USAWA WA KIJINSIA KWENYE VYOMBO VYA MAAMUZI NDIO NYENZO MAMA YA WANAWAKE NA UONGOZI.
NA, RIZIKI ABDALLA- UNGUJA
"MOJA ya nyenzo mama ya kuwawezesha wanawake katika kufikia asilimia 50 kwa 50 katika harakati za uongozi ni kuwepo na usawa wa kijinsia kwenye vyombo vya maamuzi". Amesema hayo ndugu Khamis Ali Rashid ambae ni Mratibu wa mradi wa kuwainua wanawake kiuongozi (SWIL- Strengthen Women In Leadership) kwa upande wa ZAFELA katika muendelezo wa kuwajengea uwezo wanawake katika masuala ya kiuongozi uliofanyika katika ukumbi wa ZSSF Kariakoo Mjini Zanzibar.
Muendelezo huo umewakutanisha wanawake mbalimbali wa vyama vya siasa vya Zanzibar ikiwemo CCM, CUF, CHADEMA, UDP, ACT WAZALENDO na vyenginevyo kwa lengo la kujadili mikakati na mbinu mbalimbali za kuweka mazingira rafiki kwa wanawake kushiriki kwenye masuala ya uongozi na demokrasia ili kuweza kufikia malengo yao pamoja na kutathmini changamoto wanazokumbana nazo katika harakati za kujipanga kwenye kuwania nafasi za uongozi na jinsi ya kuzitatua changamoto hizo. "Ni vyema tukajadili kwa pamoja changamoto tunazokumbana nazo ili kujuwa wapi turekebishe na wapi tuekane sawa kwenye harakati zetu za uongozi" alisema ndugu Maryam Ame ambae ni Mratibu wa Mradi wa SWIL kwa upande TAMWA.
Pia mkutano huo umewajumuisha viongozi mbalimbali kutoka vyama vya siasa vya Zanzibar kwa lengo la kuwapa mafunzo na nasaha juu ya masuala ya kuwawezesha wanawake hao kiuongozi na kutoa utatuzi wa zile changamoto wanazopitia katika kuwania nafasi hizo. Miongoni mwa viongozi waliohudhuria ni Salum Mwalimu Juma ambae ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Zanzibar " kwa morali hii tulioiona kutoka kwenu tunaimani ya kuwa hadi kufika 2025 hamasa kubwa ya wanawake katika kugombea nafasi za uongozi itaongozeka kwa asilimia kubwa" pia aliongeza kwa kusema " sisi kama CHADEMA tupo tayari kuwasaidia na kuwasimamia kwa kila hatua mtayotaka kupitia ili kuwania nafasi hizo ikiwa tu utakidhi vigezo vya kuwania nafasi hizo"
Nae ndugu Khamis Mbeto Khamis ambae ni Katibu wa Kamati maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar amesema "si Chama Cha Mapinduzi tu bali hata vyama vyengine vya siasa vya Zanzibar vihakikishe kuwa wanawake wanapatiwa nafasi za uongozi kuanzia ngazi ya Mwenyekiti na nyenginezo ikiwa uwezo wanao" pia alimalizia kwa kusema " ili kupata viongozi waliowiva katika kuongoza ni lazima waandaliwe mapema kwa misingi iliyo imara kama hivi munavofanya ZAFELA, TAMWA na PEGAO"Miongoni mwa wanufaika wa mradi huo ambao walipatiwa mafunzo nao wanaeleza kuwa "wanawake tusijifiche ni lazima tujitokeze kuonesha kuwa tunaweza na changamoto tunazopitia basi tuzifanye kuwa fursa ya kupiga hatua nyengine mbele" alisema Zainab Saleh Salum ambae ni Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Zanzibar. Nae Khayam Mustafa Yakuti ambae ni Mwenyekiti wa UVCCM Jimbo la Malindi aliongeza kwa kusema "hadi hatua hii tuliyofikia hakuna sababu ya kutufanya sisi wanawake kutopeperusha bendera za vyama vyetu katika marimba yetu ifikapo 2025 ikiwa tufata vyema taratibu na kanuni za katiba za vyama vyetu tunavyovipigania".
Pia Bi Naima Salum Hamad kutoka chama cha UDP ambae aliwahi kugombania nafasi ya Spika wa Baraza La Wawakilishi Zanzibar 2020 alimalizia kwa kusema kuwa "kama wanawake ni lazima tushirikiane kwa pamoja katika kuleta maendeleo ya nchi yetu kupitia vyama vyetu vya siasa bila kujali mila wala itikadi zetu katika uongozi, kwani maendeleo ya wote huletwa na wote".
Comments
Post a Comment