TRA MKOA WA KIKODI PEMBA WATAKIWA KUONGEZA VYANZO VIPYA VYA UKUSANYAJI WA MAPATO KISIWANI HUMO .
NA - AMINA AHMED MOH’D PEMBA.
NAIBU waziri wizara ya Fedha Tanzania Hamad Hassan Chande ameitaka mamlaka ya mapato Tanzania TRA mkoa wa kikodi Pemba kufanya utafiti utakaosaidia kupata vyanzo vipya vya mapato sambamba na kuzidisha uimarishaji wa mifumo ya ulipaji wa kodi mbali mbali zinazokusanywa na mamlaka hiyo .
Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na watendaji wa mamlaka hiyo, viongozi wananchi, taasisi za serikali na binafsi katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya kurejesha shukurani kwa walipa kodi iliyoandaliwa na mamlaka hiyo mkoa wa kikodi Pemba katika ukumbi wa Sun set Wesha Nje kidogo na mji wa Chake Chake.
Amesema licha ya kuvuka malengo ya makusanyo yaliowekwa na mamlaka hiyo mkoa wa kikodi Pemba ipo haja ya kufanya utafiti maalumu wa kuongeza vyanzo vipya vya mapato ambavyo vitasaidia kuongeza kodi zitakazotumika kwajili ya kuleta zaidi maendeleo nchini, pamoja na kuweka mifumo imara itakayosaidia walipa kodi kudai risiti za kielectoniki.
Aidha naibu huyo amewataka watendaji wa mamlaka hiyo kuendelea kushirikiana na taasisi, serikali pamoja na wananchi katika kuhakikisha wanaendelea kufanya kazi ya ukusanyaji wa mapato bila kutumia mabavu, wala kugombana na walipa kodi wao ambao ni wananchi.
Akizungumza katika kilele hicho kwa niaba ya kamishna wa TRA Tanzania meneja wa TRA Zanzibar Saleh Haji Pandu amesema kuwa kuvuka kwa malengo ya makusanyo mkoa wa kikodi Pemba kumetokana na kuongezeka hamasa kwa wananchi ambao ni walipa kodi ambapo amesema mamlaka hiyo itaendelea kuiunga mkono serikali na kuonesha mafanikio ya kikazi kwa mamlaka hiyo katika makusanyo mbali mbali.
Nae kwa upande wake Meneja wa TRA mkoa wa kikodi Pemba Arif Said Amesema kuwa mamlaka mkoa huo itaendelea kuhamasisha jamii ikiwa ni pamoja na kutoa elimu juu ya kodi kwa kuzitumia fursa mbali mbali.
Akitoa salam za mkoa wa Kusini na Kaskazini Pemba Mkuu wa mkoa wa Kusini Pemba Mattar Zahor Massoud Ameipongeza mamlaka hiyo ya TRA kwa kuendelea kuisaidia serikali kukusanya kodi kwa kutumia busara bila kuwasumbua walipa kodi ambao ni wananchi kwa namna yeyite ile ambapo amesema TRA mkoa wa kikodi Pemba ni miongoni mwa mamlaka pekee ambayo haijawahi kulalamikiwa na wananchi katika utendaji kazi wake.
Aidha Mattar amezitaka taasisi nyengine kuiga mfano huo wa TRA katika kukusanya mapato kwajili ya maendeleo ya nchi bila kutumia nguvu sambamba na kukusanya kodi kwa misingi ya kistaarabu kama inavyoelekezwa na viongozi wa nchi akiwemo Dk Samia Suluhu Hassan pamoja na Hussein Ali Mwinyi rais wa Zanzibar ili kufikia malengo yaliokusudiwa.
Katika kilele hicho Naibu waziri huyo pia Alikabidhi zawadi kwa walipa kodi waliofanya vizuri mwaka 2023 huku Mamlaka hiyo mkoa wa kikodi Pemba ikiwa imevuuka lengo la makusanyo ya kodi na kufikia asilimia 100. 9 ukilinganisha na mwaka uliopita.
Mwisho
Comments
Post a Comment