WANAFUNZI MWAMBE WATAKIWA KUTOA TAARIFA WANAPOVUNJIWA HAKI ZAO.
NA Is-haka Rubea.
WANAFUNZI wa Skuli za Mwambe za Dkt. Samia Suluhu Hassan Sec, Dkt. Hussein Mwinyi Msingi na Mwambe Msingi wamehimizwa juu ya muhimu ya kutoa taarifa pale wanapokubwa na changamoto mbali mbali zikiwemo za viashiria vya vitendo vya kufanyiwa uzalilishaji wa kijinsia.
Wito huo umetolewa na Mratibu wa Chama cha Waandishi Wanawake Tanzania, Zanzibar Tamwa Fat-hiya Mussa Said wakati akiwasilisha mada juu ya Changamoto zinazowakabili watoto katika mafunzo yaliyoandaliwa na Shirika la Save the Children na kuwajumuisha wanafunzi wa Skuli hizo.
Amesema zipo changamoto nyingi zinazowakumba watoto ikiwemo unyanyasaji wa kijinsia, kimwili, kingono, kutekelezwa na nyengine nyingi lakini watoto hao wamekuwa wakishindwa kuziripoti jambo ambalo husababisha wafanyaji kuendelea na vitendo hivyo wakitambua kuwa hawaulizwi.
Alisema watoto hao wanapaswa kuwaeleza wazazi wao, walimu, viongozi wa dini na watu wengine wa karibu kila wanapohisi kuwa kuna viashiria vya kufanyiwa unyanyasaji ili kuweza kuzuiwa visifanyike na wale ambao hubahatika kufanyiwa kwa hila au nguvu za aina yoyote wasisite kutoa taarifa hizo katika wakati muafaka.
Alisema kuwa katika eneo hilo la Mwambe yapo matukio kama ya ulawiti kwa watoto na watoto wenzao, ubakaji, ndoa za umri mdogo lakini kutokana na kunyamaziwa na watoto wanaofanyiwa huwa haziwezi kubainika hadi pale wanapoweza kubainika na kulazimishwa kusema ndipo hueleza huku wakiwa wameshachelewa.
Kwa upande wake Afisa Mradi Jumuishi katika Shirika la Msaada kwa watoto la Save the Children John Maftah alisema kuwa kila mtoto anayo haki ya kulindwa na vitendo vya ujatili ikiwemo kupigwa, kutelekezwa, kupakwa au kuozweshwa mume akiwa bado na umri mdogo.
Alisema kuvujwa kwa haki za watoto ni kinyume na haki za binadamu za juwakosesha haki zao za msingi ambapo Save the Children imekuwa ikishirikiana na wadau mbali mbali katika kuona haki za mtoto zinalindwa kwa mujibu wa sheria ya mtoto ya Zanzibar Sheria namba 6 ya mwaka 2011.
Naye Afisa Takwimu Katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Wilaya ya Mkoani Moh`d Abdalla aliongeza kusema kuwa watoto wengi wa mwambe hufanyiwa vitendo vya udhalilishaji lakini hushindwa kuripoti licha ya ofisi yake kupokea taarifa hizo kila kukicha huku Mwambe ikiongoza kwa matukio hayo.
Akizungumzia mafunzo hayo mwanafunzi Subira Khamis Juma wa Skuli ya Sekondari ya Dkt. Samia alisema ukimwa wao ulitokana na kutokujua wapi na namna gani wanaweza kutoa taarifa za udhalilishaji unapotokea kwao.
Naye Ibra Ali Bakari alikadhia kwa kusema kuwa kutokana na kupata elimu hiyo wataendelea kuhamasishana wanafunzi kuona wanaripoti matukio hayo yanapofanyiwa wanafunzi na watoto wengine wote na kutoa wito kwa wazazi kutopuuza pale wanapowapa taarifa kama hizo.
Aidha wazazi na walezi katika maeneo hayo ya mwambe wamepatiwa elimu juu ya kuwalinda watoto wao na changamoto za udhalilishaji wa kijinsia kwa kufuatilia nyenendo zao.
Rehema Mjawiri Omar kutoka dawati la polisi wilaya ya mkoani alisema kuwa suala la muhali limekuwa likichangia kuongezeka kwa vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia kwani [anapotokea suala hilo jamii hukaa na kulimaliza kienyeji badala ya kuliripoti kwa vyombo vya sheria kutokana na muhali.
Naye Hakimu Dhamana katika Wilaya ya Mkoani Suleiman Said Suleiman alisema kesi za udhalilishaji zinazofikishwa mahakamani na kushindwa kutolewa kunasababishwa na kukosekana kwa ushahidi kwa mashahidi walitegemewa kutoa ushahidi hushindwa kufika mahakamani badala ya kukaa vikao na jamii kulimaliza mitaani kwao.
Katika shughuli hiyo wanafunzi hao walijumuika kwenye kongamano la kimichezo kama vile kuruka kamba, kuvutana kamba na kupiga kucheza mpira wa miguu ambapo Mratibu wa Michezo na Utamaduni wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Wilaya ya Mkoani alishughudia na kuwashajihisha wanafunzi hao mbali na masomo yao pia washiriki kwenye michezo mbali mbali.
Save the Children aliwakabidhi kila Skuli mpira mmoja kwa ajili ya wachezaji wa mpira wa miguu na kama 10 za kurukia kwa kila skuli.
Comments
Post a Comment