YAJUE USIYOYAJUA KUHUSU ALIEKUWA RAIS, CHUO CHA KUMBUKUMBU YA MWALIMU NYERERE KAMPASI YA KARUME .


Na Riziki Abdalla, Unguja.

 TUNAPOZUNGUMZIAharakati za mwanamke na uongozi hatumaanishi tu katika nyanja za siasa ama kiuchumi bali pia katika nyanja za kitaaluma ikiwemo shule za msingi, sekondari na hata vyuo vikuu.

 Na leo mwandishi wa makala hii anaeleza nadharia finyu zilizozunguka vichwa vya watu wengi wakiwemo wanafunzi wa vyuo vikuu wakidhani ya kuwa mwanamke hawezi kuwa kiongozi katika nafasi ya uraisi eti tu kwa jinsia yake. 

Na je? Unajua nadharia hii ilifutwa baada ya chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kampasi ya karume Zanzibar kupata raisi wa kwanza mwanamke na kuleta maendeleo chanya hususani kwa wanawake wenziwe?


 “Nilikumbana na kebehi nyingi sana kipindi ambacho nilitia nia ya kugombania nafasi ya uraisi katika chuo changu lakini sikukata tamaa na nilibaki na msimamo wangu’’ alisema Mariam Khamis Abdulla ambae aliongoza chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Zanzibar kwa nafasi ya urais kwa muda wa mwaka mmoja kuanzia 2020 – 2021.

Moja ya sababu zilizomfanya Mariam kugombea nafasi ya uraisi katika chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ni hamasa aliyoipata kutoka kwa wanafunzi wenziwe pamoja na baba ake mzazi kwa kumkubalia ombi lake la kutaka kuwa raisi wa chuo hicho. “hamasa kubwa na mashirikiano kutoka kwa wanafunzi wenzngu wa chuoni hususani wanawake pamoja na ridhaa ya baba angu mzazi ndio kilichonipa nguvu ya kuamini kuwa naweza kuongoza nafasi hii” alisema Mariam.


Pamoja na uwezo mkubwa aliouonesha Mariam katika kipindi chake cha uraisi na kufanya mambo mengi mazuri kwa wanawake wenziwe ni kuweza kuanzisha dawati la jinsia ambalo limekuwa na mchango mkubwa wa kutatua matatizo ya wanawake katika mazingira ya chuo.

 “tulianzisha dawati la kijinsia baada ya kupatiwa mafunzo na TAMWA kwa lengo la kuweza kusaidiana kama wanawake pale tunapofikwa na changamoto ya aina yeyote” aliongeza kwa kusema Mariam.

Na kwa vile matatizo na changamoto za wanawake hutatuliwa na mwanamke mwenzake, Mariam Khamis Abdulla aliweza kuanzisha ipatikanaji wa taulo za kike katika chuo chake bila ya gharama yeyote ile ambapo hapo awali haukuwepo utaraibu huo “tulihakikisha taulo za kike zinapatikana tena bure kwa wanafunzi wa kike kwa lengo la kuwafanya wawe huru wanapopata dharura zao ambapo hapo mwanzo walikuwa wakinunua kwa pesa zao wenyewe” alisema Mariam.

BAADHI YA WANAFUNZI WAELEZA FAIDA WALIZOPATA KATIKA UONGOZI WA MARIAM.

    Asya Makame Haji ambae ni mwanafunzi wa fani ya Ualimu katika chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere alieleza kuwa “tumefaidika mengi kupitia uongozi wa dada etu Mariam kwani tumeweza kupata sauti na sehemu ya kusemea matatizo yetu na pia wanafunzi wengine wanawake wamepata hamasa ya kugombania nafasi za uongozi ndani ya chuo baada ya kuona uwezo wake”

Nae John Makulanga ambae ni mwanafunzi wa fani ya maendeleo ya jamii katika chuo hicho aliongeza kwa kusema “wanawake ni wakati wao sasa wa kuonesha uwezo wao kama aliotuonesha mwanadada Mariam katika uongozi wake na pia hakuwa ni mtu wa kuleta matabaka eti kwa kuwa yeye ni mwanamke” pia alimalizia kwa kusema “tungelitamani hata wanawake wengine nao wangepata nafasi hii ya uraisi na kutuletea maendeleo mazuri kama aliyotuachia dada etu Mariam.


Pia Khudhaimat Kheir Salum ambae ni Makamo Mwenyekiti wa shirikisho la vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu Zanzibar (ZAHILFE) pia alikuwa ni Mwenyekiti wa kamati ya chaguzi na maadili ZAHILFE alieleza mchango alioleta Mariam katika kipindi chake cha uongozi kwa kusema kuwa “ nisiwe mkosefu wa fadhila katika kumtolea mfano hai popote ntaposimama katika uongozi wake kwani ameweza kuleta hamasa hata kwa vyuo vyengine kuwa na raisi wanawake ikiwemo chuo cha Glorious na Emperial Collage”


Kwa kumalizia Mariam Khamis Abdulla aliwashauri wanafunzi wenziwe wa kike ambao wana kengo la kugombania nafasi za uongozi na kuwa viongozi bora kuwa “niwasihi tu wanawake wenzangu wasimamie nia zao za  kutaka kuwa viongozi bora na wasikubali kukatishwa tamaa kwa hali yeyote ile bila kuvunja heshima zao”

 

 



Comments

Popular posts from this blog

BARABARA 19 KUJENGWA KWA KIWANGO CHA LAMI PEMBA KUKAMILIKA DISEMBA 2024.

WAZAZI ZIDISHENI KUFUATILIA NYENENDO ZA WATOTO HUSUSAN NI VIJANA .

UONGOZI WA WILAYA CHAKE CHAKE KFHI WAPONGEZA JUHUDI