WADAU WAHIMIZA ELIMU YA SAIKOLOJIA KWA WAHANGA WA VITENDO VYA UDHALILISHAJI


NA, MASSOUD JUMA . 

SUALA la udhalilishaji wa kijinsia limekuwa likiitia doa sana nchi yetu ya Tanzania, khasa kwa upande wa Zanzibar. Vitendo hivi vya udhalilishaji vimeshika kasi na vinaonekana kukithiri na hasa waathirika wakubwa wakiwa ni watoto na wanawake.

Unyanyasaji dhidi ya wanawake na watoto unatajwa kuwa ni jambo la kila siku visiwani hapa, huku asilimia 14 ya wanawake wakiripotiwa kukumbana na vitendo hivi.

Vitendo vya udhalilishaji na ukatili wa kijinsia vimeripotiwa kuendelea kuongezeka visiwani hapa ambapo Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaonesha kuripotiwa kwa matukio 1,222 mwaka 2021 na kuongezeka hadi matukio 1,360 mwaka 2022, ongezeko ambalo ni la matukio 138.

Takwimu hizo zilizotolewa  Januari 2023, zinaonesha kwamba kwenye matukio 1,361 yaliyotokea mwaka 2022, matukio 1,173 yalijumuisha watoto, 185 yalihusu wanawake na matatu yalihusu wanaume ambapo kwenye matukio 1,173 ya watoto, 889 walikuwa ni wasichana, huku 284 walikuwa ni wavulana.


Hii ni idadi kubwa kwa watoto hasa wa kike kufanyiwa vitendo hivi, kwani huwakosesha watoto nguvu ya kujiamini na kutimiza ndoto zao hata katika masuala ya masomo.

Pamoja na takwimu hizo kuonyesha kuwa hali ni mbaya juu ya matukio hayo, lakini pia waathirika wa matukio hayo ya ukatili na udhaliilishaji wa kijinsia wamekuwa wakijiona sio wa thamani katik dunia, huku wengine wakifikiria kujidhuru na hata kufikiria kujiua pindi wanapokumbuka unyama waliofanyiwa.

Baadhi ya wananchi  wa Zanziabr akiwemo Salma Yassin wanaona kuwa ni muhimu kwa wahanga wa vitendo hivi kupatiwa ushauri nasaha ili waweze kuendelea na maisha na kusahau na kufuta maumivu yote ya nyuma.

“Mimi naona kuna umuhimu mkubwa wa waathirika wa vitendo vya udhalilishaji na wazazi wao kupatiwa ushauri nasaha, wengi wao hukata tamaa ya maisha, na wazazi pia huwakatia tamaa watoto wao, hii sio sawa wanahitaji kusaidiwa kisaikolojia ili mtoto aweze kuendelea na maisha mengine”, alisema Salma. 

Wanaharakati wa kupinga vitendo vya udhalilishaji Zanzibar wanasema kuna umuhimu mkubwa kwa mtu aliyepata kadhia ya kudhalilishwa kupata elimu ya utambuzi wa kujijua yeye ni nani, na hiyo itamsaidia kuichukulia changamoto yake kama ni mapito na atajikaza kuendelea na safari ya maisha.

Bi Amina Yusuf ni mwanaharakati wa kupinga vitendo hivi anasema wengi waliodhalilishwa kijinsia  wamekuwa wakipata athari za afya ya akili kutokana na namna ambavyo wamekuwa  wakiishi katika jamii, na jamii inavyowachukulia na kuwanyooshea vidole.

Bi Amina anatoa wito kwa jamii kutowanyanyapaa watu waliokumbwa na kadhia hiyo kwani wanaongezea mawazo na kuwakosesha kujiamini ndani ya jamii.

Suala la ukatili na udhalilishaji wa kijinisia ni miongoni mwa mada ambazo zinaumiza vichwa hapa visiwani znz, ambapo asasi za kiraia na taasisi za serikali na kisiasa zimekuwa zikitoa wito wa kukemea matendo hayo.

Tumezungumza na katibu mkuu wa Chama cha Demokrasia Makini ndugu Hassan Ameir Hassan, ambae ametoa wito kwa wazazi na walezi kujenga utamaduni na tabia ya kukaa na watoto wao ili kujua nyendo zao za kila siku.

Nae Hamad Mohd Ibrahim, katibu mkuu wa chama cha UPDP TAIFA amesisitiza utoaji wa elimu ya kujiepusha na vitendo vya udhalilishaji wa kijnisia kwa watoto ili wawexe kujifahamu na kujiepusha na dalili za kwanza za kuelekea kwenye udhalilishaji.

Serikali kupitia Mkurugezi wa Idara ya Ustawi wa Jamii Zanzibar, ndugu Hassan Ibrahim Suleiman  amekiri kuweko kwa umuhimu wa waathirika wa vitendo vya dhalilishaj na ukatili wa kijinsia kupewa elimu ya saikolojia ili kuondoa maumivu ya kihisia yanayoweza kusababisha hofu pamoja na kuwa na aibu ya kila wakati inayosababisha kutojiamini.

“Nawaasa wanasaikolojia kuanzisha klabu mbalimbali za ushauri nasaha kwa ajili ya kutoa ushauri nasaha katika ngazi za wilaya, shehia na mkoa ambazo zitatoa elimu kuhusu athari za matendo haya na namna ya kujikinga” alisema Hassan.

Ni vizuri kuwa na kituo maalum kwa ajili ya kuwasaidia wahanga wa vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia, kwani itawasaidia kupunguza angalau maumivu na kuwafanya waendelee mbele na maisha. Jamii pia ijitahidi kuwaunga mkono na kuwapitisha katika kipindi hicho kigumu kwa kuwapa moyo na ushauri unaofaa.

Comments

Popular posts from this blog

BARABARA 19 KUJENGWA KWA KIWANGO CHA LAMI PEMBA KUKAMILIKA DISEMBA 2024.

WAZAZI ZIDISHENI KUFUATILIA NYENENDO ZA WATOTO HUSUSAN NI VIJANA .

UONGOZI WA WILAYA CHAKE CHAKE KFHI WAPONGEZA JUHUDI