUWA VIONGOZI.
THUWAIBA HABIBU
Kasumba ni kilevi kinachompotezea mtu mwendo sahihi wa kufikiri na kufanya maamuzi.
Hii ndio iliopelekea jamii kumueleza mtu mwenye mawazo potofu na anayeukataa ukweli kuambiwa ana kasumba, yaani hajielewi na maamuzi yake hayatautiani na aliyetumia kasumba.
Katika jamii wapo watu wenye kasumba katika medani ya siasa na kuona na kutaka wengine waamini kuwa mwanamke hawezi kushika nafasi ya uongozi.
Watu hawa hujiona waposahihi kuhukumu au kuchukia wenzao kwa sababu zisizo za msingi na zisiokuwa na mantiki.
Kwa muda mrefu ipo kasumba katika jamii ya watu wengine kuona viongozi wazuri ni watu wenye umri wa makamo, watu wazima au vikongwe.
Hali hii ndio iliopelekea serikali yetu kuweka nafasi maalum za uongozi kwa vijana kwa njia ya kuteuliwa na katika miaka ya karibuni tumeona vijana wanashajiika kuzitafuta nafasi za kuwa wagombea katika chaguzi za ngazi mbali mbali.
Katika hili kundi la vijana, wamo wanawake waliogombea uongozi katika vyama vya siasa na miongoni mwa nafasi walizozitaka ni za makatibu, wenyeviti na wajumbe wa kamati mbali mbali.
Hii imepelekea nchi yetu kuwa na vijana ambao ni Wawakilishi, Wabunge na Mwaziri, tafauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Woga na hofu waliokuwa nayo wanawake inatoweka pole pole, lakini bado vipo vikwazo vinavyorejesha nyuma malengo ya baadhi yao
Hata hivyo, wapo vijana wa kike walioonyesha ujasiri na kufanikiwa kushika hatamu za uongozi.
Jamila Gorafa Hamza, mwenye ulemavu wa uoni, alitumia njia kadha kuwa kiongozi na amethibitisha fikra za kuwadharau watu wenye ulemavu kuwa ni kasumba inayofaa kufukiwa ardhini na kuwa sehemu ya historia.
Huyu ni mmoja wa wanawake waliowaonyesha vijana, hasa wanawake, kwamba kila mtu anao uwezo wa kuongoza na kutimiza majukumu yake kwa ufanisi.
‘’Nilijiunga na darasa la itikadi la Chama cha Mapinduzi (CCM) ili kupata elimu na uzoefu wa uongozi’’, alisema.
Elimu hio ilipelekea achaguliwe mjumbe wa kamati ya utendaji ya tawi la CCM la Mwanakwerekwe na juhudi zake katika mwaka 2020 zilimuwezesha kuingia katika kamati utendaji ya jimbo. Huko alipata uelewa zaidi juu ya kazi na wajibu wa kiongozi.
Baada ya mwaka mmoja aligombea katika uchaguzi wa wilaya, lakini hakufanikiwa kwa vile wapiga kura wengi walikuwa na sababu zao za kutomuunga mkono, mojawapo ikiwa alikuwa mdogo wa umri.
Muono huo haukumkatisha tamaa na ilipofika mwaka 2021 alishiriki katika Baraza la Vijana akiwa mjumbe kwa upande wa Zanzibar kwa kupata asilimia 80 ya kura.
Katika mwaka 2022 alikuwa mjumbe wa Wilaya ya Magharib "B" na anaitumikia nafasi sio hadi
Jamila alisema anakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwa pamoja na baadhi ya wanajamii kuwa na ati ati na uwezo wa watu wenye ulemavu
Alisema uchumi mdogo wa vijana wanawake, hususa ni zinapofanyika kampeni za kugombea uongozi, umekuwa kikwazo.
Hili hujitokeza zaidi kwa kupata usafiri kwa vile hulazimika awe na msaidizi wa kumpeleka huku na kule kwa vile baadhi ya watu wanaona kufanya hivyo ni kama kutwishwa mzigo wasiotaka kuubeba.
Matatizo mengine ni ukosefu wa vitendea kazi na hii inadhoofisha juhudi za kuwania nafasi za uongozi.
Katibu wa Siasa Itikadi na Uenezi katika Wadi ya Kijitoupele, Riziki Abdallah Ali, ambaye alikuwa Spika mstaafu wa Bunge wa serikali ya wanafunzi ya Chuo Kikuu Cha Zanzibar (ZU) alisema alipata mafunzo katika Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kupitia mradi wa kuinua wanawake kiungozi (SWiLL) .
