MAUMIVU YA MWANAMKE YAKOMBOA ZAIDI YA WATU 2000 KIUCHUMI.


NA THUWAIBA HABIBU, UNGUJA. 

HISTORIA inaeleza kuwa kabla ya kuja  kiongozi wa dini ya Kiislamu, Mtume Muhammad (SAW),  wanawake walionekana kama bidhaa isiyo  thamani.
Kwa bahati mbaya, licha ya dini ya Kiislamu kukemea mwendo huo, bado wapo watu  wanaokataa kutambua uwezo na mchango wa mwanamke katika kuiletea jamii maendeleo. 

Hali hii pia ilikuwepo hadi mwaka 1996 katika Wilaya ya Kati,  Unguja, ambako wanawake walioachika (wajane)walikuwa wakipitia hali ngumu ya maisha.
Baadhi yao wakahadaika na kusahau thamani ya utu wao na kutumia miili yao  kujipatia pesa za kujihudumia wao na watoto walioachiwa baada ya waume kutengana nao.
Mwenendo huu ulimsononesha binti mmoja ambaye ndoa yake ilikuwa mpya  na kutokea kupendwa na wenzake.
Alisema alijiuliza maswali mengi, mojawapo ni kwa nini shida za maisha ziwapelekee akina mama kupoteza utu na heshima yao katika jamii?

Baada ya kuitafakari hali hio aliamua kuanzisha upatu, mfumo maarufu wa kusaidiana unaotumika Visiwani tokea dahari na enzi, ili kuwaondoa akina mama hawa katika ihililaki waliokuwa nayo na kukosa msaada wa kuondokana nayo.


Kitu cha kwanza alichokifanya binti huyu, Lela Hamadi,  ni kuanzisha upatu uliowaleta  pamoja wanawake hawa na wengine katika mwaka 1997 na kuelewa kwa kina matatizo waliokuwa wanapitia

Mbali ya kuingia katika upatu huu pia alikuwemo katika upatu mwengine  uliomuwezesha kupokea  shilingi 150000.
Thamani ya fedha hizo kwa wakati ule unaweza kusema ni kama mara tatu au zaidi ya hivi sasa ulizingatia bei za bidhaa za wakati huu.

Dada huyu anayekaa koani alikwenda kwao Unguja ukuu  Tindini  ili kununua kiwanja
Lakini wakati akiwa kwao alitokea ndugu yake mmoja aliyemkopa shilingi 50,000  na hio kumkawilisha kutimiza malengo yake.

Baada ya mwaka mmoja yule ndugu yake alimrudishia pesa na ziada ya shilingi 10,000.

Alipomwambia mbona alizidisha shilingi 10,000 jawabu aliyopata ni kwamba hio ziada ni zawadi kwa sababu asingepata  mkopo asingeweza kufanya shughuli aliyekusudia ambayo ilimletea tija.

Ndugu yake alimuelezea kuwepo vikundi vya wajasiaria mali na akapelekwa kwa kiongozi wa hivyo vikundi ambaye ni mwalimu na kuwakuta wanafanya mgao wa pesa.
Hapo ndipo alipopata elimu juu ya faida ya kuwa na kikundi na wajasiria mali na wanachama kujumuika kucheza upatu.

Alitembezwa kuona shughuli za vikundi vinne na aliporudi kijijini Koani aliamua kufanya kama watu wa Unguja Ukuu ili kuwasaidia wanawake wenzake.

Sasa akiwa na miaka 46, Bi Lela anasimamia vikundi kwa miaka 22 na kutumia elimu  aliyopata  kuwaelimisha wanawake wenzake juu ya faida ya kuwa na vikundi, hasa kwa wanawake waliokuwa na hali ngumu ya maisha.
Haikuwa kazi rahisi, lakini hakukata tamaa pale alipoona muitiko sio mzuri.

Katika mwaka 2000 alifanya zoezi jengine la  kutoa elimu ya vikundi vya  ujasiria mali na mafanikio hayakukidhi haja.
Hapo tena akaona aonyeshe njia ya kujikwamua kimaisha kwa kuanzisha biashara ya visheti, kazi iliyopelekea  watu  kumjuwa zaidi kwa vile alitembeza biashara yake mitaani.

Mnamo mwaka 2001, Bi lela alishirikiana na katibu wa sheha wa Unguja Ukuu, Mzee Hassani  Ameir, kuwapatia elimu ya vikundi watu katika kanda yake ya Koani.

Kwa kuanzia walipatikana  watu 15 ambao kila mmoja alitakiwa kutoa shilingi elfu 2000 ili kununua vifaa vya kuanzisha biashara. Jumla ya fedha zilizopatiana zikawa shilingi 30000.

Kwa bahati mbaya baadhi ya wanawake  walitiwa maneno na waume zao waende kuchukua  pesa kwa vile ulikuwepo uwezekano wa kutapeliwa.

Watu 10 walidai na kupewa pesa zao na kubakia watano na kibindoni kuwepo shilingi 10000 tu.

Sintafahamu hii ilimrudisha kwa mwalimu Hassani ambaye alimshauri atafute shilingi 60000 na akaamua acheze upatu ili kupata hizo pesa.

