SHEHA MADUNGU AIOMBA SERIKALI KULIPATIA UFUMBUZI SUALA HILI KUNUSURU WATOTO KUJIINGIZA TENA KATIKA TABIA HATARISHI
- Get link
- X
- Other Apps
NA AMINA AHMED MOH’D - PEMBA.
SHEHA wa Madungu, eneo liliopo katikati ya mji wa Chake Chake,Pemba, ameitaka serikali kuangalia vyema utowaji vibali vya kuendesha michezo ya video ili kudhibiti kuporomoka kwa maadili na tabia za watoto.
MAFUNDA HAMAD RUBEA - SHEHA MADUNGU
Aliishauri serikali kuweka masharti maalum ya uendeshaji wa biashara hiyo na kufuatiliwa utekelezaji wake.
Katika mahojiano maalum, Sheha wa Madungu, Mafunda Hamad Rubea alisema juhudi za kuondoa athari za michezo hio kwa watoto zinazochukuliwa na uongozi kwa kushirikiana na wananchi wa shehia hiyo bado hazipata ufanisi mkubwa.
Alisema wamiliki bado hawajakubali kufunga biashara hiyo kwa madai wanatambulika kisheria kama walipa kodi, lakini ukweli ni kwamba biashara hii inachangia kuharibika kwa watoto kimaadili na kufanyiwa vitendo viovu .
‘’Tunashirikiana na wananchi kuipiga marufuku michezo hii, lakini bado wamiliki wanadai wanafanya kihalali kwa vile wamepewa vibali vya kufanya biashara hii. Kwahivyo, nguvu yetu imekuwa ndogo na tunaiomba serikali iipige marufuku michezzo hii nchi nzima’’, aliongeza.
Alisema michezo hii imepeleka watoto kurubuniwa na kudhalilishwa ili wapate pesa zitazowawezesha kwenda kucheza video.
Bi Mafunda aliwtaka wazazi na walezi kuendelea kushirikiana katika kudhibiti maadili ya watoto na vijana ,ikiwa ni pamoja na kufuatilia mienendo ya watoto ili kuwaepusha kujiingiza katika vitendo viovu vinavyoweza kuwaharibia maisha.
Alisema endapo wazazi wataendelea kumuunga mkono katika kudhibiti michezo hatarishi ikiwemo kama hii ya video, mikusanyiko katika maskani za vijana na uzururaji hovyo mitaani watakutasaidia kudhibiti maadili kwa watoto katika shehia hiyo.
" Wazazi na walezi watoe mashirikiano katika kuendeleza tabia njema kwa watoto na vijana kwani bado vipo viashiria katika baadhi ya mitaa na kwa bahati mbaya baadhi ya wazazi hawatoi mashirikiano mazuri ni vyema kushirikianakwa pamoja katika kujenga taifa la baadae ",alisema.
Baadhi ya wananchi katika shehia hiyo, wakiwemo Abdulahman Muhamed na Jamila Muhamed, walisema juhudi za kudhibiti maadili na kuondoa vitendo viovu zinazofanywa na sheha huyo zinahitaji msaada wa ngazi za juu za serikali
Hii ni pamoja na kutoa maamuzi juu ya kudhibiti na kuondoa hii michezo mitaani.
"Wapo wazazi ndani ya hii shehia wanaotia pamba masikioni juu ya hili, lakini tupo tunaomuunga mkono sheha na mafanikio yameanza kuonekana. Mengine yaliobaki ni serikali kweka nguvu zaidi" Alisema Abdulrahman.
"Baadhi ya wananchi tumekuwa wagumu kutoa mashirikiano, jambo ambalo linalrudisha nyuma jitihada za shehia kudhibiti maadili ipasavyo. Bado hatujashikamana kwani wakati tumejikubalisha kujenga wengine wanabomoa kimya kimya’’, alisema Bi.Jamila.
Katika kudhibiti maadili kwa vijana na watoto ndani ya shehia ya Madungu uongozi pia unawashirikisha viongozi wa dini na waalimu wa skuli na madrasa.
Mitaa inayoogoza kwa michezo hii inayoaribu mwenendo wa watoto katika sheha hio ni Madungu, Fueni na Mtoni.
Mwisho.
| |||
| |||
- Get link
- X
- Other Apps
Comments
Post a Comment