Mafunzo hayo yalimfanya kuwa imara, jasiri na kuelewa namna ya kuongoza na majukumu ya kiongozi.
Kabla ya mafunzo alikuwa na fikra potofu juu ya kijana kuomba uongozi wa ngazi ya juu kwa sababu ndani ya CCM upo umoja wa vijana (UVCCM) na alidhani hairuhusiwi kijana kugombea nafasi hizo katika chama.
Baada ya mafunzo amekuwa akitoa elimu kwa vijana wenzake ambao nao walikuwa na fikra kama zake.
Pia alihamasisha wenzake wa tawani katika Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) kugombea uongozi kama wafanyavyo wanaume.
‘’Nashukuru walijitokeza kugombea, lakini hawakubahatika. Hata hivyo, sasa woga wa wanawake kugombea umepungua na tunaahidi kujitokeza kugombea nafasi mbali mbali katika uchaguzi wa mwaka 2025’’’, alieleza.
Rahima Mussa Hassani alikumbana na changamoto katika familia yake ambazo zilitaka kukwamishwa malengo yake ya kuwa kiongozi, lakini hakusita kuelimisha kwamba jinsia zote zina haki ya kugombea uongozi.
Alifanya mazungumzo na wenzake ya kutafuta njia nzuri ya kufikia malengo yao ya kushika hatamu za uongozi.
Binti huyu alisema yeye ni mmoja wa wale waliopitia changamoto katika familia, lakini hakukata tamaa.
Alisema kuna watu ambao wanatawaliwa na mfumo dume na kuamini mwanamke sio sehemu ya utawala katika jamii, bali ni wa kutawaliwa
Maimuna kassim Yusuf ambaye pia ni mnufaika wa mradi wa SWILL alisema aliwataka wanawake wenzake wamchague akigombea nafasi mbali mbali, ikiwemo ya kuwa mjumbe wa kamati ya utendaji katika chama cha mpira wa miguu cha Wilaya ya Kati
Alisema mradi ulimjengea uwezo wa kugombania nafasi ambazo zilifikiriwa wanaume tu ndio wanaozimudu.
Kwa mtazamo wake wakati umefika wa kuwawezesha wanawake wengine kuingia katika uongozi na hususa vijana wa kuanzia miaka 15 ili watoe mchango wa kuijenga nchi.
Mratibu wa kuinua wanawake katika uongozi kutoka TAMWA, Mariyam Ame Chumu, alisema wanachukua hatu za kuwasaidia wanawake kushiriki katika uongozi
Hii ni pamoja na kutoa elimu ya kujitambua, kujielewa na kuthubutu kuwa wagombea huku wakizijuwa haki zao za kidemokrasia.
Vile vile wanatola elimu ya na namna ya kujilinda na rushwa na kujuwa sheria za uchaguzi zinavyowalinda wanapokuwa katika harakati za kugombea uongozi
Katika mradi huo vijana huunganishwa na wanasiasa wakongwe ili kupata uzoefu na kuhamasika kuchukua nafasi za uongozi.
wanazopambana nazo ni pamoja na kuitaka jamii ikubali mwanamke anao uwezo wa kuongoza na kuachana na mila na desturi zinazomkwamisha mwanamke kupata nafasi ya kuongoza wenzake
Kwa sasa mradi wa TAMWA umepunguza matatizo yanayomkatisha tamaa mwanamke asijitokeze mbele kugombrea uongozi.
Jambo muhimu ni kuondoa hofu na kujichanganya na watu wote ili uwezo wao uonekane.
Kwa kweli huu sio tena wakati wa kurejeshwa nyuma wanawake kwa kutumia kasumba ya kuona mwanamke hawezi kuongoza. Ni wakati wa kuendelea na safari ili wanawake kama wanaume wawe na haki sawa ya kugombea uongozi.
Jambo muhimu ni kwa wana jamii kutoibaguana kijnsia na badala yake waende sawia katika uongozi wa nchi yetu.
Hapa inafaa kukumbushana kwamba mwanamke ni mwalimu, mtu mwenye ujasiri, hekima na busra na sio vyema kudhara sifa hizi panapokuja suala la uongozi.
mwisho.
Comments
Post a Comment