UONGOZI WA DR SAMIA ULIVYOCHANGIA KUTATUA CHANGAMOTO 11 ZA MUUNGANO.AMBAZO ZILIKUWA SUGU



Ushirikiano wa kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar umefanikiwa kuleta mafanikio makubwa katika maeneo tofauti ikiwemo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Katika kipindi chote cha ushirikiano huo, serikali hizo zimefanikiwa kusimamia utekelezaji wa mambo ya Muungano kwa ufanisi mkubwa na kwamba hatua hiyo inathibitishwa na mafanikio yaliopatikana kwa kipindi kifupi cha serikali ya awamu ya sita baada ya kuingia kwa uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Mwenyekiti wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Najma Murtaza Giga ambaye ni Mbunge wa viti maalum kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) akiwa kama kiongozi mwanamke ambaye anayeongoza vikao vya Bunge katika muhimili huo anajitokeza kuonyesha hisia zake zenye imani na uwezo mkubwa wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika eneo la mafanikio la Muungano.

Giga ambaye kwa sasa anatumikia kwa kipindi cha pili tangu Bunge la1,  anasema Rais Samia ni mwanamke wa kwanza kuiongoza Tanzania baada ya kutokea kwa kifo cha aliyekuwa Rais wa awamu ya tano Hayati Dk.John Magufuli na kwamba ameonyesha weledi mkubwa katika kusimamia na kuzitatua changamoto za Muungano.

Katika maelezo yake anasema ana imani na uongozi wa Rais Samia kutokana na kuwa ni mzoefu katika ngazi mbalimbali za uongozi ikiwemo aliwahi kuwa Waziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na baadaye alikuwa Mbunge na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Muungano.

"Mbali na hilo pia aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba na baadaye akapata nafasi ya kuwa mgombea mwenza nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivyo mimi sina shaka kutokana na kuwa na uwezo mkubwa katika uongozi,"anasema.


Anasema Rais Samia ameonyesha uwezo mkubwa katika eneo hilo la muungano baada ya kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wake kufanikisha kutafutia ufumbuzi  changamoto  za muungano na kufanikiwa kuzitatua 11 na kubakia saba kati ya 18.

"Tokea mwaka 2006 ambapo kamati ya kujadili hoja zilizoibua changamoto za muungano kuanza rasmi kwa kipindi cha miaka 14 hadi kufikia Oktoba 2020 ni changamoto saba kati ya 25 zilizoibuliwa na kupatiwa ufumbuzi lakini kwa kipindi hichi cha Rais Samia changamoto 11 zimetatuliwa kati ya 18”, anasema.

MAENEO 11 YALIYOTATULIWA KWA KIPINDI CHA DKT SAMIA

Giga anayataja maeneo 11 ambayo ni miongoni mwa changamoto zilizokuwa zinapigiwa makelele kwa kipindi cha muda mrefu ambazo ndani ya kipindi cha muda mfupi Amezitatua.

Maeneo hayo ni uvuvi kwenye ukanda wa uchumi wa bahari kuu, mgawanyo wa mapato yatokanayo na misaada ya kibajeti, mkataba wa fedha za miradi wa ukarabati hospitali kuu ya Mnazi Mmoja,mkataba wa fedha za mradi wa ujenzi wa barabara kutoka Chake Chake hadi Wete.

Eneo jengine ni mkataba wa fedha za ujenzi wa bandari ya Mpigaduri, uwiano wa ajira kwa watumishi wanzanzibar katika taasisi za Muungano, mapato yanayokusanywa na Idara ya Uhamiaji kwa upande wa Zanzibar.

Maeneo mengine ni uingizwaji wa bidhaa za maziwa Tanzania Bara kutoka Zanzibar, uteuzi wa Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Rufaa za kodi, Mjumbe wa Bodi ya Bima ya Amana kutoka Zanzibar pamoja na mabadaliko ya usimamizi wa makusanyo ya kodi kwenye huduma za simu na kwamba kwa sasa yapo chini ya Bodi ya Mapato Zanzibar(ZRA).

Giga anasema kwa changamoto zilizobakia ana imani kuwa katika uongozi wa Rais Samia zitatafutiwa ufumbuzi licha ya kuwa anaelewa kuwa nyngine ni za muda mrefu.




CHANGAMOTO ZA MUDA MREFU

Anasema miongoni mwa changamoto ambazo ni za muda mrefu ni mgawanyo wa mapato yatokanayo na hisa ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika bodi ya sarafu ya Afrika Mashariki na faida kutoka Benki Kuu.

Nyengine ni Tume ya pamoja ya fedha ili iwe akaunti ya pamoja  zitokanazo na Muungano na kwamba kuna haja ya watanzania kutambua kuwa changamoto katika Muungano zitaendelea kuibuka.

"Tunachotakiwa sisi kama watanzania ni kumuunga mkono Rais Samia kutokana na dhamira yake njema juu ya Muungano na namna alivyothibitisha kuwa yeye ni muumini wa muungano kwa namna alivyozipatia ufumbuzi changamoto 11 kwa kipindi cha muda mfupi,"anasema.

Hata hivyo anaeleza kwamba kila mmoja ana wajibu na uthubutu wa kuyaelezea yale mazuri ambayo yanafanywa na rais Samia katika uongozi wake, hususan katika hili suala la kudumisha Muungano.

Kudumisha Muungano sio tu kwa kuona wananchi wanashirikiana kwa hali na mali bali ni pamoja na kupata fursa zote ambazo zinatokana na Muungano wenyewe.

Ni imani yangu kwamba katika uongozi wa Rais Samia hakuna jambo ambalo litashindikana na kila mwananchi anaona namna alivyokuwa kiongozi bora na wa mfano.

Nae kijana wa kutoka UVCCM jimbo la Malindi ndugu Khayam Mustafa anasema jambo lolote la mama Samia ni lazima waliunge mkono na linakuwa ni la kwao wote kwani mama ndie kila kitu katika familia.

“Sisi ni vijana wa mama, na kila jambo lake lazima tuwe nae bega kwa bega kumuunga mkono kwani yeye ndio kila kitu na ni mtegemezi wetu katika kuliletea maendeleo taifa hili”.Anasema Khayyam.

Bi Najma anamalizia kwa kusema kuwa  ni wajibu wa kila mwananchi kuhakikisha anayatunza na kuyathamini maendeleo ambayo yamewekwa kwa ajili yetu na vizazi vijavyo ili tuwe na maendeleo endelevu ndani ya nchi yetu.

Comments

Popular posts from this blog

BARABARA 19 KUJENGWA KWA KIWANGO CHA LAMI PEMBA KUKAMILIKA DISEMBA 2024.

WAZAZI ZIDISHENI KUFUATILIA NYENENDO ZA WATOTO HUSUSAN NI VIJANA .

UONGOZI WA WILAYA CHAKE CHAKE KFHI WAPONGEZA JUHUDI