WIZARA YA AFYA PEMBA YATOA NENO KWA WANAOSAMBAZA UVUMI KUHUSU MAGONJWA YA MIRIPUKO.
NA AMINA AHMED MOH'D, PEMBA.
WIZARA ya Afya Zanzibar imewataka waandishi wa habari pamoja na wahudumu wa Afya ya jamii CHV kungana pamoja katika kuiweka salama jamii juu ya majanga ya miripuko mbali mbali kwa kuelimisha na kutoa taarifa kutoka kwa vyanzo vyenye usahihi ili kuepusha mitafaruku inayowapata wananchi kutokana na uvumi hususan katika msimu wa mvua zinazoendelea kunyesha.
Mafunzo hayo ya siku moja yamewashirikisha Wahudumu wa Afya jamii CHV, Wilaya ya Micheweni, Wete, Chake na Mkoani pamoja na waandishi wa radio za kijamii zilizopo kisiwani Pemba, Tv za mitandaoni, Pamoja na baadhi ya Vyombo vya habari vya Serikali kisiwani humo.
Kauli hiyo imetolewa na Afisa Mdhamini Wizara ya Afya Pemba Khamis Bilali Ali alipokuwa akizungumza na baadhi ya wanahabari wa vyombo mbali mbali pamoja na wahudumu wa Afya jamii CHV kiswani Pemba katika mafunzo maalumu juu ya kudhibiti kusambaa kwa uvumi na maneno mbali mbali katika vipindi vya majanga huko Samail Gombani Chake.
Amesema makundi hayo yanayonafasi kubwa katika kusaidia jamii kuwa na uwelewa wa kutofautisha uvumi na taarifa potofu kwa kuweka usahihi kwa jamii na kuwaepushia hofu ambayo hupelekea taharuki kwa wananchi.
"Mtaani humo kunatolewa taarifa tofauti, watu wanatunga tu mambo mara mvua zimeanza wagonjwa wakipindupindu wameshapatikana 100 wengine wameshakufa jambo ambalo halina ukweli wala halijulikani limetokea wapi, Ili tuendelee kuilinda jamii ya Pemba juu ya majanga kama haya ya kipindu pindu ambayo kwa zaidi ya miaka 6 hayajajitokeza ni nyinyi CHV kushirikiana na wanajamii kutoa elimu, kwa kushirikiana na waandishi wa habari".
"Wao wanaelimisha kupitia vyombo vyao vya habari baada ya kupata usahihi kutoka wizara ya afya na nyinyi mnaifikia jamii moja kwa moja kuwapa elimu ambazo mmepewa na wizara, juu ya mambo mbali mbali ikiwemo kutunza mazingira, kutumia chanjo, usafi na mambo mbali mbali ambayo yatasaidia
kupatikana kwa afya salama juu ya majanga mbali mbali kwa wananchi ".
Aidha wizara ya Afya mesema kuwa mamlaka ya kutoa taarifa endapo nchi itapatwa na janga lolote la maradhi mbali mbali ni dhamana ya wizara hiyo hivyo kusambaza uvumi ambao hautakuwa na ukweli ndani yake ni moja kati ya sababu ambazo hupelekea kuongeza taharuki na hofu kwa wananchi wenzao ambapo amewaasa watu wenye tabia hizo kuacha mara moja.
"Radio vifua mitaani huko mara kumetokea janga hili mara janga lile hizo tabia tuziwache mara moja za kuomba majanga, juu ya janga lolote litakalojitokeza wizara itawajuilisha wananchi kupitia waandishi wa vyombo mbali mbali, wala hatuombi kutokee majanga na ndio mana wizara haisinzii katika kuona wananchi wanakuwa salama tahadhari za kila aina zinachukuliwa".
Kwa upande wake mkuu wa kitengo cha elimu ya afya Zanzibar Bakar Hamad Magarawa alisema kuwa lengo la kutolewa mafunzo hayo yaliyowashirikisha wanahabari na wahudumu wa afya jamii ni kusaidia kuongeza uelewa kwa wananchi juu ya kutofautisha uvumi na kujua usahihi wa taarifa mbali mbali za majanga.
"Imekuwa ni desturi kila inapotokea janga uvumi unakuwa mwingi kuliko usahihi, lilipotokea janga la korona apa uvumi ulishika kasi hofu kwa wananchi zikajaa kiasi ambacho mtu anaogopa hata kukohoa, ili kuepusha hayo tumeona ipo haja kutoa elimu hii kwa vile nyinyi ni watu ambao mnaaminika zaidi na jamii. "
Akizungumza afisa mawasiliano magonjwa ya miripuko kutoka Shirika la Afya Duniani W. H. O. Julieth Rangi amewaasa washiriki wa mafunzo hayo kuweka mikakati maalum katika kuelimisha jamii juu ya magonjwa ya miripuko na majanga mbali mbali kwa kushirikiana na wizara hiyo ambapo shirika litaendelea kushirikiana katika kuiweka jamii iliyo salama.
Mafunzo hayo ya siku moja yamewashirikisha Wahudumu wa Afya jamii CHV, Wilaya ya Micheweni, Wete, Chake na Mkoani pamoja na waandishi wa radio za kijamii zilizopo kisiwani Pemba, Tv za mitandaoni, Pamoja na baadhi ya Vyombo vya habari vya Serikali kisiwani humo.
Mwisho
Comments
Post a Comment