UTAMADUNI WA KUSAMEHEANA WATAJWA KUWA KICHOCHEO CHA VITENDO VYA UDHALILISHAJI TANZANIA.


Na Asha Ahmed

Maumivu huwa makubwa sana kwa wahanga na wazee wa wahanga wa vitendo vya udhalilishaji, watoto ambao wanaharibiwa kwa kubakwa na kulawitiwa, lakini mara nyingi huonekana baadhi ya familia kuacha kufuatilia mwenendo wa kesi zao na wengine kuzifuta kabisa. 

Wadau wa kupinga vitendo vya udhalilishaji wanasema kuwa utamaduni wa kusameheana na kuoneana muhali ndio husababisha zaidi kutoendelea kwa kesi na hivyo watuhumiwa kuendelea kukaa mitaani na kufanya vitendo vya udhalilishaji kwa watu wengiine.


Vitendo vya ukatili dhidi ya watoto, hususan ubakaji na ulawiti, vimekua ni kama janga la taifa hapa nchini, hali ambayo imeendelea kuumiza vichwa vya watendaji wa Serikali, mashirika yasiyo ya Kiserikali (NGOs), taasisi za dini na wadau wengine juu ya namna gani vitendo hivyo vinaweza kukomeshwa.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, kati ya mwaka 2017 mpaka Mei 2022, Tanzania ilirikodi jumla ya matukio 75,787 ya ukatili wa dhidi ya watoto yaliyojumuisha vitendo vya ulawiti na ubakaji.

Katika takwimu hizo mchanganuo unaonesha kwamba kati ya Januari na Mei 2022, jumla ya matukio ya kubaka 2,445 yamefanyika, matukio 717 ni ya kumpa mimba mwanafunzi na kulawiti ni matukio 553.

Takwimu kutoka Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaonesha matukio hayo yameongezeka kutoka matukio 1,222 mwaka 2021 hadi matukio 1,360 mwaka 2022, ongezeko ambalo ni la matukio 138.

Hii ina maana kwamba ukatili wa kubaka, kumpa mimba mwanafunzi na kulawiti bado ni changamoto kubwa nchini Tanzania, hali inayoita jitihada za pamoja kupambana na vitendo hivyo. Kuchukuliwa kwa hatua za kisheria dhidi ya watu wanaobainika kufanya vitendo hivyo kumetajwa kama moja ya njia imara ya kuvitokomeza.

Utafiti wa mwaka 2017 uliofanywa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Watoto (UNICEF) unabainisha kwamba kesi nyingi za ukatili wa kingono dhidi ya watoto humalizwa katika mazingira ya nyumbani, ambapo mara nyingi wazazi hushiriki kwenye michakato hiyo bila ya hata kuwashirikisha watoto wenyewe.

Afisa ustawi wa jamii kutoka ofisi ya , Mkuu wa Wilaya ya Mjini ndugu Mithle Mussa amesema kuwa suala la muhali linachangia kwa kiasi kikubwa kuendelea kwa vitendo hivi, kwani watuhumiwa huachiwa huru kutokana na kuonekana ni majirani au ndugu wa karibu, jambo ambalo huwapelekea kuendelea kutekeleza vitendo vyao vichafu kwa watoto wengine.

Nayo Ripoti ya Haki za Binadamu kwa Mwaka 2022 iliyotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) mapema mwaka 2023 ilitaja “utamaduni wa kusameheana” na “kuficha aibu ya familia” kama moja ya sababu zinazochochea vitendo vya ukatili dhidi ya watoto Tanzania.

Kuna sababu mbalimbali ambazo zinachangia kuongezeka kwa vitendo hivi, ikiwemo muhali, hongo, ukakasi wa sharia na mengineyo.

Mohammed Saleh Idd ni Wakili wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka amesema baadhi ya sheria zinazosimamia kesi za udhalilishaji bado zina ukakasi kwani zipo sheria ambazo zinalazimisha  kuthibitisha tukio la ubakaji au ulawiti kwa kukagua sehemu za siri, jambo ambalo linaweza kuzua taharuki kwa muhanga, hivyo kupelekea kuachana na kesi na mtuhumiwa kutokutiwa hatiani na hivyo kuendelea na vitendo vichafu vya udhalilishaji.

Changamoto nyengine inayotajwa ni watu kuwa na hofu na aibu, baadhi ya familia hufuta kesi kutokana na kuahidiwa malipo ya fedha na mshukiwa au kutokana na hofu waliyonayo juu ya vyombo vya sheria na upatikanaji wa haki nchini.

Baadhi ya wadau wameelekeza lawama kwa Jeshi la Polisi, wakisema kwamba taasisi hiyo imekuwa inawaruhusu wazazi kumaliza kienyeji kesi hizo za ulawiti na ubakaji. 

Jeshi la polisi limetoa ufafanuzi wa madai hayo likisema kuwa kesi pekee inayoshindwa kwenda mbele zaidi baada ya kufika Kituo cha Polisi ni ile ambayo ushahidi wake uko dhaifu, na sio sababu ya hongo ama kujuana.

Mkurugenzi wa  TAMWA –ZNZ, Dokta Mzuri Issa amewaasa wazazi, walezi, taasisi, Serikali  na Jamii kwa ujumla kushirikiana na kila mmoja kutimiza majukumu na wajibu wake ili kuhakikisha kuwa vitendo hivi vya udhalilishaji vinamalizwa kwa wahalifu kupatiwa hukumu zinazowastahili, pia amewataka wanajamii kuondosha kabisa fikra za kupunguza umri wa mtoto kwani hiyo ndio itazidi kumsababishia matatizo mtoto badala ya kumsaidia.


Comments

Popular posts from this blog

BARABARA 19 KUJENGWA KWA KIWANGO CHA LAMI PEMBA KUKAMILIKA DISEMBA 2024.

WAZAZI ZIDISHENI KUFUATILIA NYENENDO ZA WATOTO HUSUSAN NI VIJANA .

UONGOZI WA WILAYA CHAKE CHAKE KFHI WAPONGEZA JUHUDI