WADAU WAHIMIZA UTEKELEZAJI WA SERA NA SHERIA ZINAZOSIMAMIA MASUALA YA UDHALILISHAJI


Na Asha Ahmed, Unguja.

Katika muendelezo wa harakati za Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania TAMWA ZNZ kupambana na kesi za udhalilishaji Zanzibar, kimekuwakutanisha wadau mbalimbali kwa ajili ya kujadili utekelezaji wa sera na sheria zinazosimamia masuala ya udhalilishaji Zanzibar.

Wadau hao ni pamoja na mahakimu kutoka mahakama maalum ya udhalilishaji, maafisa kutoka ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka, wanasheria, Jeshi la Polisi, msaidizi kamishna kutoka chuo cha mafunzo, watoa msaada wa kisheria, maafisa kutoka asasi mbalimbali za kiraia na serikali pamoja na waandishi wa habari.

Lengo kuu la mkutano huo lilikua ni kujadili sera na sheria na kuangalia ni kwa namna gani zinatekelezwa katika kupambana na vita ya udhalilishaji hapa visiwani Zanzibar, ambapo wadau hao walisikitishwa sana kwa kuwepo na sera na sheria nyingi na madhubuti lakini zisizotekelezwa jambo ambalo linachangia kuongezeka kwa vitendo vya udhalilishaji.

Mratibu wa TAMWA ZNZ kwa upande wa Pemba Fathiya Mussa amesema wameona ipo haja ya kuitisha mkutano huo wa wadau kwa ajil ya kujadili na kuzifahamu sera na sheria ambazo zinakwamisha harakati za kupinga vitendo hivi vya udhalilishaji hapa Zanzibar.

“Tumekutana rasmi hapa ili kuangalia ni kwa namna gani sera na sheria zetu zinafanya kazi katika kupunguza vitendo hivi, matukio haya ya udhalilishaji kuendelea kuyasikia kila siku ni jambo linaloumiza kichwa sana” alisema.

Katika ripoti za takwimu zinazotolewa na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar inaonesha ongezeko la kesi hizi ambapo kwa mwaka 2022 jumla ya matukio 1360 yameripotiwa ambayo ni sawa na ongezeko la matukio 138 kutoka katika matukio 1222 yaliyoripotiwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita (2021).

Katika mkutano huo alikuwepo pia Dokta Sikujua Omar ambae ni mkufunzi kutoka katika Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) ambae aliwasilisha mada kuhusiana na sera mbali mbali ambazo kwa namna moja ama nyengine zinahusiana katika kupinga vitendo vya udhalilishaji, miongoni mwa sera zilizowasilishwa ni pamoja na sera ya watoa huduma ya msaada wa kisheria, sera ya utamaduni wa mzanzibari, sera ya maendeleo ya vijana, sera ya watu wenye ulemavu na nyenginezo.

Dokta Sikujua alihoji wadau kuwa sera zote hizo zipo kwa ajili ya kumlinda mtoto na makundi maalum lakini je zinatekelezwa kwa ukubwa gani katika kufikia dhumuni lake hilo? huku akisisitiza kuwa ni muhimu kwa wadau wote wanaoungana kupinga masuala haya kuzijua na kuzifahamu sera hizi ili iwe rahisi kuhimiza utekelezaji wake.

Afisa kutoka katika ofisi ya mkurugenzi wa Mashtaka Mohammed Saleh akiwasilisha mada kuhusiana na sheria mbalimbali alionesha baadhi ya madhaifu ambayo huwa yanachangia kukwama kwa kesi za udhalilishaji huku akiitolea mfano sheria ya ushahidi ambayo inamtaka mhanga kukaguliwa sehemu za siri ili kuthibitisha kutokea kwa tukio, jambo ambalo huzua taharuki kwa wahanga.

Akichangia mada katika mkutano huo Hakimu kutoka mahakama ya Mkoa Vuga Khamis Ali amesema ipo haja pia ya kubadili baadhi ya sheria ambazo zimeshapitwa na wakati ili kuendana na wakati huku akitolea mfano sheria ya elimu

Nae hakimu Nayla kutoka katika mahakama maalum ya kesi za udhalilishaji ametoa wito kwa walimu wa maskuli kuacha kuzificha kesi hizo badala yake kusaidia kuziripoti ili wahanga wapate haki yao.

“Kama kuna walimu ambao wanaficha kesi hizi ni bora kubadilika, na hawa walimu wa ushauri nasaha wanatakiwa kuzidisha juhudi za kuripoti kwani matendo mengi yanayotokea mashuleni hufichwa” alisema

Afisa msimamizi wa miradi ya kupambana na udhalilishaji kutoka TAMWA ZNZ Zaina Salum amesema ipo haja kwa mahakama kuanza kutumia ushahidi wa kielektroniki kwani ni wa kudumu na husaidia sana kuwapunguzia mzigo wahanga.

Zaina aliongeza kuwa kwa sasa kuna wimbi kubwa la watoto wanaotelekezwa jambo ambalo huchangia kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa kesi hizi za watoto wanaokinzana na sheria hivyo ni jukumu la wadau pia kuangalia ni kwa namna gani watazuia masuala haya ya utelekezaji wa watoto.

Mkutano huo ulifungwa kwa maazimio ya wadau wote kuwa ni lazima kuhimiza utekelezaji wa sera na kubadilishwa kwa sheria zote  ambazo zimepitwa na wakati na zile ambazo zinatoa mwanya kwa wahalifu kuutumia na kuendeleza matukio haya. 


Comments

Popular posts from this blog

BARABARA 19 KUJENGWA KWA KIWANGO CHA LAMI PEMBA KUKAMILIKA DISEMBA 2024.

WAZAZI ZIDISHENI KUFUATILIA NYENENDO ZA WATOTO HUSUSAN NI VIJANA .

UONGOZI WA WILAYA CHAKE CHAKE KFHI WAPONGEZA JUHUDI