MIAKA MIWILI YA KAZI: TAMWA YAWASILISHA RIPOTI
NA MASSOUD JUMA.
WADAU wa kupinga vitendo vya udhalilishaji Zanzibar, wamekutana kwa pamoja katika ukumbi wa mikutano wa ZURA, kwa ajili ya kusikiliza ripoti iliyowasilishwa na TAMWA ZNZ juu ya utekelezaji wa mradi wa kutumia jukwaa la habari kupinga vitendo vya udhalilishaji.
Akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa bodi ya TAMWA ZNZ Bi Asha Abdi, alisema kuwa mradi huo wa kutumia waandishi na vyombo vya habari kuzuia udhalilishaji ni mradi wa muda mrefu ambao TAMWA ZNZ wanatekeleza kwa mashirikiano makubwa na Shirika la Kitaifa la Maendeleo la Denmark (DANIDA).
Bi Asha aliongeza kuwa lengo la mkutano huo ni kutathmini maendeleo ya mradi kwa muda wa miaka miwili kutoka ulipoanzia mpaka hii Septemba 2023, ambapo ndio mwisho wa utekelezaji wa mradi huo.
“Kwa kweli tulipotoka sipo ambapo tupo hivi sasa, mambo yamebadilika kidogo kutokana na jitihada mbalimbali zinazochukuliwa na serikali pamoja na wadau wengine, tunashukuru jitihada za serikali pia katika kupambana na mambo haya ikiwemo kuanzisha mahakama maalum ya kesi za udhalilishaji”, alisema bi Asha.
Takwimu kutoka Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali inaonesha kuwa matukio hayo yameongezeka kutoka matukio 1,222 mwaka 2021 hadi matukio 1,360 mwaka 2022, ongezeko ambalo ni la matukio 138.
Takwimu hizo zinaonesha kwamba kwenye matukio 1,361 yaliyotokea mwaka 2022, matukio 1,173 yalijumuisha watoto, 185 yalihusu wanawake na matatu yalihusu wanaume. Kwenye matukio 1,173 ya watoto, 889 walikuwa ni wasichana, huku 284 walikuwa ni wavulana.
Akizungumza wakati wa kuwasilisha ripoti ya miaka miwili ya utekelezaji wa mradi huo wa kutumia vyombo vya habari kupinga vitendo vya udhalilishaji, afisa mradi huo Zaina Salum amesema kuwa mradi umewajengea uwezo karibu waandishi wa habari wachanga 10 kutoka Unguja na Pemba, kwa ajili ya kufanya utafiti wa kihabari, kuibua na kufanya ufatiliaji wa vitendo vya udhalilishaji na kuviripoti kupitia vyombo vya habari.
“katika utekelezaji wa mradi huu tuliweza kutengeneza mtandao wa waandishi wachanga 10, ambao tuliwapatia mafunzo maalum ya namna bora ya kuziibua, kuzifanyia utafiti na hatimae kuziripoti katika vyombo vya habari”, alisema Zaina.
Nae mratibu wa TAMWA ZNZ kwa upande wa Pemba, amesema kuwa wanafanya kazi kwa karibu sana na watu wa mtandao wa kupinga udhalilishaji katika ngazi ya shehia ambapo kwa mwaka 2022 ilifuatilia takriban matukio 144 kwa Unguja na Pemba.
Rahma Suleiman ni miongoni mwa wanahabari wachanga waliopatiwa mafunzo hayo ya kaundika habari za kupinga vitendo vya udhalilishaji anaishukuru sana TAMWA ZNZ kwa kumpatia mafunzo hayo kwani yamewasaidia sana kufanya kazi zao kwa ufanisi na kuwajengea ujasiri na kujiamini katika ufuatiliaji wa kesi hizo katika maeneo tofauti ndani ya jamii na katika vyombo vya serikali.
“tulipewa mafunzo ya kuripoti matukio haya kwa usahihi na kuripoti mwendelezo wa kesi zote, tunaishukuru sana TAMWA kwani mafunzo yametujengea ujasiri na pia yametuwezesha kupata tuzo mbalimbali za uandishi habari bora” alisema Rahma.
Mradi huu pia ulisaidia kutoa matibabau na msaada wa kisaikolojia kwa wahanga na familia zao, ambapo kwamwaka 2022 jumla ya familia 80 za wahanga zilipatiwa matibabu na ushauri nasaha ambao uliwasaidia kuwatoa katika dimbwi la kujiona hawafai tena katika jamii.
“kwa kushirikiana na wataalam wa ushauri nasaha, mwaka 2022 tulitoa msaada wa kisaikolojia kwa waathirika wa vitendo hivyo na familia zao 80, na kwa mwaka 2023 waathirika 160 tuliwapa msaada huo wa ushauri nasaha”, alisema Fat-hiya Mussa, mratibu wa TAMWA ZNZ.
Akizungumza kwa niaba ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, muwakilishi kutoka wizara hiyo ndugu Mohd Jabir alisema kuwa TAMWA ZNZ wamekua ni msaada mkubwa kwa wizara na imewasaidia sana kwa kuwapa taarifa za kutosha wakati wizara inafanya tathmini ya utekelezaji wa mpango mkakati wa kitaifa wa kupinga udhalilishaji.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na hakimu kutoka mahkama ya watoto Mheshmiwa Zuwena Mohammed ambae alieleza kuwa changamoto kubwa inayosababisha watoto kuendelea kufanya uhalifu wa vitendo hivi ni kukosekana kwa jela ya watoto hivyo watoto huachiwa huru baada ya wazee wao kuwalipia faida badala ya kupata adhabu kwa kosa wanalolifanya.
“sheria imeelekeza kuwa na vyuo maalum vya kurekebisha sheria vya watoto wanaokinzana na sheria, lakini bado hakuna vituo hivyo na badala yake wanatozwa faini ambayo inalipwa na wazazi, baadae wanarudi kwenye jamii vilevile bila kurekebishwa”, alisema Zuwena.
Dokta Sikujua Omar ni mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Zanzibar katika kitivo cha sheria, amesema kuwa bado kuna changamoto katika sheria, ameshauri kungekua na sheria moja tu ya masuala haya ya udhalilishaji na hivyo ingesaidia kuona ni kwa namna gani tunamlinda mtoto kutokana na sheria hiyo moja.
“tukiwa tunaangalia ni kwa namna gani tutamaliza kesi hizi, ni lazima tuangalie chanzo chake ambacho ni aina ya malezi yetu, tuangalie kama malezi yetu ya sasa yanamlinda mtoto, idadi bado ni kubwa ya kesi za watoto wanaokinzana na sheria”, aliongeza Dokta Sikujua.
Mkutano huo ulimalizika kwa wadau hao kutoka katika Taasisi zote kukubaliana kwa pamoja kuendeleza mapambano ili kumaliza na kutokomeza kabisa vitendo hivi, ili jamii hasa watoto na wasichana wawe salama, pia wamekubaliana kuwa suala hili si la mtu mmoja na ni muhimu kuimarisha ulezi wetu kama wazazi na jamii kwa ujumla. Pia wamekubaliana juu ya umuhimu wa kuwepo kwa marekebisho ya baadhi ya sheria zinazokwaza ama kuipa mianya vitendo hivyo.
Bila shaka kukamilika kwa mradi huo itakua sio mwisho wa mapambano dhidi ya vitendo hivi, kila mtu akitimiza wajibu wake, vitendo hivi vitakwisha kabisa na vitabaki historia hapa katika visiwani kwetu Zanzibar.
Comments
Post a Comment