MABADILIKO WATENDAJI ZRA PEMBA WALETA MATUMAINI KWA WAFANYA BIASHARA
NA, AMINA AHMED MOH’D - PEMBA.
BAADHI ya Wafanya Biashara wilaya ya Mkoani mkoa wa Kusini Pemba wamepongeza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na mamlaka ya mapato Zanzibar ZRA juu ya maswala ya utolewaji wa elimuya kodi na hatua za ukusanyaji wa mapato ukilinganisha miaka iliyopita.
Kauli hizo zimetolewa na wafanya biashara kutoka mitaa na maeneo mbali mbali ya wilaya hiyo walipokuwa wakizungumza mbele ya Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mapato Zanzibar ZRA Pemba Jamal Hassan Jamal aliefika ndani ya wilaya hiyo kuzungumza na kusikiliza changamoto za wafanyabiashara maeneo tofauti ikiwa ni mwezi maalum wa kurejesha shukurani kwa walipa kodi ulioandaliwa na mamlaka hiyo.
Wamesema suala la utolewaji wa taaluma juu ya njia sahihi za ulipaji kodi zimeimarika na jambo ambalo awali lilikuwa ni changamoto kubwa kwa wafanya biashara na watendaji wa mamlaka hiyo katika kukusanya mapato.
Tunashukuru ZRA Pemba watendaji wamebadilika tofauti na awali uelewa na taaluma wanazidi kutupatia kila tunapohitaji,wamekuwa karibu sana na sisi wamekuwa marafiki ambao wanatuhamasisha kuwa walipaji kodi kwa hiari zile vuta ni kuvute zimepungua". Alisema Yussuf Mussa Makame Mfanya biashara wa saruji, pamoja na mbao Mkoani .
Aidha Wafanya biashara hao wameiomba mamlaka hiyo kuwashirikisha kunapotokea mabadiliko katika taratibu mbali mbali za ulipaji a kodi.
" Tumezipokea shukurani zenu hizi kwa mikono miwili na sisi tunaahidi tutaendelea kuiunga mkono serikali kwa kuwa walipa kodi wazuri, kodi ambazo zinarudi kwetu kufanya maendeleo mbali mbali".
"Kunapotokea mabadiliko yeyote mtushirikishe sisi wafanya biashara kwa sababu hatuna lengo la kukwepa kulipa kodi sote tunajenga nyumba moja hivyo mabadiliko yanayotuhusu walipa kodi msiyakalie kimya yakitokea mtuambie ili mnapofanya mabadiliko tusiwe tunalalamika".alisema mfanya biashara Said Hemed
Katika Hatua nyengine wafanya biashara hao wameishukuru Serikali ya awamu ya 8 kwa kuendelea kuleta maendeleo katika wilaya hiyo ikiwemo ujenzi wa masoko, uimarishwaji wa bandari kutoa fursa kwa wafanya biashara, na kuwakubalia maombi yao katika kuwekeza na kujenga vyanzo vipya vya kufanyia biashara.
"Maendeleo ya wazi wazi tunayaona sisi kama wafanya biashara kwetu hili ni jambo la faraja tunapata moyo zaidi katika kulipa kodi, tunaona barabara zinajengwa, mahospitali na vifaa, bandari masoko vyote hivyo ni kwa muda mchache wa awamu hii ya nane tunatamani rais wetu akae siku zote asiondoke tena kwa sababu kile kilio tulichokuwa tunalia zamani kimeondoka tulikuwa tunalilia maendeleo na yamekuja kwa kasi na yanaendelea"alisema Hemed Muhammed mfanya biashara wa Vifaa vya ujenzi na vyombo vya moto.
Mkurugenzi wa ZRA Pemba Jamal Hassan Jamal Amesema lengo la kutembelea walipa kodi wa hiari waliofanya vizuri katika wilaya hiyo kwa mwaka 2023 ni kurejesha shukurani kusikiliza changamoto sambamba na kupokea maoni katika kuimarisha zaidi utendaji kazi wa mamlaka hiyo.
Aidha Jamal amesema mamlaka hiyo itaendelea kushirikiana vyema na walipa kodi katika kuona malengo yaliowekwa na serikali juu ya kuboresha maendeleo katika nyanja mbali mbali yanafikiwa.
Hata hivyo amewataka wafanya biashara kuendelea kutoa mashirikiano na mamlaka hiyo ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa wanapokabikiwa na changamoto mbali mbali juu ya mifumo ya ulipaji kodi.
Miongoni mwa maduka hayo yaliotembelewa ni Pamoja na Maduka ya biashara za vyakula, vipodozi, mbao, Saruji, Nguo na mengineyo kutoka maeneo mbali mbali ndani ya wilaya hiyo.
Mwisho
Comments
Post a Comment