Alipozipata pesa mnamo mwaka 2002 akafunga safari ya kwenda  Unguja Ukuu Tindini  kuzipeleka na akapewa kisanduku, mabuku, peni, penseli, muhuri ili kuratibu shughuli za kikundi atachokianzisha.

Aliitisha kikao katika uwanja uliopo nje ya nyumba yake kuwataka watu kujiunga  na kikundi na  hapo ndipo imani ya wanakijiji wa Koani ikarudi na kupata watu 24 
Mwalimu alimtembele Pale kikundi kilipopata watu 30 kwa vile sheria inaeleza kuwa kikundi kinatakiwa anagalau kuwa na watu watu 15.

Katika kikao hicho pakafanyika uamuzi wa taratibu za kikundi na namna mgao utavyokuwa na kueleza njia mbali mbali za kuendesha kikundi kwa uweledi.

Upatu ulichezwa kwa mwaka mzima na hapo ndipo ukaanza mgaowa kila mtu kupata shilingi 78000. Matokeo hayo yaliwafurahisha wana kikundi na kuiona faida ya umoja na kuwa na upatu.

Kilichofuata ni wanachama kuweza kuchukua mikopo ili kuendeleza biashara zao  na yeye alikuwa mmoja wao aliyetumia mkopo huo kuendeleza biashara yake ya visheti.

Kikundi kikaimarika na kupata wanachama zaidi na kwa vile wapo waliokuwa waishi mbali kidogo Bi Lela akakigawa kikunde sehemu mbili, kimoja cha watu wa Charawe na chengine cha watu wa Jambiani
Mwalimu mwengine , Mustafa Makame Mgeto,  baada ya kuona alikigawa kikundi sehemu mbili akamteua kuwa kiongozi wa vikundi hivyo
Bi Lela alisema hakutaka kuchaguliwa kushika nafasi ya uongozi, lakini kutokana na yule tomwalimu na wanawake wenzake kuwa na imani naye  alikubali kubeba dhamana hio.

Kazi yake ya kwanza ilikuwa kuandika barua na kuipeleka Jozani katika Jumuiya ya Mikopo na Maendeleo( JOCDO) ambapo alipatiwa mafunzo ya kuongoza vikundi
Baada ya mafunzo akapewa kazi ya kutoa elimu kwa watu wa  Umbuji na matokeo yake ni kuibuka kwa vikundi vitano katika eneo Hilo 
Alisema alijikuta anachaguliwa mwalimu mkuu wa vikundi vya kanda ya Uzini
Niliongeza juhudi na kuanzisha  vikundi katika maeneo tofauti  ndani ya kanda yangu, Koani vikundi 19 , kitumba 9, kidimni 11,ubago 4, mpapa 3, umbuji 5, pagali 1,tunduni 3, mchanga 3, dongonwe 2, gana5, kiboje 4 na Mwera 2, alieleza kwa sauti ya furaha.
Idadi ya vikundi ikawa 68, kila kikundi kikiwa na watu 30 na kwa vikundi kuw na wanachama 2070 abao walipatiwa elimu ya kufanya kazi kwa pamoja.
Alisema nje ya kandayake alipata vikundi 15 viliokusanya watu 570 katika maeneo ya Fumba, Bweleo, Kisakasa, Kibaha, Kisarawe , Mwanza, SOS, Darajabovu na Kaskazini A.
Alitoa elimu sehemu zote hizo na kuwa karibu na wanachama wake ili waweze kuojikomboa na kuacha kudhalilishwa na wanaume.
Namshukuru Mungu nimefanikiwa kwa kiasi fulani, alisema.
Hivi sasa wapo  wanavikundi  ambao wanamiliki biashara za maduka na nyenginezo na anaona fahari na kufurahia mafanikio hayo kwa vile alitoa mafunzo yaliyozaa matunda.
Wapo pia, yeye akiwa mmoja wao, walioweza kupata kupata pesa za kusomeshea watoto wao kwa vile watoto wanamtegemea yeye kwa vile  sasa ni mjane aliyefiliwa na mumewe.
Mshika hazina wa kikundi kiitwacho "sisi tushindwe tuna nini,"Nusura Ali , alisema jambo kikubwa linalompoa faraja ni kuona anaweza kuchukua pesa na kumsomesha mtoto wake.

Katika  kikundi chengine kinacho itwa Hizo ndio fikra zenu wanachama walieleza kufurahia mafanikio waliyoyapata na sasa wengi wameachana na tabia  ya kusubiri waume  zao au watu wenggine kuwapa pesa za matumizi.
Kwa muhtasari, huu ni mfano mmoja tu wa mafanikio na uwezo wa manamke wa kuwa  kiongozi mzuri na anayeweza kuonyesha njia ya mafanikio inayowakomboa watu na shida za maisha.
    mwisho

Comments

Popular posts from this blog

BARABARA 19 KUJENGWA KWA KIWANGO CHA LAMI PEMBA KUKAMILIKA DISEMBA 2024.

WAZAZI ZIDISHENI KUFUATILIA NYENENDO ZA WATOTO HUSUSAN NI VIJANA .

UONGOZI WA WILAYA CHAKE CHAKE KFHI WAPONGEZA JUHUDI